Friday, June 18, 2010

Nilirudisha fomu ya Ubunge Ubungo 6/6

AHADI ZA JK HAZIJATEKELEZWA-MNYIKA

MKURUGENZI wa Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw. John Mnyika jana alirudisha fomu za kuomba kuwania ubunge katika Jimbo la Ubungo na kumshutumua Rais Jakaya Kikwete kuwa ameshindwa kutekeleza ahadi alizotoa kwa Watanzania, likiwamo la kuleta maji Dar es Salaam.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara kabla ya kurejesha fomu hizo, Bw. Mnyika alisema pamoja na ahadi hiyo ya maji kutotekelezwa na Rais Kikwete kuwatupia mzifo Dawasa na Dawasco, pia ameendelea kutoa 'ahadi hewa' zinazoongeza ugumu wa maisha kinyume na alivyoahidi maisha bora kwa kila Mtanzania wakati anaomba kuchaguliwa.Akihutubia mkutano huo uliojaa mashabiki wake na wasikilizaji wengine katika eneo la Manzese, Bw. Mnyika alisema baada ya kuingia madarakani serikali ya awamu ya nne kumekuwa na kero nyingi kutokana na viongozi wengi kuwa wabinafsi na hivyo kutumia fedha za umma kujilimbikizia mali.

"Tulitegemea serikali kufufua viwanda vilivyokufa ili kuwapatia ajira wamachinga na mamalishe wanaohangaika katika viwanda hivyo, lakini mambo yamekuwa kinyume na matarajio," alisema Bw. Mnyika.

Alisema mabadiliko ya kweli yatapatikana kwa wananchi kupiga kura kuwachagua viongozi wanaopenda maendeleo.

Bw. Mnyika alikosoa kauli aliyoitoa Rais Kikwete wakati wa ziara yake jijini Dar es Salaam hivi karibuni kuwa anawafahamu kwa majina madiwani wanaouza viwanja na kuwaonya, kuwa ina nia ya kuwalinda wezi.

"Kama Kikwete hatachukua hatua dhidi ya madiwani na meya, suala la kuuza viwanja vya wazi na vya umma, litafikishwa kwa wananchi kuamua," alisema Bw. Mnyika

Alisema mfumo wa sasa umekuwa wa wananchi kutumikishwa na viongozi kwa maslahi yao badala ya viongozi kuwatumikia wananchi kama inavyotakiwa.

Mkutano huo ulisindikizwa na maandamano yalioanzia Manzese hadi Ofisi za CHADEMA Jimbo la Ubungo kurudisha fomu.

Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Jamii (CCJ), Bw. Dickson Ng'hily aliyesema demokrasia haiwezi kuwepo kama nchi itaongozwa na chama kimoja kwa muda mrefu.

"Tumeungana na CHADEMA ili kuwatia moyo Watanzania kuwa hatutakiwi kulala mpaka kieleweke, tunatakiwa kupigana imara hadi tupate maisha bora kwa kuchagua viongozi bora," alisema Bw. Ng'hily.

Chanzo: http://majira.co.tz/index.php?option=com_content&view=article&id=426:ahadi-za-jk-hazijatekelezwa-mnyika&catid=1:latest-news&Itemid=18

Picha mbalimbali wakati nikirudisha fomu zinapatikana hapa:

NIPE NIKUPE: http://nipenikupe.blogspot.com/2010/06/john-mnyika-arudisha-fomu-kwa-kishindo.html

NA

WAVUTI: http://www.wavuti.com/4/post/2010/06/john-mnyika-achukua-fomu-za-ubunge-ubungo.html

No comments: