Tuesday, August 21, 2012

Taarifa Fupi kuhusu Kazi za Maendeleo Jimboni Ubungo (AMUA)


UTANGULIZI:
Kwa nyakati mbalimbali kumekuwepo na mijadala kwenye mitandao ya kijamii kuhusu utendaji kazi wangu katika kuwezesha maendeleo Jimboni Ubungo. Mijadala hiyo imeshika kasi jana tarehe 20 Agosti 2012 siku nzima baada ya habari kwenye ukurasa wa mbele wa gazeti la Tanzania Daima “Mnyika kinara bungeni” ambayo imerejea rekodi za bunge na kuniweka katika orodha ya wachangiaji wa mara kwa mara bungeni.

Napokea kwa unyenyekevu pongezi zilizotolewa na wachangiaji mbalimbali lakini izingatiwe kuwa michango yangu bungeni ni matokeo ya heshima mliyonipa ya kuwawakilisha. Aidha yapo maoni machache ambayo yametoa tafsiri tenge kuhusu kazi ya mbunge na wengine mmetaka nieleze nimefanya kazi gani za maendeleo jimboni Ubungo.

Tarehe kama ya leo 21 Agosti 2005 nilianza mchakato wa kuwa kugombea ubunge nikiwa kwenye chakula na watoto yatima, tarehe kama hiyo mwaka 2010 nilianza kampeni za uchaguzi mitaani Ubungo, tarehe hii hii kwa mwaka huu wa 2012 naomba niitumie kutoa taarifa fupi ya utekelezaji kwa masuala ya maendeleo katika mwaka wa fedha 2011/2012 uliomalizika tarehe 30 Juni 2012; taarifa ya kina ya utekelezaji nitaitoa nitakapotimiza miaka miwili ya utendaji.

AHADI NILIZOTOA WAKATI WA UCHAGUZI WA MWAKA 2010
Kabla ya kueleza kazi nilizofanya katika kutimiza majukumu ya kibunge katika kuwezesha maendeleo jimboni ni muhimu nikawapa rejea ya ahadi nilizotoa wakati wa uchaguzi wa mwaka 2010 ili kupata msingi  wa kupima utekelezaji.

Wakati wa kampeni nilitoa ahadi chache na kuelekea mwishoni mwa kampeni niliorodhesha ahadi zote na kuziweka kwenye maandishi ikiwa ni mkataba kati ya mbunge na wananchi wa kutumika kama rejea katika kipindi cha miaka mitano ya utumishi 2010 mpaka 2015.

Ahadi hizo ziko katika kipeperushi cha AMUA ambacho tulikisambaza kwenye kaya mbalimbali jimboni wakati wa kampeni, ahadi hizo nilizirudia mara baada ya kuchaguliwa na zinapatikana hapa:  http://mnyika.blogspot.com/2010/11/ujumbe-wa-mbunge-shukrani-twende-kazi.html

UTEKELEZAJI KATIKA KIPINDI CHA MWAKA MMOJA NA NUSU
Toka kuapishwa mwezi Novemba 2010 mpaka mwezi Juni 2012 ni takribani mwaka mmoja na na miezi tisa  ya kuwatumikia wananchi wa Ubungo kwa nafasi niliyochaguliwa ya mbunge wa Ubungo; hizi ni baadhi katika orodha ya za maendeleo ambazo nimeshiriki jimboni:

ELIMU:
Akili na vipaji ambavyo kila mwanadamu amejaliwa ndiyo mtaji mkuu wa kujikwamua kimaisha. Katika muktadha huo katika kipindi husika nimesimamia yafuatayo kuwezesha elimu bora:

Mbunge amefuatilia kupitia vikao vya manispaa ya Kinondoni na kupitia ziara jimboni, maswali bungeni ili kuhakikisha ruzuku ya bajeti ya elimu kwa wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari, inafika na kuboresha upatikanaji wa vifaa vya elimu na huduma zingine za muhimu katika Jimbo la Ubungo, katika mwaka 2012/2013 nitafuatilia kwa karibu zaidi kasoro zilizobainika katika mwaka 2011/2012 .

Katika kipindi husika mbunge ameendelea kutetea haki na maslahi ya walimu na wanafunzi wakiwemo wa elimu ya juu wa Jimbo la Ubungo. Aidha, nimeshiriki katika kuwezesha uamuzi wa kuhamisha fedha katika mafungu mengine yasiyokuwa ya lazima kuelekeza katika matengenezo ya madawati kwa shule za msingi na sekondari ambapo zaidi ya madawati 7,000 yamesambazwa katika Jimbo la Ubungo kutoka Manispaa ya Kinondoni, Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo (CDCF) na kutoka Sekta Binafsi. Kwa ushirikiano na madiwani tumefuatilia kuhakikisha mgawo wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa madarasa na vyoo katika shule za msingi na sekondari katika kata mbalimbali kutoka katika Manispaa ya Kinondoni na Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo (CDCF), orodha ya shule na viwango vya fedha vilivyotumika inaweza kupatikana katika Ofisi ya Mbunge. 

Mbunge amependekeza sehemu ya fedha za mfuko wa kuchochea maendeleo ya jimbo (CDCF) kutumika kutoa elimu maalum ya kuwawezesha wananchi kujua haki zao, fursa zilizopo na namna ya kujiendeleza,   haswa kwa akina mama, vijana na walemavu. Mfano; haki za mirathi kwa wajane na kukuza vipaji kwa vijana. Hata hivyo, utekelezaji wa kazi hii haukuwezekana kwa kutumia CDCF kwenye mwaka wa fedha 2011/2012 kutokana na utata kuhusu tafsiri ya shughuli za kuchochea maendeleo zinazoweza kutengewa fedha kutoka kwenye mfuko, hivyo shughuli hiyo itazingatiwa kwa ukamilifu kwenye mwaka wa fedha 2012/2013 baada ya kibali kupatikana.

Ili kuziba pengo nje ya CDCF katika mwaka 2011/2012 kupitia ofisi ya mbunge Ubungo na Asasi ya Maendeleo Ubungo (UDI) tumefanya programu ya “Toa Kitabu Kisomwe” na pia kuunganisha vijana na wanawake na elimu maalum kupitia taasisi zingine.

Mbunge amechangia asilimia 20 (20%) ya mshahara wake kwa mwezi kwenye masuala mbalimbali ya elimu, orodha ya baadhi ya michango kwa shughuli za elimu kwa wanafunzi na walimu wa msingi, sekondari na vyuo inaweza kurejewa katika Ofisi ya Mbunge (majina ya waliopewa michango yamehifadhiwa kulinda faragha).

Kazi hizi zitapanuliwa zaidi katika mwaka wa fedha 2012/2013 kupitia Mfuko wa Elimu Ubungo tutakaouzindua karibuni.

AJIRA: 
Katika kuwezesha upatikanaji wa mitaji kwa vijana na wanawake kuweza kujiajiri mbunge alifanikiwa kushawishi Manispaa ya Kinondoni kuongeza fedha za mikopo kwa vikundi vya kina mama na vijana ambapo awali zilikuwa zikitengwa milioni 20 tu, na hivyo milioni zaidi ya 200.

Orodha ya vikundi vilivyopatiwa mikopo na mitaji mpaka sasa katika Jimbo la Ubungo inapatikana kwenye Ofisi ya Mbunge. Aidha, mbunge ametetea wafanyabiashara wadogo kuendelea kutengewa maeneo ya biashara na katika mwaka 2011/2012 amewezesha kamati maalum inayohusisha wafanyabiashara na Manispaa kuundwa kwa ajili ya kuwezesha wafanyabiashara wa Ubungo kupatiwa maeneo katika masoko yaliyotengwa. Katika mwaka 2012/2013 hatua zitaendelea kuchukuliwa kwa ajili ya wafanyabiashara ndogo ndogo ambao hawajapata maeneo mpaka sasa.

Mbunge amefanya ziara ya kikazi katika kiwanda cha nguo cha Urafiki ili kuzungumza na wafanyakazi na menejimenti katika kuisimamia serikali kushughulikia matatizo yaliyojitokeza katika kiwanda na kuathiri ajira na ujira bora. Matokeo ya ziara ya mbunge na ufuatiliaji bungeni yamefanya kiwanda hicho kutembelewa pia na kamati ya bunge na mawaziri husika ambapo hatua zimeanza kuchukuliwa, katika mwaka wa fedha 2012/2013. Mbunge ataendelea kufuatilia kwa karibu matatizo yanayoendelea kuhusu ufisadi na uwekezaji katika kiwanda husika.

Aidha, mbunge amefuatilia pia masuala ya ajira katika viwanda vilivyofunguliwa kwenye maeneo ya uwekezaji wa kiuchumi (EPZ/SEZ) yaliyopo katika jimbo la Ubungo ikiwemo kutaka kutengwa kwa maeneo maalum ya wawekezaji wadogo.

Katika kupanua wigo wa ajira mbunge amefuatilia pia kuhusu viwanda vingine vilivyobinafsishwa au kuuzwa miaka ya nyuma katika Jimbo la Ubungo mathalani Ubungo Garments;  Ubungo Spinning Mill;  Polysacks Ltd; Tanzania Sewing Thread; Coastal Diaries (Maziwa) na  Kiwanda cha Zana za Kilimo (UFI); na hatimaye serikali imemjibu kuwa waraka utawasilishwa kwenye baraza la mawaziri ili kurejesha viwanda vilivyodidimizwa kinyume cha masharti ya mikataba. Katika utekelezaji wa hatua hiyo, mbunge amependekeza kuwa miongoni mwa maeneo ya viwanda yatakayorejeshwa kutengwe eneo maalum kwa ajili ya wenye viwanda vidogo vidogo katika jimbo la Ubungo ili kupanua wigo wa ajira hususan kwa vijana katika mwaka wa fedha 2012/2013.

Mbunge ameunga mkono jimboni na ndani ya bunge madai ya ujira bora na stahili za wafanyakazi wa sekta ya umma na binafsi kama walimu, madaktari/manesi, polisi, madereva nk. Hata baada ya nyongeza ndogo ya mishahara iliyopatikana kufuatia shinikizo la migomo kutoka vyama vya wafanyakazi, mbunge ataendelea kuungana na wafanyakazi na wabunge wengine katika kutaka kuboreshwa kwa maslahi ya wafanyakazi na mazingira ya utoaji huduma hususan katika sekta za elimu, afya, usalama na mahakama. Katika ya masuala ambayo aliyapata kipaumbele katika mwaka wa fedha 2011/2012 ni nyongeza ya posho ya lishe (rationing allowance) kwa askari polisi kutoka laki moja mpaka laki moja unusu suala ambalo serikali imelitekeleza katika bajeti ya mwaka wa fedha 2012/2013.

MIUNDO MBINU:
Msimamo wangu katika kipindi chote umekuwa kwamba pamoja kuunga mkono uwekezaji kwenye upanuzi wa barabara kuu, ujenzi wa miundombinu ya mradi wa mabasi yaendayo haraka na ujenzi wa fly overs, miradi hii kwa ujumla wake iliyotengewa zaidi ya bilioni 240 inachukua muda wa kati na muda mrefu hivyo kukamilika kwake ni mpaka mwaka 2015 au zaidi. Hivyo ili kupunguza msongamano katika barabara kuu ya Morogoro, pamoja na mbinu zingine mbunge amekuwa mstari wa mbele kutaka barabara za pembezoni zijengwe kwa haraka; hatimaye baada ya ufuatiliaji wa mara kwa mara kupitia ziara jimboni, vikao vya manispaa, vikao vya bodi ya barabara, ziara jimboni, mawasiliano kwa barua na mamlaka husika na kuhoji bungeni Serikali imekubaliana na mapendekezo tuliyowasilisha hivyo maamuzi yamefikiwa kuwa barabara husika zihudumiwe na Serikali kuu (TANROADS) badala ya Manispaa.

Jumla ya shilingi bilioni 10.5 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara zifuatazo:  Mbezi Luis kupitia Goba mpaka Mbezi Tangi Bovu; Mbezi kwa Yusuph- Msakuzi- Mpiji Magohe mpaka Tegeta/Bunju; Mbezi-Malambamawili-Kinyerezi, Kimara-Mavurunza-Bonyokwa; Ubungo Maziwa-External, Kimara-Kilungule-Makoka-Makuburi, Kimara-Matosa-Mbezi; Ubungo-Msewe-Chuo Kikuu na nyingine katika maeneo mengine.

Katika mwaka wa fedha 2012/2013 Mbunge ataendelea kuisimamia serikali ili itenge bilioni 100 kujenga kwa kiwango cha lami barabara tajwa za pembezoni za kupunguza msongamano haraka zaidi na pia kuboresha usafiri wa maeneo ya pembezoni kwa kuwa baadhi ya barabara hizo zilitengenezwa kwa kiwango cha changarawe kwenye mwaka wa fedha 2011/2012 lakini zimeharibika tena baada ya mvua zilizonyesha katika jiji la Dar es salaam.

Katika mwaka wa fedha 2011/2012 tumefuatilia madaraja mbalimbali kujengwa ikiwemo Daraja Golani, Msewe, Matosa nk pia kupitia mfuko wa maendeleo ya Jimbo (CDCF) vivuko kwa watembea kwa miguu vimejengwa Makurumla na Msigani; orodha zaidi ya matengenezo ya barabara yaliyofanyika inaweza kurejewa katika Ofisi ya Mbunge.

Kufuatia ufuatiliaji wa karibu kwa njia mbalimbali hatua imechukuliwa ya kupeleka umeme katika eneo la Goba Matosa (hata hivyo bado kuna malalamiko ya eneo lilirukwa la Mgeni Chongo) ambalo tunaendelea kufuatilia.

Aidha, miradi iliyokuwa imekwama kwa muda mrefu ya kupeleka umeme katika miradi ya maji ya King’ongo na Kilungule inaendelea kutekelezwa kwa haraka zaidi. Mbunge amefuatilia mara kwa mara ahadi ya Rais ya kupunguzwa kwa gharama za umeme na hatimaye ahadi imetolewa ya utekelezaji kuanza kuanzia Januari 2013, pia kanuni za Februari 2011 zimetungwa kuhusu kurejeshwa kwa gharama kwa wateja wanaolazimika kuvuta umeme zaidi ya umbali wa kawaida.

Katika mwaka 2012/2013 mbunge ataendelea kuisimamia serikali kurekebisha kanuni hizo kwa kuwa zina vifungu visivyotekelezeka na kutaka pia gharama za nguzo na nyinginezo ziwekwe kwenye bili ya mteja kama umeme uliolipiwa kabla. Orodha ya maeneo mengine katika Jimbo la Ubungo ambayo ufuatiliaji umefanyika kuhusu kusambaziwa umeme inapatikana katika Ofisi ya Mbunge.

MAJI:
Katika kufuatilia masuala ya maji nilianza kwa kufanya Kongamano la Maji katika Jimbo la Ubungo mwanzoni mwa mwaka 2011 ili kuwakutanisha wananchi, mamlaka husika na wadau wengine katika kuunganisha nguvu kupata ufumbuzi.

Hatua nyingine zote nilizochukua baada ya hapo zilikuwa ni za ufuatiliaji kuwezesha utekelezaji wa haraka. Nikiri kwamba katika hatua za awali ushirikiano kutoka DAWASA, DAWASCO na Wizara ya Maji ulikuwa mdogo kwa kiwango cha kuamua kuwaunganisha wananchi kupitia ‘maandamano ya maji’ kwenda DAWASCO. Toka wakati huo ushirikiano umeongezeka kwa upande wa DAWASCO ambapo nimeshafanya nao ziara ya kikazi ya kata mbalimbali ya kutembelea maeneo yenye matatizo na hatua zimechukuliwa ambazo zimewezesha baadhi ya maeneo kuanza kutoka maji.

Pia, wakati wa hatua hizo nimewaonyesha DAWASCO biashara haramu ya maji iliyokuwa ikiendelea na baadhi ya maeneo wamechukua hatua ikiwemo kwa watendaji wao. Hata hivyo, udhaifu wa kimfumo uliopo ni mkubwa kuliko hatua ambazo zimeweza kuchukuliwa mpaka sasa. Katika mazingira hayo nilianza pia kutaka hatua za DAWASA na tayari nao nimefanya nao ziara ya kikazi kwenye vyanzo vya maji pamoja na matenki ya maji, na kutaka hatua za haraka za ushirikiano kati ya DAWASA na DAWASCO.

Kwa maana ya miradi ya muda mrefu ya mwaka 2013/2014 kumetengwa fedha kuanzia mwaka 2012/2013 zaidi ya bilioni 200 kutokana na fedha za MCC na Mkopo wa India kwa ajili ya upanuzi wa vyanzo vya Ruvu Juu na Ruvu Chini, ujenzi wa Bwawa la Kidunda na ujenzi wa mabomba mengine miradi ambayo itagusa wananchi wa Ubungo. Hata hivyo, hatua hizi za muda mrefu hazileti matumaini bila hatua za haraka ambazo zilipaswa kuchukuliwa katika mwaka wa fedha 2011/2012.

Katika kuwezesha hatua za haraka kwa mwaka wa fedha 2011/2012 nilifuatilia ratiba ya mgawo wa maji kuweza kutolewa kwa mbunge na kwa ngazi za kata na mitaa na kufuatiliwa ili mgawo uwezeshe kuheshimiwa bila ya upendeleo wa baadhi ya maeneo au hujuma kwa ajili ya kuwezesha biashara haramu ya maji. Ofisi ya mbunge wakati wote imetaka kupatiwa taarifa pale mamlaka husika au ngazi tajwa zinaposhindwa kufuatilia ratiba husika ili kuweza kuingilia kati. Kuanza kuweka miundombinu ya maji katika maeneo yaliyorukwa kwenye awamu ya kwanza ya uwekaji wa mabomba, tayari utekelezaji umeshaanza katika maeneo ya Mbezi na maeneo mengine utafanyika kuanzia mwanzoni mwa mwaka 2013 kwa mujibu wa ahadi zilizotolewa na DAWASCO/DAWASA kwa mbunge.

Katika kutekeleza ahadi ya kuhamasisha ujenzi wa visima kwenye maeneo ambayo hayafikiki kirahisi na mtandao wa maji ya bomba kama suluhisho la muda, huku tukifuatilia ufumbuzi wa kudumu katika maeneo hayo, mbunge amefuatilia uchimbaji wa visima uliokuwa umesimama katika maeneo ya Mavurunza/Bonyokwa, Kilungule na King’ongo kwa kwenda maeneo husika, kuziandikia mamlaka zinazohusika na kuhoji kwenye vikao vya manispaa, bungeni na kufanya ziara za ukaguzi wa maendeleo ya miradi.

Uzinduzi kwa miradi ya Mburahati ulifanyika mwanzoni mwa mwaka 2011 na hatimaye sasa uzinduzi wa maeneo yaliyotajwa utafanyika katika mwaka huu wa 2012 kwa kuratibiwa na DAWASA na Wizara ya Maji.

Aidha, uchimbaji wa visima kama hivyo unaendelea katika maeneo ya Saranga na Malambamawili. Aidha, kupitia miradi ya Manispaa ikiwemo mradi unaofadhiliwa na benki ya dunia mbunge amefuatilia uchimbaji katika maeneo ya Mpiji Magohe, Msakuzi, Makoka na Msumi ambao unasuasua kutokana na udhaifu wa kiutendaji.

Mbunge ameunga mkono jitihada zinazofanywa na wadau wengine wa maendeleo Jimboni Ubungo katika masuala ya maji hususani Shirika la Kibelgiji (BTC) katika maeneo ya Kwembe na Kibamba na amewasiliana na DAWASA/DAWASCO kwa ajili ya hatua za kusaidia miradi husika na TANESCO kwa upande wa kuweka transfoma yenye uwezo mkubwa zaidi ili kuwezesha pampu za maji kwenye maeneo husika ziweze kufungwa. Orodha ya maeneo mengine yaliyochimbwa visima vidogo ipo katika Ofisi ya Mbunge.

Mbunge amefanikiwa kufanya suala la maji kuwa moja ya masuala yanayojadiliwa mara kwa mara kwenye vikao vya Manispaa ya Kinondoni hali ambayo haikuwepo kabla. Aidha alipendeza na hatimaye ukafanyika ufuatiliaji wa miradi iliyo chini ya jamii au mamlaka za ngazi ya chini iliyokwama kwa muda mrefu na hivyo kukosesha wananchi maji katika maeneo mbalimbali ambayo hayapewi huduma ya moja kwa moja na DAWASA/DAWASCO. Kati ya miradi hiyo baadhi imefufuliwa kama wa Msewe Golani na mingi inaendelea kusuasua ikiwemo ya kata ya Goba. Mbunge amependekeza kwa DAWASA kwamba maeneo ambayo hayakuwa yakihudumiwa na DAWASCO ikiwemo ya kata ya Goba yachukuliwe moja kwa moja na mamlaka husika kwa kuwa kutokana na ongezeko la watu maeneo hayo hayawezi kuhudumiwa kwa ufanisi na kamati za maji kama ilivyokuwa miaka ya zamani.

Mbunge amefuatilia pia masuala ya bei na ubora wa maji na kuitaka bei ya maji inayotozwa kwenye Viosk inaendana na viwango vilivyopangwa na mamlaka husika (EWURA), kufuatia hatua hizo operesheni zimefanyika katika maeneo ambayo yanatoza maji kinyume na bei iliyotangazwa na DAWASCO imeingia mikataba na waendeshaji wa vioski husika kuhusu bei elekezi. Hata hivyo, changamoto imeendelea kuwa ni usimamizi wa utawala wa sheria katika kuhakikisha bei inayotozwa ni ile inayopaswa kutoswa kwa mujibu wa maagizo ya EWURA. Katika kipindi husika mbunge ametaka pia EWURA itoe bei elekezi kwa upande wa maji katika jiji la Dar es salaam kwa upande wa sekta binafsi ili kudhibiti pia biashara holela ya maji ya kwenye malori. Katika mwaka wa fedha 2011/2012 EWURA iliahidi kutoa kanuni za kudhibiti biashara husika hatua ambayo mpaka sasa haijachukuliwa, suala ambalo mbunge atalifuatilia katika mwaka wa fedha 2012/2013.

UWAJIBIKAJI:
Mbunge amekuwa mstari wa mbele katika kupambana na ufisadi na matumizi mabaya ya fedha ngazi mbalimbali ili kuchangia katika  kuhakikisha fedha nyingi zinazopatikana kila mwaka zinatumika kuwahudumia wananchi, ikiwemo kwa kutaka kushughulikiwa kwa mapungufu yaliyoanishwa na wakaguzi wa hesabu katika vipindi vilivyopita. Mathalani mbunge amefuatilia utekelezaji wa mapendekezo ya Ukaguzi Maalum (Special Audit) ya Kituo cha Mabasi cha Ubungo uliofanyika mwaka 2009 lakini utekelezaji wa matokeo ulikuwa ukisuasua. Alifanya hivyo kupitia bungeni na katika vikao vya halmashauri ya Jiji la Dar es salaam na hatimaye baadhi ya mapendekezo yametekelezwa ikiwemo kumwondoa mkandarasi aliyekuwa akikusanya mapato chini ya kiwango; aidha mbunge ataendelea kufuatilia mapendekezo mengine kuhusu mikataba mibovu iliyoingiwa katika kituo husika.

Mbunge amefanya hivyo vile vile kuhusu vitega uchumi vingine vya Jiji la Dar es salaam ikiwemo Shirika la Usafiri Dar es salaam (UDA). Aidha, kwa kushirikiana na madiwani amefuatilia pia miradi hewa au ya chini ya kiwango iliyofanyika katika miundombinu, elimu na maji na hatua mbalimbali zimechukuliwa kama zinavyoelezwa katika Taarifa za Ofisi ya Mbunge.

Mbunge kupitia uwakilishi bungeni na kupitia hatua zingine nje ya bunge amezifuatilia mamlaka za serikali kuhusu masuala mbalimbali yanayowagusa wananchi wa Ubungo, mathalani EWURA katika nishati/mafuta, SUMATRA katika usafiri na TANESCO katika umeme.

Katika mwaka wa fedha 2012/2013 mbunge atafanya ziara za kikazi pamoja na mamlaka husika katika maeneo mbalimbali yenye kero ili kuziwezesha kuendelea kuchukua hatua zaidi kuhusu maeneo hayo kwa ajili ya kuchangia katika maendeleo ya wananchi na nchi kwa ujumla.

Mbunge amefanya mikutano na wananchi katika kata zote 14 za Jimbo la Ubungo kwenye maeneo mbalimbali ya kiserikali na ya kichama kwa ajili ya kutimiza wajibu wa uwakilishi kabla na baada ya vikao vya bunge.

Aidha mbunge ameshiriki katika mikutano ya wakazi ya masuala ya maendeleo jimboni kama ambavyo imetajwa katika Taarifa ya Utendaji. Mbunge amewezesha ofisi ya mbunge kuwa vitendea kazi pamoja na wasaidizi wawili wakati wote baada ya kukwama kupata vifaa kutoka kwenye mfumo wa kawaida wa kiserikali.

Aidha, katika mwaka wa fedha 2011/2012 maombi ya mbunge kupata ofisi ya kutumia jimboni kutoka kwenye majengo ya manispaa au ya wilaya yalikataliwa na katika mwaka 2012/2013 mbunge ataweka mkazo katika kufuatilia eneo kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya mbunge.

Aidha, mbunge amewajibika katika kuisimamia serikali bungeni na kushiriki katika kutunga sheria. Rejea katika ofisi ya Mbunge kuhusu kazi za mbunge bungeni inaeleza masuala ambayo mbunge ameisimamia serikali bungeni, hatua zilizochukuliwa na serikali kupitia mchango wake na pia sheria ambazo amewasilisha majedwali ya marekebisho katika vifungu mbalimbali vilivyokubaliwa na vilivyokataliwa.

USALAMA:
Mbunge amechangia katika harambee ya ujenzi wa Kituo cha Polisi Mavurunza ambapo vifaa vya awali vilichangiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo (CDCF) lakini pia fedha taslimu zilichangwa na mbunge kutoka mfuko wake binafsi. Aidha, kupitia CDCF mbunge amechangia pia kwenye ujenzi wa Kituo kidogo cha Polisi Golani Msewe na pia kituo cha Polisi Kata ya Sinza.

Pia, mbunge ameanza ufuatiliaji wa ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Kimara katika eneo lenye nafasi tofauti na eneo la sasa la barabarani la Mbezi kwa Yusuph; kufuatia ufuatiliaji wa mbunge tayari Wizara ya Mambo ya Ndani imeiandikia barua Manispaa ya Kinondoni kuomba eneo.

Kadhalika, mbunge amefuatilia kuhusu eneo la ujenzi wa kituo cha Polisi kata ya Goba ambapo kwa mujibu wa taarifa toka ngazi ya kata eneo limekwishapatikana. Katika mwaka wa fedha 2012/2013 mbunge ataweka kipaumbele katika kazi ambazo zilianza kwenye mwaka wa fedha 2011/2012 ili ziweze kukamilika.

Mbunge ameshirikiana na polisi na viongozi wa kata/mitaa kufanya harambee kuhakikisha doria inakuwepo ili kupunguza vitendo vya wizi, ukabaji na ujambazi hususani kwenye maeneo yenye vitendo vingi vya uhalifu mathalani ya Kimara B kupitia ulinzi shirikishi na polisi jamii.

Aidha, ili kuwe na mfumo endelevu wa kuhudumia vikundi vya ulinzi shirikishi mbunge alipendekeza kwamba masuala ya ulinzi na usalama kuwa sehemu ya vipaumbele vya maendeleo katika mapato ya ndani ya Manispaa kama ilivyo kwa sekta za elimu, afya, barabara nk. Kwa usimamizi wa Meya pendekezo hilo liliingizwa kwenye baraza la madawani na kutakiwa kutekelezwa kupitia fedha zinazobaki katika kata kutokana na ufanisi katika makusanyo ya ndani ili kuimarisha ulinzi na usalama.

AFYA:
Mbunge aliguswa na kasi ya kupungua kwa fedha za wahisani katika bajeti ya afya kwa masuala ya matibabu kwa wanaoishi na UKIMWI/VVU, Wazee, Walemavu na wagonjwa wa kifua kikuu, hivyo pamoja na kuhoji bungeni na kutaka nyongeza ya bajeti kwenye Wizara ya Afya amechukua hatua jimboni kwenye ngazi ya Manispaa kwa kupendekeza kiwango cha fedha toka vyanzo vya ndani kuongezwa hatua ambayo imeanza kuchukuliwa kwa ajili ya mwaka wa fedha 2012/2013.

Kwa ajili ya afya mazingira mbunge alipendekeza kwamba tathmini ifanyike kuhusu mfumo mzima wa uzoaji taka katika kata mbalimbali za Jimbo la Ubungo na Manispaa ya Kinondoni kwa ujumla kutokana na kukithiri kwa uchafu katika maeneo mbalimbali. Kufuatia pendekezo hilo Meya alifanya mkutano na wenyeviti wa mitaa na watendaji wengine ambapo maazimio ya hatua mbalimbali yalifikiwa ambayo yameboresha uzoaji taka katika maeneo machache. Hata hivyo, matatizo ya uchafu yameendelea katika maeneo mengi, hivyo katika mwaka wa fedha 2012/2013 mbunge ataendelea kuisimamia serikali kuu na serikali za mitaa katika kuchukua hatua kubwa zaidi kuhusu udhaifu wa kimfumo ambao ulishababainishwa tayari unaochangia kasi ndogo ya uzoaji taka ngumu na uondoaji wa maji taka katika Jiji la Dar es salaam.

ARDHI:
Mbunge amefuatilia kwa ajili ya kuhakikisha wananchi wa eneo la Ubungo Maziwa wanapewa fidia stahiki. Aidha, mbunge amefuatilia na hatimaye fidia imeanza kulipwa kwa wananchi eneo la Riverside wanaopaswa kubomolewa kupisha njia mbadala ya kwenda Kibangu.

Hata hivyo, suala la fidia ya ardhi kwa upande wa wananchi wa Kwembe kupitisha ujenzi wa Chuo Kikuu eneo la Mlongazila limekwama kwa Serikali kuchukua msimamo wa kutoa fidia ya maendelezo/mali pekee. Mbunge anaendelea kufuatilia suala hilo katika mwaka wa fedha 2012/2013 kwa kushirikiana na wananchi waliofungua kesi mahakamani wakati utekelezaji wa mradi ukiendelea. Kwa upande mwingine, kiasi cha shilingi bilioni 10 kimeweza kutengwa kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi wa Ubungo walio karibu na mitambo ya umeme ambao walikuwa wanadai fidia toka mwaka 2004.

Mbunge amesisitiza kupitia vikao vya Mkoa, halmashauri ya Jiji, Manispaa na bunge kuhusu haja ya serikali kuweka kipaumbele katika kusimamia mpangilio mzuri wa makazi na kuhamasisha upimaji wa viwanja ili wananchi wapate hati na leseni za makazi kwa urahisi na kwa bei nafuu kutokana na matatizo ya gharama kubwa na ucheleweshaji yaliyoko hivi sasa. Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi amemjibu mbunge kuwa wizara itawekwa mfumo ili hati iwe inatolewa kwa haraka katika muda usiozidi miezi sita. Mbunge amefuatilia mradi wa urasimishaji unaofanywa na Ofisi ya Rais (MKURABITA) katika eneo la Kimara Baruti, aidha mbunge ametaka elimu kutolewa kwa wananchi na madiwani na watendaji wengine kuhusu namna fursa za upimaji na urasimamishaji zinavyoweza kutumiwa katika maeneo yao.

Mbunge amefuatilia vile vile taarifa kuhusu mji wa kiungani (Sattellite town) ya Luguruni na maeneo jirani ya mji huo na kubaini kasoro kama zinavyoelezwa katika Taarifa ya Utendaji, aidha Wizara imeahidi kwamba muendelezaji mwenza wa mji huo amepatikana na kwamba kasoro zinazoendelea zitarekebishwa.

Mbunge amefuatilia kupitia hoja binafsi na maswali katika manispaa na bungeni kuhakikisha viwanja vya umma vilivyouzwa kinyume na taratibu na viwanja vya wazi vilivyovamiwa, vinarejeshwa. Mfano: viwanja vya Makurumla, Sinza, Ubungo, Makuburi, Mbezi nk. Kufuatia hatua hizo, sehemu ya viwanja hivyo imejadiliwa kwenye baraza la madiwani la manispaa ya Kinondoni na pia Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi ametembelea kata ya Sinza na kuweka mabango kwa ajili ya wahusika kubomoa. Katika mwaka wa fedha 2012/2013 mbunge ataendelea kufuatilia kwa karibu ili ubomoaji uanze.

HITIMISHO:
Nihitimishe kwa kurejea msimamo wangu kuhusu kazi za mbunge ambao nimekuwa nao miaka mingi kabla ya kuingia kwenye siasa na niliurudia mwanzoni mwaka 2010 wakati natangaza nia ya kugombea Ubunge:
“Naamini kwamba mbunge (ambaye pia kwa nafasi yake ni diwani katika halmashauri) ana wajibu katika maeneo makuu manne (kwa kadiri ya umuhimu) katika kuwezesha maendeleo Jimboni kwake na kwa taifa kwa ujumla:

Mosi; kusikiliza na kuwakilisha wananchi, Pili; kuisimamia na kuiwajibisha serikali na viongozi wake, Tatu; kushiriki katika kutunga sheria, Nne; kuhamasisha upatikanaji wa huduma.

Hata hivyo, sehemu kubwa ya wabunge wetu hawaweki kipaumbele katika majukumu ya kwanza matatu ambayo ndio msingi wa ubunge wenyewe. Matokeo yake ni matakwa ya wananchi kutokuwakilishwa kikamilifu, ufisadi, rushwa, matumizi mabaya ya madaraka na mikataba mibovu; uwepo wa sheria dhaifu na kutetereka kwa utawala wa sheria na mifumo ya haki masuala ambayo yanakwaza jitihada za maendeleo za wananchi binafsi za taifa kwa ujumla.

Wabunge wengi wanawaza kwamba jukumu kubwa la mbunge ni kutoa bidhaa na huduma kwa wananchi; wakiacha taifa katika lindi la umasikini na kufanya sehemu ya wananchi kujenga mazoea ya kutegemea hisani toka kwa viongozi wa umma na wafadhili wao.

Mwaka 2005 pamoja na majukumu hayo makuu matatu, nilizungumzia suala la mfuko wa maendeleo ya jimbo. Lakini si katika mwelekeo wa mfuko wa sasa uliopitishwa kuwa sheria. Kwa hiyo, wakati nikiunga mkono jukumu la mbunge kuhamasisha maendeleo na kushiriki kwenye shughuli za kijamii, siamini katika mazoea na mfumo wowote unaomfanya mbunge kuwa “mtoa bidhaa na huduma” (mithili ya ATM) kwani unarutubisha ufisadi wa kisiasa na kuhatarisha mwelekeo mzima wa utawala bora. Kama ambavyo siamini pia katika siasa chafu za rushwa, uongo na aina nyingine ya upofu wa kimaadili katika kampeni na uongozi kwa ujumla.

Haiwezekani wakati ambapo makisio yanaonyesha kwamba zaidi ya trilioni mbili (sawa na milioni milioni mbili) zinapotea kila mwaka kupitia misamaha ya kodi, upangaji bei hovyo kwa bidhaa za Tanzania, biashara haramu kati ya Tanzania na nchi za nje au makampuni ya kimataifa halafu wananchi wakubali kupumbazwa na bidhaa za milioni chache zinatolewa na viongozi wa umma walioshindwa kurekebisha hali hii”
, Mwisho wa kunukuu. Msingi wa msimamo huu unaweza kurejewa kwa ukamilifu hapa: http://mnyika.blogspot.com/2010/03/natangaza-rasmi-dhamira-ya-kugombea.html

Hivyo, ufanisi wa ubunge wangu upimwe kwa kuzingatia msimamo huo ambao niliwaeleza wananchi wakati wa uchaguzi hivyo nilichaguliwa ikifahamika wazi kuwa huo ndio wajibu ambao nitautekeleza katika kipindi cha miaka mitano.

Bado naendelea kuamini kwamba jimbo la Ubungo na taifa kwa ujumla tutapiga hatua ya haraka zaidi ya maendeleo kupitia mabadiliko katika mifumo yetu ya mgawanyo wa rasilimali na usimamizi wa matumizi ya fedha za umma na pia kwa kuweka mazingira bora ya kisera, kisheria na kiutendaji wa sekta binafsi.

Tuliyoyafanya mpaka sasa ni sehemu tu katika mahitaji makubwa ya maendeleo kutokana na pengo la miaka 50 ukilinganisha na fursa ambazo taifa letu linazo; hata hivyo naamini miaka mitatu iliyobaki itafanya miaka mitano ya kuisimamia Serikali iliyopo madarakani hivi sasa pamoja na udhaifu wote uliokuwepo kuleta tofauti katika maendeleo majimboni. Ni katika muktadha huo wakati mwingine tunazimika kuwakilisha na kuwasilisha matakwa ya wananchi namna hii: http://www.youtube.com/watch?v=ES4OMOD_xME tukiamini kwamba watawala wenye dhamana kwa sasa ya kukusanya kodi watasikiliza na kuzingatia vipaumbele vya maendeleo vya wananchi.

Aidha, baada ya kazi mkutano wa nane wa bunge naomba kutumia fursa mjadala utakaofuatia taarifa hii kupata maoni yenu kuhusu masuala ninayopaswa kuyapa kipaumbele katika kuwawakilisha na kuwatumikia jimboni katika kipindi cha mwezi Septemba mpaka Oktoba 2012 kabla ya kuanza kwa mkutano wa tisa wa bunge na pia kuhusu maandalizi ya mwaka 2013. Kero nyingi zinazoendelea kuwepo kwa sasa ni neema iliyojificha (blessing in disguise) ili tuendelee kuunganisha nguvu ya umma kuendeleza wimbi la mabadiliko. 

Narudia tena kuwakumbusha kuwa nguvu ile ile tuliyoitumia kwenye kutafuta kura na kulinda kura ndio naiomba toka kwenu katika hatua hii ya kufanya kazi za kuwezesha maendeleo kwa kutimiza wajibu kila mmoja wetu kwa nafasi yake, kuisimamia serikali na kuunganisha rasilimali za wadau wengine; 

Maslahi ya Umma Kwanza.

Nimeandika taarifa hii leo tarehe 21 Agosti 2012 siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwangu.
Wenu katika uwakilishi wa wananchi,

John Mnyika (Mb)
Jimboni-Ubungo





7 comments:

Anonymous said...

Kamanda hongera sana na Mungu akujalie. Napenda sana michango yako yenye mantiki pamoja na utendaji wako Bungeni na Jimboni kwako. Pia naomba umfikishie Mch.Msigwa salaam zangu hasa katika mchango wake alioutoa Bungeni ambao ulitugusa sana sisi wazalendo wa nchi hii. Ule mchango wake ni wa kipekee sana kwani haukuwa na elements zozote za ushabiki unaoharibu nchi yetu hasa Bunge letu la JMT. Hongera sana Mh.Mnyika.
Okangi.

Anonymous said...

nikupongeze kwa ufuatiliaji wako bungeni kwenye vikao mbalimbali. ongeza bidii kwenye suala la maji na barabara

Anonymous said...

Nakupongeza kwa uwakilishi mzuri na uwajibikaji. Pamoja na yote uliyoyasimamia, hususan maji, sinza D - madukani yote hadi Vatican bado maji ni tatizo, je, kwenye hili unalisemeaje ? Hatua gani zimechukuliwa na hali ikoje ? Mama Ipyana

Anonymous said...

Mheshimiwa Mbunge kwanza nakupongeza kwa kutoa taarifa juu ya utekelezaji wa ahadi zako. Very few MP do provide feedbacks. Pili nakuomba ujitahidi kuwasiliana na mamlaka husika ili kuweza kupanua huduma za zahanati ya Kimara, kwakweli inahudumia watu wengi sana, haina nafasi ya kutosha. Angalau ingeongezewa hadhi iweze hata kulaza wagonjwa. Pia kuna baadhi ya wilaya kuna kitu kinaitwa Community Health Fund (CHF) au mfuko wa afya ya jamii. ebu fuatilia suala hili ili wananchi wakowaweze kufaidika na huduma hii.

Anonymous said...

Tunakuamini, Tupo nyuma yako.
MDAU, Chuo Kikuu Ardhi.

Anonymous said...

Hongera sana Mh. JJ. Kama mwananchi mtarajiwa wa Msakuzi nikuombe tu kuwa mjadala wako angalau katika vikao vya manispaa pamoja na mambo mengine mengi yanayohusiana na maendeleo ya Jimbo letu, basi usisitize na kuiimiza serikali basi kuwa SIKU ZOTE WATU HUFUATA HUDUMA NA SI HUDUMA KUFUATA WATU. Hivyo, umeme na maji kwa maeneno hasa yanayokua Msakuzi, Kibamba, Kwembe, Mpigi n.k. TANESCO wasambaze nguzo ili kushawishi watu wahamie kwa haraka zaidi na kupunguza hadha za upangaji wa kihuni unaoathiri shughuli zetu za kila siku za kimaisha hapa mjini. Ni hayo tu Mh.
Inshallah, 2015 U A THE HERO with M4C YES WE CAN

Anonymous said...

Mheshimiwa mbunge, naomba kama unaweza jaribu kufuatialia barabara ya kutoka kwa Msuguri kwenda Msingwa ambayo ilijengwa kwa kuweka kifusi hafifi ili ccm watushawishi tuwapigie kura iligharimu shilingi ngapi za kitanzania. Kama unakumbuka hii barabara ilijengwa mwezi wa kumi kama sijakosea ilikuwa ni kipindi cha uchaguzi mkuu. juzi juzi walileta greda likaparuza kiaina pia ikumbukwe unapoleta greda na kuparuza unaondoa kokoto yote ambayo inazuia uterezi. kwa sasa makaravati mengi yapo kwenye hari ya kututenganisha na upande wa pili lakini yanaangaliwa tuu bila ya kuchukua hatua za makusudi ya kutengeneza.
Maji kwetu ni janga la kitaifa kwani tunalazimika kununua maji kwa bei ya juu sana yaani ndoo kwa sasa ni Tshs 500/=
Kuna malalamiko juu ya transforma inayopeleka umeme Msingwa kuwa ni ndogo sana kulinganisha na wakazi wa sasa wa msingwa. mbali na malalamiko hayo hakuna juhudi zozote zinazochukuliwa na Tanesco juu ya hili tatizo kibaya zaidi wanazidi kuunganishia wateja wakati transforma haitoshi. Amini usiamini jioni umeme ni low voltege mpaka kufikia 100/105 hii ni hatari kwa maisha ya vifaa vyetu.
Pia kun malalamiko kuhusu kamati ya maji ya Msingwa kuwa mapato ya maji hayako wazi! Kama ukiweza hebu jaribu kufatilia hayo.
Ahsante sana nakutakia kazi njema ya ujenzi wa Taifa lenye rasilimali lakini maskini wa kutupwa kwa sababu ya viongozi dhaifu!