Friday, August 3, 2012

Muswada binafsi kwa hati ya dharura: Marekebisho ya Sheria za Hifadhi ya Jamii

Leo tarehe 03 Agosti 2012 kwa mujibu wa Kanuni ya 68 (7) ya Kanuni za Kudumu za Bunge na kwa kuzingatia kuwa marekebisho yamefanyika kwenye ratiba ya bunge ambapo Mkutano wa Bunge sasa umepangwa kuahirishwa tarehe 16 Agosti 2012 na hoja za wabunge zimeondolewa kwenye ratiba.

Nimeomba muongozo ama Serikali itoe kauli bungeni ya kutengua tangazo lililotolewa na Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) ili kuwezesha mafao ya kujitoa kuendelea kutolewa au uongozi wa Bunge uruhusu niwasilishe muswada binafsi wa sheria kwa hati ya dharura tarehe 16 Agosti 2012 kwa ajili ya kufanya marekebisho kwenye sheria husika ili kuruhusu mafao ya kujitoa kuendelea kutolewa.

Pamoja na hatua hiyo ya kuomba muongozo nimechukua hatua ya ziada ya kumwandikia Katibu wa Bunge kumweleza kusudio la kuwasilisha Muswada Binafsi juu ya Marekebisho ya Sheria za Hifadhi ya Jamii (The Social Security Laws (Ammendments) Act wa mwaka 2012 kwa hati ya dharura kwa mujibu wa Kanuni ya 81 ya Kanuni za Kudumu za Bunge (Toleo la Mwaka 2007).Lengo la Muswada huo ni kufanya marekebisho yenye kuwezesha kurejeshwa kwa fao la kujitoa (withdrawal benefits) ili kuruhusu kuendelea kutolewa kwa mafao kwa mwanachama wa mfuko ya hifadhi ya jamii anapoacha kazi na kuhitaji kupewa mafao yake kabla ya kufikisha umri wa kustaafu kwa hiari (miaka 55) au kwa lazima (miaka 60) au pale anapopata ulemavu wa kudumu.

Nimeomba kupatiwa ushauri na usaidizi wa kisheria kwa mujibu wa Kanuni ya 21 (1) (d), (e) na (2) ili kuweza kuandaa Muswada Binafsi wa Sheria kwa mujibu wa Kanuni ya 81 (1), Taarifa ya Muswada huo kwa mujibu wa Kanuni ya 81 (2), hati ya kuwasilisha muswada kwa dharura na hoja ya kutengua masharti kuhusu muda wa utangazaji wa Miswada ya Sheria kwa mujibu wa Kanuni ya 81 (5) ya Kanuni za Kudumu za Bunge (Toleo la Mwaka 2007).

Kwa mujibu wa Kanuni ya 81 (5) masharti kuhusu muda wa utangazaji wa Miswada ya Sheria yanaweza kuwekwa kando na kutenguliwa kwa hoja kutolewa na kuamuliwa kama kutawasilishwa Bungeni hati iliyowekwa saini na theluthi mbili ya Wajumbe wote wa Kamati kama ni Muswada wa Kamati na kwa Muswada wa Mbunge hati iliyowekwa saini na Wabunge wasiopungua kumi inayoeleza kuwa muswada binafsi uliotajwa katika hati hiyo ni wa dharura.

Naomba kutoa taarifa kwamba kuanzia jumatatu tarehe 6 Agosti 2012 nitaanza kukusanya saini za wabunge wanaounga mkono kuwasilishwa kwa muswada tajwa kwa hati ya dharura kufanya haraka marekebisho yenye kuwezesha kurejeshwa kwa fao la kujitoa (withdrawal benefits) ili kuruhusu kuendelea kutolewa kwa mafao kwa mwanachama wa mfuko ya hifadhi ya jamii.

Nimeomba pia kwa Katibu wa Bunge kwa mujibu kifungu cha 10 cha Sheria ya ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge Cap 296 R.E 2002 kupatiwa nakala ya taarifa na nyaraka zifuatazo kwa ajili ya kujiandaa kuwasilisha muswada husika: Social Security Ammendment Act no.5 ya mwaka 2012, Sheria za Hifadhi ya Jamii zinazohusika, Taarifa na mapendekezo yaliyowasilishwa na kupelekea kufutwa kwa mafao ya kujitoa (withdrawal benefits) na maelezo kuhusu hatua ambayo kifungu husika kiliingizwa na hatimaye kupitishwa na Bunge tarehe 13 Aprili 2012.

Pamoja na kuomba taarifa na nyaraka kupitia kwa Katibu wa Bunge natoa mwito kwa wadau wa mifuko ya hifadhi ya jamii kutunipatia maoni na mapendekezo kwa ya kuzingatiwa kwenye Muswada Binafsi wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Sheria za Hifadhi ya Jamii (The Social Security Laws (Ammendments) Act wa mwaka 2012 katika kipindi cha wiki moja.

Ikumbukwe kwamba kifungu cha kufuta mafao ya kujitoa kilichozua mgogoro hakikuwepo wakati muswada uliposomwa kwa mara ya kwanza bungeni tarehe 1 Februari 2012 bali kiliwasilishwa kupitia jedwali la marekebisho ya Wizara lililowasilishwa tarehe 13 Aprili 2012 bila malengo na madhumuni yake kuelezwa kwa ukamilifu.

Kupitishwa kwa kifungu hicho kumethibitisha maneno niliyoyatoa bungeni kuwa tumefika hapa tulipo kutokana na ‘uzembe wa bunge na wabunge’ na kwa hili pamoja na mchango nilioutoa bungeni kwa maandishi siku hiyo juu ya haja ya kuwa mfumo mpana zaidi wa pensheni na hifadhi ya jamii (universal pension and social security) pamoja na kuwa sikuunga mkono kifungu husika kilichoingizwa kinyemela naomba radhi kwa wananchi wa Ubungo na wafanyakazi kwa kutokuwasilisha jedwali la marekebisho kupinga kifungu hicho kuingizwa.

Izingatiwe kuwa ili kurekebisha hali hiyo tarehe 27 Julai 2012 kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa Nishati na Madini kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani niliitaka Serikali itoe maelezo maelezo kuhusu taarifa zilizotolewa bungeni tarehe 13 Aprili 2012 kuwa wafanyakazi ikiwemo wa migodini kupitia vyama vyao walihusishwa kutoa maoni yaliyopelekea kufutwa kwa fao la kujitoa (withdrawal benefits); suala ambalo Chama Cha Wafanyakazi wa Migodini (TAMICO) kililikanusha.

Hata hivyo, Waziri wa Nishati na Madini wakati wa majumuisho ya Hotuba yake tarehe 28 Julai 2012 hakutoa majibu yoyote bungeni kuhusu suala hilo hali ambayo imesababisha migongano kuendelea katika migodi mbalimbali kuhusu madai hayo hali ambayo kwa taarifa nilizozipata tarehe 1 na 2 Agosti 2012 inaweza kusababisha migomo migodini. Kufutwa kwa fao la kujitoa kumelalamikiwa pia na wafanyakazi na wadau wa hifadhi ya jamii katika Jimbo la Ubungo na katika taifa kwa ujumla.

Hata hivyo, suala hili na tukio husika litumike kama rejea ya bunge na wabunge kuikatalia Serikali kuwasilisha marekebisho yenye athari kubwa kipindi cha mwisho na hivyo wabunge kukosa fursa ya kupata maoni ya wananchi na pia Serikali itakiwe kuomba radhi kufuatia kulipotosha bunge kuwa wadau wa hifadhi ya jamii hususan wafanyakazi na vyama vyao walishirikishwa na kuridhia wakati ambapo wamejitokeza na kukanusha madai hayo yaliyotolewa na Wizara bungeni.

Kwa upande mwingine kufutwa kwa mafao ya kujitoa msingi wake haupo kwenye marekebisho ya sheria yaliyofanyika tarehe 13 Aprili 2012 pekee bali ni udhaifu katika mfumo mzima wa kisera na kisheria wa hifadhi ya jamii nchini hali ambayo inahitaji wadau kutaka mabadiliko makubwa.

Hivyo, naungana na wote wenye kutaka Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) kutengua taarifa kwa umma iliyotolewa ya kueleza kuwa “kufuatia kuanza kutumika kwa Sheria hiyo (ya 13 Aprili 2012) maombi mapya ya kujitoa yamesitishwa kwa kipindi cha miezi sita hadi pale miongozo itakapotolewa ili kuwezesha Mamlaka na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kutoa elimu kwa Wadau”.
Aidha, pamoja na Mamlaka kueleza kwamba sitisho la fao la kujitoa si kwa sababu za Kiserikali au Mifuko kufilisika ni vizuri mamlaka ikaeleza kwa uwazi na ukweli sababu zingine za kufanyika kwa marekebisho hayo zaidi ya ile ya kutimiza malengo ya Hifadhi ya Jamii ambayo ni kuhakikisha kuwa Mwanachama anapostaafu anapata mafao bora yatakayomwezesha kumudu hali ya maisha ya uzeeni. Tahadhari za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika taarifa za Hesabu za mwaka 2010/2011 na miaka mingine zinaashiria masuala ya ziada ambayo yanaweza kuwa yameisukuma Serikali kuja na mbinu zingine za kuhakikisha uendelevu wa mifuko ikiwemo kupitia marekebisho ya sheria za hifadhi ya jamii.

