Wednesday, October 3, 2012

Mnyika ‘akomalia’ ujenzi wa shule na barabara Mburahati

Na Mwandishi Wetu

Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika amesema kuwa mgogoro kuhusu eneo la ujenzi wa Shule ya Sekondari Mburahati umeelekea kupatiwa ufumbuzi ambapo sasa mapendekezo ni kujenga shule hiyo katika mwaka wa fedha 2012/2013 katika eneo la wazi jirani na kituo cha polisi katika kata hiyo hivyo wakazi wanapaswa kutoa maoni yao iwapo pendekezo hilo ni muafaka.


Aidha, amewataka wananchi kama ambavyo waliungana pamoja bila kujali vyama vyao katika kufuatilia suala hilo waelekeze nguvu katika kufuatilia kuhakikisha kwamba ujenzi wa barabara ya Mburahati mpaka Mabibo NIT iliyoanza kujengwa kwa kiwango cha lami kwa kusuasua ikiwa imetengewa kiasi cha shilingi milioni 504 kwenye mwaka wa fedha 2011/2012 unaendelea na kukamilika kwa haraka zaidi kwa kuongezewa fedha katika mwaka 2012/2013.

Mnyika aliyasema hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Mburahati hivi karibuni na kusisitiza kuwa barabara hiyo ina umuhimu wa pekee wakati huu ambapo barabara ya Morogoro iko katika ujenzi wa Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka (DART) hivyo barabara hiyo ikikamilika kwa kiwango cha lami ikikamilika itaweza kuchangia katika kupunguza foleni ikiwa njia mbadala.

Mnyika alisisitiza kuwa pamoja na wananchi kuchagua wabunge na madiwani bado wanawajibu wa kutimiza wajibu wa kiraia wa kufuatilia masuala ya msingi ya maendeleo ili kuhakikisha uwajibikaji.

Alisema kuwa katika kufanya hivyo, vyama vya siasa navyo vina wajibu wa pekee ndio maana Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kwamba chama legelege huzaa serikali legelege hivyo pamoja na ziara za kiserikali anazozifanya jimboni kwa nyakati mbalimbali amejiunga pia katika ziara ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jimboni Ubungo ili kukiwezesha chama nacho kutimiza wajibu wake.

Awali Mnyika alieleza shule ya sekondari ya Mburahati ilianzishwa mwaka 2010 na kupewa usajili ikitumia madarasa ya kuazima ya shule ya msingi Muungano. Amesema ulizuka mvutano wa kundi moja likitaka wanafunzi wa shule ya msingi wasambazwe katika shule jirani za Barafu, Bryson na Mburahati ili shule hiyo igeuzwe kuwa sekondari huku kundi lingine wananchi wakitaka shule ya sekondari ijengwe kwenye eneo la wazi lillovamiwa na CCM katika mtaa wa Barafu au eneo la karibu na kituo cha polisi cha Mburahati.

Mnyika alisema kuwa kufuatia hali hiyo na baada ya wananchi kumtaka kuingilia katika katika mkutano alioufanya kata ya Mburahati tarehe 26 Februari 2012 alifanya hivyo kupitia mikutano ya Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni na hatimaye akaihoji bungeni kwenye mkutano wa bunge la bajeti uliomalizika mwezi Agosti 2012. Kufuatia kuingilia kati amepewa majibu kuwa sasa ujenzi huo utafanyika katika eneo la wazi jirani na Kituo cha Polisi Mburahati.

No comments: