Wednesday, July 22, 2009

Pinda kupindisha kanuni za Uchaguzi wa Vitongoji, Vijiji na Mitaa?

Pinda kupindisha kanuni za Uchaguzi wa Vitongoji, Vijiji na Mitaa?

Na John Mnyika

Katika mchezo wowote haiyumkiniki refa kuwa mchezaji wa moja ya timu zinazoshindana. Wala haifikiriki wakati huo huo refa huyo huyo akawa kocha, mchezaji na mtungaji wa kanuni za mchezo. Lakini maajabu hayo ni jambo la kawaida katika sheria zetu kuhusu chaguzi za vitongoji, vijiji na mitaa.

Chini ya sheria zetu, kanuni za chaguzi hizo hutungwa na Waziri mwenye dhamana ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI). Na kwa mujibu wa muundo wa sasa wa utawala wa Tanzania pamoja na kuwa na waziri wa nchi anayehusika na TAMISEMI, mwisho wa siku mwenye dhamana kamili ya “Wizara” hii ni Waziri Mkuu, ambaye kwa sasa ni Mheshimiwa Mizengo Pinda.

Izingatiwe kuwa mfumo wa utawala wa nchi yetu unaanzia katika vitongoji, vijiji na mitaa ambayo ina mamlaka kadhaa ya kiutendaji na kimaamuzi.

Uchaguzi wa ngazi hii umekuwa ukifanyika mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu hivyo hutumika kama msingi wa vyama vya siasa katika uchaguzi mkuu na kuandaa mfumo wa chama kutawala kuanzia ngazi ya chini.

Ama kwa hakika Waziri Mkuu yuko katika majaribu makubwa mwezi huu wakati ambapo watanzania wanasubiri mwezi ujao wa Agosti atangaze rasmi katika gazeti la serikali kanuni za uchaguzi wa vitongoji, vijiji na mitaa. Hii ni kwa sababu kwa mujibu wa sheria, kanuni hizi kwa sasa zinatungwa na Waziri mwenye dhamana ya tawala za mikaoa na serikali za mitaa.

Mtihani huu unakuwa mgumu kwa kuwa miezi michache iliyopita mnamo tarehe 20 Februari 2009, wadau mbalimbali ikiwemo ofisi yake, vyama vya siasa, asasi za kiraia na msajili wa vyama vya siasa walifikia makubaliano kuhusu masuala ambayo yanapaswa kuingizwa kwenye kanuni husika.

Wahenga walisema kinyozi hajinyoi; lakini hapa Waziri Mkuu Pinda amepewa mtihani wa kujinyoa kwa kupewa jukumu la kutunga kanuni za uchaguzi ambazo yeye na chama chake ni sehemu ya washiriki.

Wadau wanasubiri kuona kama atatekeleza makubaliano ya wadau na kutunga kanuni zenye kusimamia misingi ya uchaguzi huru na haki. Ama Waziri Mizengo atafanya mizengwe na kutunga kanuni za uchaguzi zisizoweka uwanja sawa wa kisiasa na hatimaye kuleta uchafuzi badala ya uchaguzi?

Kujiuliza huku kwa wadau kunasababishwa na kumbukumbu za mwaka 2004, ambapo kama ilivyo sasa kanuni za uchaguzi wa vitongoji, vijiji na mitaa zilitungwa na Waziri mwenye dhamana badala ya chombo huru cha kusimamia uchaguzi mathalani tume ya uchaguzi.

Mwanya huu wa kisheria wa mchezaji kujitungia mwenyewe kanuni za mchezo ulifanya kanuni hizo kutungwa kupendelea chama kinachotawala kwa kuweka mianya ya hujuma za kiuchaguzi. Matokeo yake ni uchaguzi uliopita wa vitongoji, vijiji na mitaa kutokuwa huru na haki kutokana na mapungufu mengi ambayo hata serikali yenyewe iliyakiri.

Mathalani upigaji kura kutokuwa wa siri, fujo katika mikutano ya uchaguzi, matayarisho kuwa hafifu, kuinguliwa na maafisa na watendaji wa kata na vijiji ambao walifikia hatua ya kuwatisha wananchi na kutotoa taarifa za muhimu za uchaguzi, kukosekana kwa daftari la wapiga kura na uchaguzi kusimamiwa na chombo kisicho huru cha kiserikali moja kwa moja(Wizara ya TAMISEMI).

Wakati mchakato wa uchaguzi huo ukiendelea vyama vya upinzani vikaenda mahakamani, baadhi ya taratibu za uchaguzi huo zikazuiwa lakini uchaguzi wenyewe haukuzuiwa. Mahakama ikaamua uchaguzi uendelee wakati kesi ya msingi inaendelea kusikilizwa kwa maelezo kuwa serikali tayari ilishaingia gharama za maandalizi ya uchaguzi!

Kutokana na mapungufu hayo CCM ilishinda kwa asilimia 96 na kupata mtaji haramu wa kisiasa ambao ilianza nao kama hujuma katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 na kufanya uwanja wa ushindani wa kisiasa usiwe sawa. Na hivyo, CCM ikashinda kwa takribani asilimia 80 katika uchaguzi mkuu mwaka mmoja baadaye.

Ilitarajiwa kwamba marekebisho ya haraka yangefanyika, hata hivyo hakuna hatua za maana zilizochukuliwa kati ya mwaka 2005 mpaka 2008. Kesi iliyofunguliwa na vyama vya upinzani mwaka 2004 mpaka sasa bado ni kizungumkuti. Kwa upande mwingine, Serikali ilikuwa ikiitisha mikutano na vyama na kuiahirisha bila maamuzi ya msingi kufikiwa kuhusu marekebisho yanayostahili kufanywa katika sheria na kanuni zinazosimamia chaguzi husika. Mithili ya mbinu ya timu iliyoshinda kupoteza muda ili mpira umalizike; lakini kwa kuwa refa ni kocha mchezaji, hakukuwa na wa kupuliza filimbi wala kutoa kadi!

Mwaka 2009, mwezi Februari ndipo serikali imesaini makubaliano na wadau kuhusu uchaguzi huu. Kwa kisingizio cha ufinyu wa muda, masuala ya msingi yaliyopaswa kufanyiwa marekebisho mengi hayapo kama sehemu ya makubaliano hayo. Kwa mara nyingine tena, serikali imechelewesha muda na baadaye kutumia kisingizio cha muda kukwepa kufanya mabadiliko ya msingi ya kisheria ya kuhakikisha uchaguzi huu unakuwa huru na wa haki.

Shabaha ya makala hii ni kuibua mjadala wa kukumbusha makubaliano haya ili wadau waweze kufuatilia kwa karibu kuhakikisha kwamba walau makubaliano hayo yanazingatiwa na Waziri Mkuu Pinda katika kutunga kanuni.

Kama mchakato wa utungaji wa kanuni utaendelea kufanyika kimya kimya bila rasimu ya kanuni kupelekwa kwa wadau ikiwemo vyama vya siasa kupitiwa kabla ya kuchapwa kwenye gazeti la serikali makubaliano hayo yanaweza kupindishwa.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo; yafuatayo hayatafanyiwa marekebisho: umri wa kugombea; utabaki miaka 21 badala ya kushuka mpaka 18. Wagombea binafsi;hawataruhusiwa.

Kuhusu kilio cha miaka mingi cha wadau cha kutaka Uchaguzi usimamiwe na Tume ya uchaguzi kama ilivyo katika baadhi ya nchi nyingine duniani; makubaliano yameweka bayana kuwa uchaguzi utaendelea kusimamiwa na serikali kupitia waziri mwenye dhamana ya serikali za mitaa. Kwa mantiki hiyo basi hata hoja ya kutaka kanuni za uchaguzi zitungwe na chombo huru haitazingatiwa.

Mwito wa Vyama vya siasa kutaka viwezeshwe kutoa elimu ya uraia nao hautazingatiwa. Serikali ilishaweka msimamo kuwa jukumu la kutoa elimu ya uraia litaendelea kuwa la serikali, vyama vya siasa vinaweza kutoa kwa kutumia rasilimali zao.

Hoja ya kutaka uchaguzi wa madiwani uende sambamba na chaguzi zingine za mitaa nayo haitarajiwi kuwepo katika kanuni zitakazotolewa na Waziri Mkuu Pinda. Uchaguzi wa madiwani utaendelea kuwa na uchaguzi mkuu mwaka 2010; hii ni kwa sababu suala hili linahitaji marekebisho ya kisheria na serikali imeshatamka wazi kwamba muda umeshakwisha wa kufanya marekebisho husika.

Haya ni masuala nyeti ambayo wadau wengi wangependa yafanyiwe marekebisho lakini hakuna mabadiliko yoyote ambayo Serikali itayafanya kuhusu masuala hayo katika kanuni zinazotungwa ambazo Waziri Mkuu Pinda atazitangaza siku za usoni.

Mtiririko wa masuala haya kwa ujumla unadhihirisha kwamba serikali haikupanga kufanya mabadiliko ya msingi na kutoa uzito unaostahili kwa uchaguzi wa vitongoji, vijiji na mitaa. Kirasilimali makubaliano yalilenga tu kwamba katika bajeti ya mwaka wa fedha 2009/10 serikali itatenga bilioni nane(8) tu zitakazotumika kusimamia na kuratibu uchaguzi wenyewe ngazi ya halmashauri ifikapo Oktoba 2009.

Wakati serikali ikipanga kutenga fedha kiasi kidogo kama hicho kwa ajili ya kuendesha uchaguzi wa vitongoji, vijiji na mitaa nchi nzima, tume ya uchaguzi kwa upande wake inatarajia kutumia bilioni 42.9 kama gharama za kuboresha daftari la wapiga kura pekee kuanzia mwaka 2009. Tume hiyo hiyo inakadiria kutumia bilioni 64.5 kuendesha uchaguzi wa mwaka 2010. Itakumbukwa kuwa mwaka 2005, Tume ya uchaguzi ilitumia bilioni 62.5 katika uchaguzi mkuu.

Hata wadau wengine wa maendeleo hawajaweka mkazo wa kutosha kuhusiana na uchaguzi huu, mathalani miradi ya Shirika la Umoja wa Mataifa na michango ya washirika wa kimaendeleo kuhusu uchaguzi, imeelekezwa katika uchaguzi wa mwaka 2010 pekee.

Hata hivyo, kwa mujibu wa makubaliano; marekebisho yafuatayo yatafanyika na kuzingatiwa katika kanuni zinazotarajiwa kutolewa mwezi Agosti mwaka 2009. Hivyo wadau wanapaswa kujadili na kufuatilia kuhakikisha kwamba Waziri Mkuu Pinda hapindishi maamuzi hayo.

Kanuni zinapaswa kuelekeza kwamba kutakuwa na karatasi maalum za kura zenye nembo ya halmashauri husika; karatasi hazitakuwa na majina ya wagombea, majina yatabandikwa sehemu ya wazi baada ya uteuzi. Ndoo maalum za plastiki zenye kuonyesha(transparent) zitatumika kupigia kura badala ya masanduku ya kura.

Uchaguzi utafanyika kwenye majengo ya umma, kama hakuna msimamizi atashirikiana na vyama kupata sehemu muafaka. Kanuni zinapaswa zieleze kuwa uchaguzi wa Wenyeviti wa Kijiji, Wajumbe wa Halmashauri za Kijiji na Wenyeviti wa Vitongoji utafanyika katika kitongoji ili kuwafanya wapiga kura wengi kuweza kufika na kupiga kura zao; Kampeni zitafanyika kwa muda wa siku saba kama ilivyo kwa kanuni za 2004. Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Mitaa na wajumbe wa Kamati za Mitaa utafanyika katika mitaa husika, vituo vitakuwa zaidi ya kimoja kulingana na wakazi wa mtaa.

Kwa mujibu wa makubaliano Orodha ya wapiga kura(Local Voter register) itaandaliwa siku 21 kabla ya uchaguzi ili kutoa nafasi kwa wapiga kura kukagua orodha na kuweka pingamizi. Orodha itaandaliwa na watumishi wa umma lakini wasiwe watendaji wa vijiji, mitaa au kata. Uthibitisho wa mpiga kura utatokana na jina lake kuwepo katika orodha ya wapiga kura, vitambulisho vitavyotumika kumtambulisha chochote kati ya vifuatavyo- kadi ya mpiga kura, kitambulisho cha kazi, hati ya kusafiria, kadi ya benki, kadi ya bima ya afya, kitambulisho cha chuo/shule, leseni ya uderava au wakazi kama mpiga kura hana kitambulisho chochote.

Kanuni zinapaswa kuwa na kifungu cha kamati ya rufaa ambayo wajumbe wake watateuliwa kutokana na hali ya eneo husika ila hawatakuwa kati ya wafuatao; afisa anayehusika na uteuzi wa wagombea, msimamizi au msimamizi msaidizi wa uchaguzi, kiongozi wa ngazi yoyote wa chama cha siasa, mtumishi wa halmashauri, kiongozi yoyote wa dini. Masuala haya na mengine yako mikononi mwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, wadau wanajiuliza; atatunga kanuni za uchaguzi zenye kuzingatia haki na demokrasia au ataleta mizengwe ya kupindisha makubaliano? Tunasubiri!

Mwandishi wa makala hii ni Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CHADEMA anayepatikana kupitia 0754694553, mnyika@yahoo.com na http://mnyika.blogspot.com

No comments: