Sunday, March 7, 2010

Tamko la Mnyika kuhusu Taarifa ya SMVU

TAMKO KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU TAARIFA YA SEKRETARIATI YA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA


UTANGULIZI:

Tarehe 24 Februari 2010 Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ofisi ya Rais- Sekretariati ya Maadili ya Viongozi wa Umma ilitoa taarifa kwa umma kuhusu habari iliyotoka katika Gazeti la Jambo Leo Jumapili tarehe 21 Februari 2010 iliyokuwa na kichwa cha habari “ Mkapa Kitanzini-adaiwa kuvunja katiba bila kuwajibishwa”.

Taarifa hiyo iliyotolewa na Kamishna wa maadili ilitolewa kama tangazo la kulipia katika gazeti la Mtanzania la ijumaa tarehe 26 Februari, 2010; na baadaye taarifa hiyo ikachapwa kama Tangazo la kulipia tena katika magazeti mengine likiwemo Mwananchi, magazeti ya serikali nk. Karibuni kabisa, tangazo hilo likatolewa kwa mara nyingine kwa kulipia katika gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa Machi 5 mwaka 2010.

Maudhui ya tangazo hilo hususani matumizi ya maneno kama ‘nia mbaya’, ‘uongo’ na kiwango cha kutolewa kwake katika magazeti mbalimbali kukanusha habari iliyoandikwa na gazeti moja ni dalili ya propaganda ambazo zinafanyika kwa kutumia fedha za umma hivyo ni muhimu nikatoa taarifa hii kwa umma kufanunua masuala kadhaa ya msingi ya kuzingatiwa.

Taarifa ya sekretariati ya viongozi wa umma imekanusha habari iliyoandikwa na Jambo Leo tarehe 21 Februari 2010 lililomnukuu “John Mnyika-Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CHADEMA kwamba alisema kuwa Rais Mkapa hakutaja mali zake baada ya kutoka madarakani.”

Taarifa ya Sekretariati ya Maadili wa Viongozi wa Umma iliendelea kusema kwamba “Sekretariati inathibitisha kwamba Rais Mstaafu Mheshimiwa Benjamin William Mkapa aliwasilisha tamko lake alipoacha wadhifa wake wa Rais wa awamu ya tatu kwa mujibu wa kifungu cha 9(1) D cha Sheria ya maadili ya viongozi wa umma namba 13 ya mwaka 1995”.

Taarifa hiyo ya Sekretariati ya maadili ya umma ilimalizia kwa “kuwaelekeza wahariri na wanasiasa wa aina ya ‘Mnyika’ kuwasiliana na uongozi wa sekretariati” ili kupata usahihi na ukweli wa taarifa za mali na madeni ya viongozi.

“Nimeshangazwa na Sekretariati ya maadili ya umma kutoa tamko bila kurejea kauli zangu kamili kama ambavyo nilizitoa kwenye kipindi cha Kipima Joto kilichorushwa katika kituo cha luninga cha ITV ijumaa tarehe 19 Februari 2010 pamoja na Jambo Leo kudokeza kuwa chanzo cha habari yako ni kipindi husika.”

Izingatiwe kuwa Majadiliano katika kipindi hicho kilichorushwa moja kwa moja (live) yalihusu swali “ Kanuni za Maadili ya Viongozi wa Umma; Je, zinasaidia?”, na kwamba ilitangazwa katika kipindi husika kuwa sekretariati ilialikwa katika kipindi cha siku hiyo lakini haikutuma mwakilishi yoyote.


HOJA ZILIZOPASWA KUTOLEWA MAELEZO NA SEKRETARIATI YA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA:

Katika kipindi husika nilitoa kauli ya kumtaka Rais Kikwete kuchukua hatua yeye binafsi pamoja na ofisi ya Rais ikiwemo Sekretariati ya Maadili ya Viongozi wa Umma kuhusu tuhuma zifuatazo ambazo kwa miaka kadhaa zimekuwa zikitawala miongoni mwa umma hususani katika vyombo vya habari:

Kwamba katika kushughulikia suala la mmomonyoko wa maadili katika uongozi wa umma ikiwemo suala la ufisadi lazima tuweke malengo ya muda mfupi na malengo ya muda mrefu. Malengo ya muda mrefu ni kubadili mfumo wa utawala kwa kufanya mabadiliko ya uongozi, kuweka dira ya pamoja, maadili ya taifa, utamaduni wa uwajibikaji na kufanya mabadiliko ya katiba yenye kujenga taasisi. Wakati tukisubiri mabadiliko hayo ambayo kwa kiasi kikubwa yanatokana pia na uchaguzi wenye kupunguza nguvu ya chama kimoja katika vyombo vya maamuzi, hatuwezi kama taifa kuacha ufisadi na ukiukwaji wa maadili ukaendelea badala yake tunaweza kutumia katiba na sheria zilizopo kuchukua hatua za haraka.

Kwamba Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 132 imeweka msingi wa kuundwa kwa Sekretariati ya Maadili ya Viongozi wa Umma na kwamba Ibara ya 70 kuwasilisha taarifa ya mali na kifungu cha 71 kinataja sababu za kukoma kuwa mbunge kutokana na kukiuka masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa umma. Lakini kila mwaka Sekretariati imekuwa ikilalamika kwamba wapo viongozi ambao hawajazi. Na mwaka 2008 na 2009 Waziri husika alilieleza Bunge kuwa kuwa kuna ambao hawajajaza fomu husika; lakini mpaka sasa hakuna aliyeondolewa kwenye nafasi kwa sababu hiyo. Nikaendelea kueleza kwamba pamoja na kuwa Sheria husika imekinzana na katiba kwa kueleza adhabu nyingine chini ya kuondolewa madarakani; sekretariati haijawahi kueleza adhabu ambazo imezitoa. Hivyo, nikaitaka sekretariati ieleze wazi hatua ambazo imechukua; jambo ambao katika taarifa yao kwa umma hawajaligusia kabisa.

Kwamba jambo la msingi ni kuwa tunahitaji viongozi wetu wasimamie utawala wa sheria na suala hili la maadili ya viongozi wa umma, wakalaumiwa haipaswi kuwa Sekretariati ya maadili bali watawala hususani Rais wa nchi. Na nikanukuu kifungu cha 5 kipengele cha (1) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa umma ya mwaka 1995 ambacho kinasema bayana kuwa itakuwa ni wajibu wa Rais kuchukua hatua zitakazoleta mabadiliko ya maadili yenye lengo la kuweka msingi wa kuongeza imani kwa wananchi kuhusu uadilifu wa viongozi. Hivyo, nikatoa kauli ya kumtaka Rais Kikwete yeye mwenyewe au kupitia ikulu au Wizara ya Utawala bora kueleza hatua ambazo zimechukuliwa kwa viongozi ambao wanatuhumiwa kukiuka kanuni za maadili ya uongozi wa umma. Nikatoa mfano kwamba Rais Mstaafu Mkapa amekuwa akituhimiwa kufanya biashara ikulu na kwenye kashfa ya Kiwira; Je, ni hatua gani ambazo Rais ameelekeza zichukuliwe zaidi ya kusema kwamba aachwe apumzike (jambo ambalo ni ishara ya kupuuza misingi ya kikatiba na kisheria inayotaka uwajibikaji wa viongozi wawapo madarakani na hata wanapostaafu) ? Nikakumbusha kwamba Rais Mstaafu Mkapa alipoingia madarakani alitaja mali zake zote hadharani, lakini alipotoka hakutaja mali zake zote. Tuhuma zinazotolewa juu ya Mkapa zile za ufisadi na hata za kutotaja mali zote ni za uvunjaji wa Katiba na Sheria; hatua gani zimechukuliwa? Pia, nikatoa mfano mwingine wa Adrew Chenge(Mb) ambaye uchunguzi wa SFO ya Uingereza umebaini kuwa ana akaunti nje ya nchi; je fedha zote zilitangazwa kwenye tamko lake la mali na madeni? Iwe ametangaza au hakutangaza sekretariati ilipaswa kuchukua hatua ya kumchunguza kwa kuwa sheria haisemi tu Sekretariati ipokee taarifa bali ina mamlaka ya kuchunguza ukweli wa taarifa husika na uhalali wa kimaadili wa umiliki wa mali. Sekretariati ya Maadili ya Umma haikujibu tuhuma za msingi zaidi ya kusema tu kwa ujumla kuwa Rais Mstaafu Mkapa alitangaza mali zake kwa kujaza fomu zinazotolewa na chombo hicho.

Kwamba wapo wanaojenga hoja kuwa kama watu wanatuhuma dhidi ya viongozi basi wakakague mali katika sekretariati au wawasilishe malalamiko rasmi; hoja hii haizuii Rais na Sekretariati kuwajibika kwa kuwa Sheria hiyo hiyo inatamka kwamba tuhuma zinazotakiwa kushughulikiwa ni pamoja na Sekretariati yenyewe kuanzisha uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazohusu viongozi wa umma zikiwemo ambazo zimejitokeza katika vyombo vya habari. Hivyo, Rais Kikwete na Sekretariati wanawajibika kueleza kwa umma ni hatua gani zimechukuliwa kwa viongozi wa umma ambao tuhuma zao zimekuwa zikitajwa mara kwa mara kwenye vyombo vya habari ikiwemo wale waliotajwa hadharani kwenye Orodha ya Mafisadi (list of shame) toka Septemba 15 mwaka 2007. Nilieleza kwamba hata kwenye kashfa ya Richmond, TAKUKURU wakati huo ikiitwa TAKURU pamoja na kutoa ripoti mbovu ya kuusafisha mchakato wa zabuni hiyo bado ilikiri kwamba RICHMOND ilikuwa ikipata taarifa za ndani ya serikali. Viongozi wa umma waliokuwa wakitoa taarifa za umma kinyemela kwa Richmond ili kushinda zabuni ni wazi walikiuka sheria ya maadili ya viongozi wa umma lakini hakuna hatua ambazo sekretariati ilichukua hata baada ya taarifa hizo kutolewa kwenye vyombo vya habari. Sekretariati ya Maadili ya Umma haikujibu suala hili katika taarifa yake.

Kwamba kwenda kukagua ama kuhakiki daftari la mali na madeni ya viongozi wa umma kunapoteza maana kwa kuwa Kanuni zilizotungwa na Serikali vipengele cha 6 na 7 vinaelekeza bayana kuwa ukishakagua mali husika huruhusiwi kuzizungumzia hadharani (ambayo masharti makubwa ya ziada pamoja na Sheria ya maadili ya viongozi wa umma). Nilikumbusha kwamba Wanaharakati walifungua kesi ya kikatiba mahakama kuu Aprili 2008 kupinga vipengele tajwa kesi ambayo mpaka sasa hukumu yake haijatolewa. Sekretariati ya Maadili ya Umma haikulitolea taarifa suala hili pia.

Msingi mkuu wa hoja zangu nilizotoa ni kwamba uwepo wa kanuni za maadili pekee hauwezi kusaidia iwapo kanuni hazisimamiwi, na pia hauwezi kusaidia iwapo kanuni ni mbovu. Nilieleza bayana kwamba sheria na kanuni husika hazina meno ya kutosha lakini hata yale meno kidogo yaliyopo hayang’ati; kwa kuwa hakuna hatua stahili zinazochokuliwa. Kwani mpaka sasa Sekretariati haijawahi kutoa taarifa ya yoyote kuhusu aliyewahi kuchukuliwa hatua za kisheria kwa kutokutangaza mali zake ama kutoa taarifa za uongo katika fomu husika. Hivyo, pamoja na udhaifu wa sheria, changamoto kubwa zaidi ni kutokusimamiwa kwa utawala wa sheria ambao katika suala hili la maadili wahusika wakuu katika kusimamia sheria husika ni ofisi ya Rais hususani sekretariati ya maadili ya viongozi wa umma.

MASWALI NA MASUALA YA ZIADA AMBAYO OFISI YA RAIS NA SEKRETARIATI YA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA WANAWAJIBIKA KUYAJIBU NA KUYATOLEA TAARIFA:

Mosi; Watanzania wenzangu na mamlaka husika zizingatie kwamba msingi wa tuhuma nilizotoa tarehe 19 Februari 2010 kuhusu Mkapa kufanya biashara Ikulu, matumizi mabaya ya madaraka katika mchakato wa Kiwira na kutokutoa taarifa za mali zake zote na madeni yake baada ya kutoka madarakani ni kutolewa kwa tuhuma hizo mara kadhaa mwaka 2006, 2007, 2008 na 2009 bila kutolewa majibu kamili na Sekretariati ya Maadili ya Viongozi wa Umma au Rais Mstaafu Mkapa mwenyewe. Tuhuma kuwa Rais Mstaafu hakutaja mali zake zilianza kutolewa bungeni na Fatma Maghimbi (Mb) wakati akichangia mjadala kuhusu Hotuba ya Rais Kikwete aliyoitoa tarehe 30 Disemba 2005 wakati akizundua bunge. Sekretariati ya Maadili ya Viongozi wa Umma haikutoa tamko wakati huo. Viongozi wengine waliowahi kutoa tuhuma hiyo hadharani na kunukuliwa na vyombo vya habari ni pamoja na: Profesa Ibrahim Lipumba (Tanzania Daima-20/04/2008); Profesa Mwesiga Baregu (Mwananchi-21/11/2009). Aidha taarifa kwamba Rais Mstaafu Mkapa hajawahi kutangaza mali zake baada ya kutoka madarakani ziliandikwa pia na wanahabari kadhaa mathalani: Rai (12/1/2006); Tanzania Daima (01/04/2009) nk. Hivyo, Sekretariati ya Maadili ya Umma inapaswa kueleza Rais Mstaafu Mkapa alijaza lini hasa tamko juu ya mali zake? Na kwanini Sekretariati haikutoa taarifa katika kipindi chote toka mwaka 2006 pamoja na tuhuma hiyo kuandikwa na vyombo mbalimbali vya habari mpaka pale Gazeti la Jambo Leo lilipozirudia katika toleo lake la Jumapili tarehe 21 Februari 2010 ? Tamko la Sekretariati limekidhi sehemu ya matakwa ya sheria husika lakini halijakidhi mahitaji ya umma na misingi ya uwajibikaji hivyo, kupitia tamko hili natoa mwito wa Rais Mstaafu Mkapa mwenyewe kutaja mali zake hadharani kama sehemu ya ‘ukweli na uwazi’ ambao amekuwa akihimiza toka mwaka 1995 alipoingia madarakani katika kipindi chake cha kwanza cha Urais.

Pili; kwa kuwa Sekretariati ya Maadili ya Umma imejitokeza rasmi kutoa kauli ya kujibu kwa niaba ya Rais Mstaafu Mkapa, naiomba ijibu maswali yafuatayo ambayo umma umekuwa ukijiuliza na yako ndani ya mamlaka ya sekretariati husika kuyazungumzia: Je, Sekretariati ya Maadili ya Viongozi wa Umma imehakiki mali zote na madeni ya Rais Mkapa ili kuthibitisha usahihi na ukweli wa taarifa zilizowasilishwa? Je, mali zilizotajwa zinajumuisha pia mali zinazotajwa kumilikiwa na Rais Mkapa na mkewe zikihusishwa na tuhuma mbalimbali za kukiuka Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma mathalani kufanya biashara Ikulu kupitia kampuni ya ANBEN, kujiuzia bei chee mgodi wa umma katika kashfa ya Kiwira ambayo Rais Mkapa alitajwa kuwa mmoja wa wanahisa? Je, Sekretariati ilichukua hatua gani baada ya tuhuma hizo kutolewa hadharani na kwenye mamlaka mbalimbali ikiwemo bungeni zikihusisha pia kukiuka kifungu 12(1)(a) kinachokataza kiongozi kutumia taarifa zinazopatikana kwenye uongozi wa umma kwa manufaa binafsi? Suala hili linahusu pia tuhuma dhidi ya Andrew Chenge (Mb) katika kashfa ya Rada zinahusu pia kukiuka Sheria ya Maadili ya Viongozi wa umma kifungu 12(e) kwa kupokea maslahi ya kiuchumi wakati wa manunuzi na mikataba. Sekretariati imepewa mamlaka kwa mujibu wa sheria husika kifungu 18(4) kuanzisha na kufanya uchunguzi wa tuhuma hata kama hakuna mtu aliyekwenda kuwasilisha malalamiko rasmi na pia inaweza kuchunguza tuhuma hata zilizotoka kwenye vyombo vya habari kwa mujibu wa kifungu 22(4). Hivyo, Sekretariati inapaswa kueleza umma toka tuhuma zitolewe hadharani kupitia Orodha ya Mafisadi (List of Shame) Septemba 15 mwaka 2007 uchunguzi gani imeukamilisha na hatua kuchukuliwa kwa watajwa wote? Izingatiwe kuwa pamoja na uchunguzi wa awali unaoweza kufanywa na Sekretariati kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma namba 13 ya mwaka 1995 kifungu 22(2); uchunguzi kamili unafanywa na baraza ambalo kwa mujibu wa kifungu 26(5) linapaswa kufanya uchunguzi wake hadharani ili umma uweze kufahamu.