Ili bunge liweze kutimiza wajibu wa kuishauri na kuisimamia serikali kufanya marekebisho yanayostahili ya sheria husika kwa haraka ni muhimu ratiba ya bunge ikabadilishwa.

Tafsiri ya marekebisho ya ratiba yaliyofanyika ni kuwa hoja binafsi niliyoiwasilisha kwa katibu wa Bunge kutaka bunge lijadili na kupitisha maazimio ya hatua za haraka za kuboresha upatikanaji wa majisafi na ushughulikiaji wa majitaka haitapata nafasi ya kujadiliwa bungeni. Aidha ratiba hiyo mpya hoja binafsi iliyoelezwa kuwa itawasilishwa na Mbunge wa Kisarawe Seleman Jafo kuhusu kufutwa kwa mafao ya kujitoa kufuatia marekebisho ya sheria za Hifadhi za Jamii nayo haitawasilishwa kwenye mkutano huu wa Bunge unaoendelea kama ratiba haitafanyiwa marekebisho.

Hata hivyo, izingatiwe kuwa chanzo cha kufutwa kwa mafao ya kujitoa ni marekebisho ya sheria za hifadhi ya jamii hivyo ufumbuzi wa kurejesha fao la kujitoa unapaswa kuwa ni marekebisho ya sheria hatua ambayo njia ya haraka ya kuifikia ni kuwasilishwa kwa muswada wa sheria ama na serikali au kamati au mbunge badala ya hoja binafsi.

Hoja binafsi inaweza kuwezesha bunge kujadili na kupitisha maazimio ya kuitaka Serikali kuwasilisha marekebisho ya sheria au kuishauri na kuisimamia serikali na mamlaka zake katika utekelezaji wa sheria lakini sheria itaendelea kuwa palepale mpaka marekebisho yatakapofanywa kwa kuwasilishwa muswada wa sheria hatua ambayo nimeamua kuanzisha mchakato wa kuwezesha ichukuliwe.

Wenu katika kuwawakilisha wananchi,

John Mnyika (Mb)


03/08/2012


Bungeni-Dodoma

20 comments:

Dismas said...

Big up kaka

MathiasLyamunda said...

Nimesoma na nimeona jinsi kipengele hicho kilivyochomekwa kwa hila! Endelea kutuwakilisha! I hope watakukubalia maana nahisi haya matekebisho hayakuwekwz kwa bahati mbaya.

Anonymous said...

Asante Mnyika. Hii hoja ni pana zaidi ya kuijadili kwa kuangalia wafanyakazi wa migodini tu kwani inaathiri wafanyakazi wote na hasa wa sector binafsi. Iwasilishe kwa upana huo nasi tupo nyuma yako. Asante sana

Anonymous said...

Yes ni kweli muheshimiwa , tunafanya kazi za mikataba na waajiri wako huru kupunguza watu according to their faida , mafau ya kujitoa yanasaidia saana mtu kuanza na ishu nyingine, mishahara tunayopata haiwekeki kwa kuwa ni midogo na familia za Kiafrica mizigo ya kusaidiana ni mikubwa mno, so hailet sense nikose kazi leo ninamiaka 34 nihangaike mpaka 55, pia hatujawahi kuona wazee wa Nchi hii wakisitiriwa so waache kama ilivyokuwa

Anonymous said...

SERIKALI TUNAOMBA IACHE UNYANGANYI NA KUINGILIA MIFUKO , TUNATOA PAY AS YOU EARN WHAT ELSE THEY WANT ! WAACHE HII MIFUKO IJIENDESHE YENYEWE BILA KUINGILIWA

Unknown said...

pa1 xaana

Unknown said...

hapo bana hiyo sio kodi wala sio nini pesa ya wafanyakazi wenyewe suala la kusema mtu akiacha kazi asubiri mpaka miaka 55 hiyo sio haki kwanza matarajio ya maisha ya mtanzania ni miaka 48 sasa hiyo 55 nani afike??? au ndo wanatafuta njia ya kuzila hizo pesa kama mababu zetu tunavyowaona wanaangaika kuzifuatilia?? cc tunaomba waache kama ilivyokua sioni tatizo lolote watafute sector nyingine uko ndo waweke sheria zao za ajabu ajabu hizo...

Anonymous said...

nimeisoma hiyo nia, nimeona kinachojitokeza wazi zaidi ni kuwa wafanyakazi wa migodini ndio wanailalamikia sheria hii. waliosalia wananung'unika tu, hawajaikataa rasmi!

nimeona kuna dalili kuwa serikali imelidanganya bunge, ikiwa wabunge hutakiwa "kuthibitisha" inakuwaje sasa upande wa serikali.

hii mifuko ya jamii imepaswa kuanzishiwa benki i.e nssf bank, ppf bank, n.k, hoja ya kuwakopesha wanachama huko ndiko inaweza kutekelezwa kwa usahihi zaidi.

hii mifuko ya jamii ianzishe mitandao ya kijamii itakayokuwa pamoja na mambo mengine, na jukumu la kuwakutanisha wanachama kwa mijadala inayohusu mifuko husika. kwa maamuzi yoyote makuu sharti ipigwe kura na wanachama itakayopigiwa mtandaoni.

kwa jinsi hiyo tutaepukana na kitisho cha serikali kuifilisi mifuko hii ya jamii

Anonymous said...

Hili ni Suala la kitaalam, Nadhani ingekua bora tukaweka hisia mbali tukafanya utafiti wa kitaalam. Hii ni social security and retirement plan tusipoteze maana yake wala tusiichanganye an savings plan.

Anonymous said...

Mfanyakz anapoacha kaz apewe mafao yake

Anonymous said...

Mfanyakaz ifike mahala amiliki maisha yake na si serkali i control maisha ya mfanykz

Anonymous said...

Mafao hayo ni pesa halali ya mfanyakazi serikali haina mchango wowote kwa hili sasa vp ipangie watu matumizi ya pesa zao?kwa uchache wenu bungeni tunawaelewa na tuwakilisheni.Nature za kazi za mining hasa underground lini utafikia miaka 50?wafanye utafiti wa nature za kazi za watu.Mtu anafanya kazi ktk ujenzi wa barabara na mkataba ni miaka 2 sasa vp akae mpka umri huo?tuangalie na thamani ya pesa yetu inaporomoka kila kukicha.

Anonymous said...

1.Hayo mafao yana tusaidia sisi watoto wa wakulima,tunapanga tufanye kazi kwa muda wa miaka mi wili au mitatu ili hiyo hela ya mafao iweze kukusaidia kulipa ada maaana bodi yenyewe wanatoa 20%.haya ndo yamenikuta mimi nawengine wengi tu tunaitegemea hiyo hela ili tuweze kujiendeleza vinginevyo shule itatushinda.

2.Najiuliza makampuni yenyewe ya magumashi mpaka tufikishe miaka 55 yata kuwepo hayo makampuni?

3.Je,hiyo hela itakua na thamani ileile baada ya miaka 55?

Ki ukweli wame kurupuka na hayo mabadiliko binafsi si yaungi mkono,ninyi kama wabunge tunaomba myapinge ki msingi haya tusaidii bali yana tukanda miza.

Anonymous said...

Mswada na sheria hiyo imelenga kuubeba mfuko wa ifadhi ya jamii wa NSSF. Sababu kubwa nikwambwa serikali ina daiwa sana na mfuko kuo...ukizingatia ujenzi wa UDOM, daraja la kivuko la kigamboni...na miradi minginea mingi.

SASA BASI:

WAFANYKAZI WAWE HURU NA PESA ZAO.wachukue muda wowote watakapohitaji pesa zao.
KILA MTU ABEBE MSALABA WAKE.
SOLIDARITY FOR EVER.

Anonymous said...

haya mafao ni pesa halali ya wafanyakazi,serikali isitake kuiba pesa za watu,patachimbika hooooooooooooooooooo

Mjema Fredrick said...

Kaka nimefurahi sana kuona unawajibika kutuwakilisha bila kuchoka, binafsi nafarijika sana. Mimi kiukweli siitaki hiyo sheria hata kidogo, Nikiwa kama kijana sitarajii kuajiriwa muda wote mpaka nifika miaka 55 lazima niweze kupata pesa zangu wakati naweza kufikiri vizuri na kuweza kujiajiri! Hii serikali inahubiri watu wajiajiri halafu inataka kupokonya pesa zetu kwa kisingizio cha sheria mbovu kama hzo eti inatutunzia mpaka tukiwa wazee, UPENDO HUO SERKALI YA VIONGOZI WABADHIRIFU KAMA HAWA TULIONAO WAMEUTOA WAPI!? Mbona wazee wanadai mafao yao mpaka wanavua nguo haiwaonei huruma, Mimi nasema hivi ni LAANA inawatafuna na wasicheze na hii level ya wafanyakazi maana tumechoka, kodi tunalipa kubwa, bado na pesa yetu ya mafao wanaitaka!? Kaka tuwakilishe vyema tunakuamini na mimi nasema sitarudi nyuma kwenye hili, wale wafanyakazi walio zoea kutishwa na kuogopa nawapa pole! Waache uhuni wa kitoto, huo wizi hata kuku afanyi!

Unknown said...

Nadhani nina haki kuwalaumu wabunge kwa uzembe mnaoufanya pindi mkiwa bungeni hadi sharia zisizo na tija kwa wadau[wapiga kura] zinapitishwa kimyakimya, mfano ni hii ya kung'ang'ania hela ya wafanyakazi wakati wameshawalipa kodi zenu. Sasa hela tuliyojiwekea inakuwaje inatungiwa sheria ya kibabe kwenye nchi inayojiita huru??????/

Zengo said...

Kudhibitisha kuwa hawa watu wanakurupuka ni kuwa, mifuko hii miwili imekuwa ikijitegemea tangu mwanzo, NSSF na PPF ni kwa ajili ya waajiriwa wa mikataba kwenye makampuni binafsi-hawa hawahitaji kabisa hiyo sheria ya SSRA, kwa sababu zifuatazo
1. Kazi zao ni za muda mfupi mfupi na mara nyingi wanahama, kuacha kazi na kufanya shughuli zingine kwa muda kisha kuajiliwa tena.
2. Kazi zao kwa maana ya professional development ni ndogo sana
3. Mishahara yao iko juu kuliko wafanyakazi wa serikalini ambalo ni kundi la pili (generalization)

Kundi lingine ni kundi la PSPF na LAPF, kwa kawaida hawa ni permanent employees ambao kwao, suala la pension limekuwa ni maongezi yao ya kila siku. hivyo sheria hii ambayo inapingana na sheria ya mifuko ya jamii ya mwaka 2001 imetengenezwa kwa ajili ya kulikandamiza kundi la kwanza ambalo ni wengi zaidi. Sijajua kwa mtu aliyeko sekta binafsi anayelipwa kama specialist milioni 12 kwa mwezi atakuja kulipwa kiasi gani baada ya kustaafu kama siyo kupumbazana na kukusanya pesa zetu wakijua kuwa baada ya muda fulani watakuwa wamepata fedha wanazohitaji na baadae kurudisha sheria ya kujitoa ili kuepuka kuwaingiza watu wenye mishahara mikubwa walioko makampuni binafsi kuhangaika kuwalipa pension.

Wito: Nakuomba mheshimiwa ulivalie njuga suala hili. Ukitaka sahihi zetu na majina yetu tuko tayari kujiorodhesha kwa wingi tunaopinga unyanyasaji huu.

Anonymous said...

Asante Mh. Mnyika kwa juhudi zako, lakini nipo na Ombi moja ambalo ni la jinsi Serikali ya CCM inavyotubesha mizigo kwa maslahi ya washikaji wa JK, tumeangalia jinsi Bunge limekuwa la Dili hasa wabunge wa CCM, lakini hizi asante za Mh. Rais zinatuumiza sana kwa mfano kugawa Mikoa na Wilaya mpya ni Upuuzi tu, mfano mm nilikuwa Iringa kutoka Iringa mjini hadi Kilolo km 45, kule kuna Wilaya mpya lakini staff wote wanaishi Mjini, asubuhi wanawasha DFP Kilolo mchana Town hadi gari ya Polisi na Ocd Maskani yao Ilula, hizi huduma wanapata mjini kama ni hivyo kulikuwa na sababu gani ya kufungua hiyo wilaya kama si kupeana ASANTE?! Mishahara ya hawa Staff ni kodi zetu NAOMBA UFANYIKE UTAFITI KHS HIZI ASANTE KIKWETE, MTU KASHINDWA KUINGIA BUNGENI ANATAFUTIWA UKUU WA WILAYA AU MKOA SI SAWA.

Unknown said...

Tuingie barabarani kama watazingua mana hapa nilipo sina ajira mkata umeisha nasubiri maamuz ya watu ambao ckutafuta nao pesa natukanwa na mzungu kila asubuhi then my fellow black people nao waweka sheria pesa yangu ipo cku tutachoka hakuna asio penda kukaa ofcn