Tuesday, May 1, 2012

Daraja Golani-Suca na Barabara Mburahati-Mabibo

Mkandarasi aliyepewa zabuni ya ujenzi wa daraja la Golani-Suka anapaswa kuanza mapema ujenzi wa daraja hilo muhimu linalounganisha kata za Kimara na Saranga ili kupunguza kero kwa wananchi hasa wakati wa mvua.


Mwezi huu wa Aprili nimefuatilia kuhusu hatma ya daraja hilo na hatimaye mkataba wa ujenzi wa daraja husika umesainiwa kati ya Manispaa ya Kinondoni na Mkandarasi Kika Co. Ltd kwa gharama za shilingi milioni 447.

Hata hivyo, ujenzi wa daraja husika haujaanza suala ambalo linahitaji Manispaa ya Kinondoni kumsimamia kwa karibu mkandarasi husika ili ujenzi uanze kwa haraka kwa kuwa mchakato wa zabuni ulianza kuanzia mwanzoni mwa mwaka 2012.

Izingatiwe kwamba kutokuwepo kwa daraja katika eneo hilo mwaka miaka mingi kumefanya mawasiliano katikati maeneo hayo kuwa magumu nyakati za mvua na kusababisha madhara ya kibinadamu na mali wananchi wanapovuka mto katika eneo hilo wakati wa mafuriko.

Baada ya kuwawakilisha wananchi kutaka ujenzi wa daraja hilo lilingizwa kwenye bajeti ya Manispaa ya Kinondoni kwa mwaka wa fedha 2011/2012 hata hivyo miezi ikiwa imebaki takribani miwili kabla ya mwisho wa bajeti husika ujenzi wa daraja hilo ulikuwa haujaanza bado.

Hatua kama hiyo inahitajika pia kwa barabara ya Mburahati mpaka Mabibo NIT ambayo inapaswa kuanza kujengwa kwa kiwango cha lami ikiwa imetengewa kiasi cha shilingi milioni 504 kwa ajili ya kuchangia katika kupunguza msongamano wa magari katika barabara ya Morogoro .

Tathmini ya utekelezaji wa bajeti inaonyesha kwamba kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ni ndogo pengo ambalo linapaswa kuzibwa kwa kusimamia kwa karibu miradi inayopaswa kuanza katika muhula uliobaki wa mwaka wa fedha 2011/2012.

1 comment:

Anonymous said...

Kazi nzuri kaka. Hi ndio vitu wananchi tunataka na sio porojo tu.