Tatu; Sekretariati itoe taarifa ya kueleza bayana imechukua hatua gani kwa viongozi wa umma ambao hawajataja mali na madeni yao au wametoa taarifa za uongo kama ilivyoelezwa kwa miaka kadhaa na sekretariati yenyewe pamoja na Ofisi ya Rais ( Rejea- Habari Leo 12/1/2007, 26/1/2007; 29/1/2007; Mwananchi 18/09/2007 na taarifa zingine zilitolewa kwenye vyombo vya habari mwaka 2008 na 2009). Aidha ikumbukwe kwamba Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Hawa Ghasia wakati akiwasilisha makadario ya bajeti ya fedha ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2008/2009 alitoa ahadi kuwa Serikali ingewachukulia hatua za kisheria viongozi wa umma 3,186 kwa kuwa hawakurudisha fomu za tamko la mali. Pia, Taarifa ya Mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Nne katika kipindi cha miaka mitatu iliyotolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais(Utawala Bora)-Sofia Simba mwaka 2008 ilisema kwamba serikali inachunguza baadhi ya viongozi baada ya kubaini wana mali zaidi ya walizotaja kwenye fomu baada ya kuhakiki mali za viongozi 260 tu kati ya viongozi zaidi ya 7000 ambao ilipaswa kuhakiki mali zao. Sekretariati ni muhimu pia ikatoa taarifa ya kuuleza umma kwanini haikagui mali za viongozi wote kama inavyohitajiwa kwani hapo kabla iliwahi kueleza kupitia kwa kamishna wake mkuu kwamba ina uhaba wa fedha za kuweza kutekeleza kwa wakati zoezi hilo la kisheria ( Habari Leo- 18/09/2007). Badala ya kutumia fedha nyingi za walipa kodi kwenye kutoa matangazo ya maneno ni muhimu kwa sekretariati kuwekeza katika kufanya vitendo vya uhakiki, uchunguzi na kuchukua hatua stahili kwa manufaa ya umma. Sekretariati ikumbuke kuwa Rais Kikwete aliagiza toka mwaka 2007 wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Nane wa CCM kwamba mali zote za viongozi wa umma zitahakikiwa na kuchunguzwa badala ya utaratibu wa zamani wa kuorodhesha tu kwenye daftari.

Nne; Natambua kwamba Sekretariati ya Maadili ya Viongozi wa Umma imewaelekeza wahariri na wanasiasa wa aina ya “Mnyika” kuwasiliana na uongozi wa sekretariati ili kupata taarifa za mali na madeni ya viongozi. Kabla sijatoa tamko la kukataa ama kukubali maelekezo hayo kuna masuala ambayo wahariri na wanasiasa ambao Sekretariati imewabatiza jina la ‘aina ya Mnyika’ ni lazima tukapatiwa ufafanuzi. Sekretariati ituhakikishie kwamba hata baada ya kupitia taarifa za kumbukumbu hizo za mali na madeni ya viongozi tutaendelea kutumia uhuru wetu wa kikatiba wa haki ya kupata na kutoa taarifa kama ulivyotolewa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 18 vipengele (a) (b) (c) (d) badala ya kuzibwa mdomo kutoendelea kuzungumzia mali hizo baada ya kukagua daftari. Izingatiwe kuwa Waziri mwenye dhamana kwa mamlaka aliyopewa na Sheria kifungu 20(3) alishatunga kanuni zenye vipengele 6(1) (2) na 7(2) (c) vinavyokataza mwananchi kuzizungumzia popote taarifa hizo baada ya kuzikagua . Kwa upande mwingine, sekretariati ituhakikishie kwamba itatoa taarifa zote kwa wakati kwa kadiri ya tukavyohitaji kwa sababu kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma kifungu 20(1)(2) taarifa zote zinapaswa kuingizwa kwenye daftari ambalo linaweza kukaguliwa na umma kwa nyakati zote zinazofaa. Hivyo Sekretariati itoe kwanza tamko kuwa imefikia wapi kuwaruhusu Viongozi wa Vyama vya Upinzani ambao kwa barua yenye kumbukumbu CCTN/TC/DSM/UF/2008/002 ya mwezi Aprili 2008 waliomba kukagua matamko ya mali za viongozi hususani waliotuhumiwa kwa ufisadi lakini mpaka sasa inakaribia miaka miwili sekretariati haijaruhusu daftari la mali husika kukaguliwa likiwemo tamko la Rais Mstaafu Mkapa . Ikumbukwe kwamba viongozi wa vyama walikwenda kwenye Sekretariati na kutimiza masharti yote ikiwemo kujaza fomu na kufanya malipo ya ada ya ukaguzi; Sasa Sekretariati inawahakikishia kwa kiasi gani wahariri na wanasiasa ‘aina ya Mnyika’ kwamba tukienda hivi sasa tutapatiwa taarifa kuhusu Mkapa na wengine ama utakuwa ni mwendelezo mwingine wa kufunika mijadala ya umma kwa kisingizio cha kusubiria ‘taarifa sahihi’ kutoka kwenye sekretariati hiyo?. Wakati tukisubiria maelezo na maelekezo ya ziada toka Sekretariati ya Maadili ya Uongozi wa Umma tutaendelea kuandika na kuzungumza kuhusu suala hili kama sehemu ya kuhamasisha uwajibikaji wa viongozi na kutetea rasilimali za taifa.


Imetolewa tarehe 07 Machi 2010 na:




John Mnyika
mnyika@chadema.or.tz
0754694553








No comments: