Tuesday, June 29, 2010

Mnyika ataka Londa, Kandoro na Makamba wahojiwe ufisadi wa ardhi

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuf Makamba na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Abbas Kandoro, wanastahili kuhojiwa katika kashfa ya uuzwaji viwanja vya wazi katika manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Viongozi hao katika chama tawala na serikali, wanadaiwa kuhusika katika kashfa hiyo walipokuwa Wakuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa nyakati tofauti.

Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa, Makamba anatajwa kama Katibu Mkuu wa CCM na pia anatajwa kwa nafasi yake alipokuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Chadema inataka viongozi hao wahojiwe kwa vile wanatajwa kwenye taarifa ya kamati ya siasa ya halmashauri kuu ya CCM wilayani Kinondoni.

Alisema taarifa hiyo ya siri ya Machi 15, mwaka juzi, ilihusu mgogoro wa madiwani wa manispaa ya Kinondoni dhidi ya Meya wake, Salum Londa, mpasuko miongoni mwa madiwani, ubadhirifu wa fedha, mali ya manispaa na uongozi mbovu katika manispaa hiyo.

Mnyika alisema Kandoro, ambaye ndiye aliyemrithi Makamba kwa nafasi hiyo mkoani humo, anatakiwa ahojiwe kwa vile naye anatajwa katika taarifa hiyo.

Mbali na Makamba na Kandoro, Chadema pia inataka Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, William Lukuvi, awaeleze Watanzania alikuwa anafahamu nini kuhusu kashfa hiyo, ambayo inawataja kwa majina Londa na madiwani wengine wa manispaa ya Kinondoni kwenye tuhuma za rushwa na uuzaji wa viwanja.

Katika taarifa hiyo, Londa anatuhumiwa kupokea rushwa ya Sh. milioni 20, na kwa sababu hiyo Chadema, inataka asiishie kuhojiwa tu, bali akamatwe na kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo.

Kwa mujibu wa Mnyika, Chadema inataka viongozi hao wahojiwe na Polisi pamoja na kamati iliyoundwa na Lukuvi hivi karibuni.

Kamati hiyo iliundwa kwa lengo la kupitia maeneo yote ya wazi ya jiji la Dar es Salaam, kuyabaini na kuainisha kama yalivyo katika ramani kuu (master plan).

Hatua hiyo ingefanikisha kufahamu orodha kamili ya maeneo hayo, yalipo, yamepangiwa shughuli gani na wamiliki ni akina nani na utaratibu gani ulitumika kuyagawa.

Mnyika ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Chadema, alisema wanataka viongozi hao wahojiwe na wengine kukamatwa ili kujiridhisha kwamba, dhamira ya kuundwa kwa kamati hiyo si mchakato wa kisiasa wa kuelekea Uchaguzi Mkuu.

Alisema siasa hizo zinaweza kutumiwa kupitia kero zinazowakabili wananchi kwa muda mrefu na mbazo serikali ya awamu ya nne haijazishughulikia tangu iingie madarakani.

“Sasa kama kweli wana dhamira ya dhati ya kuchukua hatua, tunataka polisi na kamati husika wamhoji Makamba kwa sababu anatajwa humu (kwenye taarifa ya CCM) siku zote, anatajwa kama Katibu Mkuu wa CCM, anatajwa kama kwa nafasi yake alipokuwa Mkuu wa Mkoa,” Mnyika alisema.

Aliongeza: “Wamhoji Kandoro, kwa sababu anatajwa humu. Na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam wa sasa hivi, Lukuvi, ambaye ndiye ameunda kamati, na yeye awaeleze Watanzania alikuwa anafahamu nini kuhusu hii taarifa ya mwaka 2008.”

Taarifa hiyo ya CCM ni ile inayowataja kwa majina Londa na madiwani wengine kwenye tuhuma za rushwa za uuzaji wa viwanja.

Wakati Chadema ikishinikiza hivyo, sakata hilo linaonekana `kumchanganya akili’ Meya Londa, ambaye hivi sasa anahaha kumsaka mchawi.

Meya Londa aliitisha kikao cha dharura cha Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Kinondoni jana, katika kile kilichoelezwa kuwa ni kuwatafuta madiwani wanaohusika katika uvujishwaji wa taarifa zinazohusu kadhia hiyo.

Kwa mujibu wa habari za kuaminika kutoka ndani ya kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa baraza hilo, Meya Londa anadaiwa kukanusha tuhuma zinazomkabili.

Londa na madiwani wengine watano wa manispaa hiyo, walikwisha kuhojiwa na polisi wa kanda maalumu ya Dar es Salaam juu ya tuhuma za uuzaji wa viwanja.

Mmoja wa madiwani waliohudhuria kikao cha jana, alieleza kuwa ajenda iliyotawala kikao hicho ilihusu masuala ya uuzaji wa viwanja vya wazi.

Hata hivyo, madiwani wengine walipoulizwa kikao hicho kilikuwa kinahusu nini, walisema kilikuwa kililenga masuala ya kisiasa yanayokihusu CCM.

Kwa upande mwingine jana maofisa mbalimbali wa serikali walikutana katika manispaa hiyo kwa ajili ya kikao maalumu cha kuendelea kufanya uchunguzi wa kashfa ya uuza viwanja kinyume cha sheria na taratibu.

Kikao hicho kilifanyika ukumbi wa jirani na walipokuwa wamekaa madiwani hao, ambapo pande zote hazikuruhusu waandishi wa habari kuhudhuria.

Alipoulizwa na waandishi wa habari, Londa alithibitisha kufanyika kikao hicho cha madiwani, lakini akasema ajenda kuu ilikuwa ni kuzungumzia masuala ya Chama cha Kuweka na Kukopa (Saccos) ilichoanzishwa na madiwani hao.

“Unajua sisi tuna Saccos yetu hapa kama madiwani na kwa kuwa tunamalizia muda wetu, lazima tuchukue fedha kwa ajili ya kwenda kufanyia kampeni,” alisema.

Meya huyo alionekana kutotaka kujibu maswali zaidi kutoka kwa waandishi wa habari waliofika ofisini kwake, ili kupata ufafanuzi kuhusu kikao alichoitisha.

Awali, Mnyika alisema wanatilia shaka utendaji wa kamati hiyo inayoanza kazi yake leo kwa sababu mbalimbali, ikiwamo muundo wake na uadilifu wa mwenyekiti anayeiongoza, Albina Burra.

Alisema Burra, ambaye ni Mkurugenzi katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kurugenzi anayoiongoza wizarani hapo mwaka 2007, 2008 na 2009, imekuwa ikituhumiwa kwa ufisadi katika mgogoro wa ardhi eneo la Luguruni-Kibamba, katika manispaa hiyo. Burra ni Mkurugenzi wa Mipango Miji na Vijiji katika Wizara hiyo.

Kutokana na hali hiyo, alisema ili shaka iondoke, wanataka kamati hiyo ifanye kazi kwa uwazi, ikiwa ni pamoja na kuviruhusu vyombo vya habari na wadau wengine kufuatilia majadiliano ya kamati, Lukuvi aeleze mamlaka na mipaka ya kazi ya kamati, itakamilisha lini kazi yake na ripoti yake iwekwe hadharani.

Aliwataka wananchi popote walipo kujitokeza kutoa ushahidi kwa kamati na kusema watakaohofia usalama wao, wawasiliane na Chadema kwa namba ya simu 0784222222 na barua pepe: kinondoni@chadema.or.tz This e-mail address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it ili wakawawakilishe.

Pia, alimtaka Lukuvi kuielekeza kamati ili katika kufanya kazi yake leo, izingatie kauli ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa hadharani mwaka huu, alipotembelea Manispaa Kinondoni kwamba anawajua kwa majina madiwani waliouza viwanja vya umma na kuwataka waache jambo hilo, la sivyo atawataja.

Alipoulizwa na Nipashe jana, Makamba alisema hapaswi kuhojiwa, bali anastahili kuulizwa ili aeleze ukweli wa mambo kuhusu mambo yote ya Jiji la Dar es Salaam.

Alisema ameongoza Dar es Salaam kwa takriban miaka 10, hivyo anajua mambo mengi yanayohusu sekta mbalimbali, ikiwamo ardhi.

“Anayehojiwa ni mhalifu, mimi sihojiwi. Londa ndiye anayepaswa kuhojiwa kwa sababu ndiye mwenye matatizo. Mimi niulizwe, nieleze ukweli wa mambo.

Mwingine anayestahili kuulizwa ni Kapteni (John) Chiligati (Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi) yeye anahusika na ardhi,” alisema Makamba.

Kwa upande wake, Kandoro alisema uamuzi wa kuhojiwa au la, uko mikononi mwa Kamati ya Lukuvi, hivyo ushauri uliotolewa na Chadema juu yake, haoni kuwa ni tatizo.

“Kwani tatizo liko wapi? Chadema wametoa maoni yao. Sasa wenye kamati wataamua wanihoji ama vipi,” alisema Kandoro.

Jumatano wiki iliyopita, Lukuvi alimfukuza kazi Ofisa Ardhi wa Manispaa hiyo, Magesa Magesa kwa tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi, akidaiwa kuidhinisha ujenzi katika kitalu namba 1274 na 1275 eneo la Msasani, Peninsula kwa Kampuni ya Tanzania Building Works. Tayari Magesa amefikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.

Mbali na kashfa hiyo, Manispaa ya Konondoni imejiweka pabaya kutokana na vitendo vya ukiukaji wa sheria, taratibu na kanuni za ardhi, na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kinondoni katika ripoti yake ya uchunguzi wa kadhia ya uvunjwaji wa ofisi ya Kata ya Msasani, imetaka uchunguzi ufanywe dhidi ya watendaji wa Manispaa hiyo.

Kamati hiyo ya Ulinzi ilifikia hitimisho hilo baada ya kubaini vitendo vingi vya ukiukaji wa sheria, kanuni na taratibu vilivyofanywa na watendaji wa Manispaa hiyo, kiasi kinachoamsha kuwepo kwa msukumo wa kufumbia macho kanuni za utumishi wa umma.

CHANZO: NIPASHE-26/06/2010

No comments: