Monday, November 12, 2012

SABABU ZA AWALI ZA KUKATA RUFAA DHIDI YA UAMUZI WA SPIKA WA TAREHE 9/11/2012 WENYE MWELEKEO WA ‘FUNIKA KOMBE’


Baada ya habari kutolewa jana na leo juu ya uamuzi wa Spika kuhusu tuhuma kwamba baadhi wa wabunge na wajumbe wa kamati ya Nishati na Madini walijihusisha na vitendo vya rushwa katika kutekeleza kazi zao za kibunge, nimeulizwa na baadhi ya wanahabari na wananchi kwa simu na kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii sababu za kusimama bungeni tarehe 9 Novemba 2012 mara baada ya Spika kutoa uamuzi huo na kutaka kuomba muongozo.

Nalazimika kutoa ufafanuzi huu nje ya bunge baada ya mkutano wa bunge kuahirishwa bila Spika kunipa fursa ya kusema jambo hili bungeni kwamba nilitaka muongozo wake kwa mujibu wa Kanuni ya 5(1) na 5 (2) kuwa nakusudia kukata rufaa dhidi ya uamuzi wake kutokana na kuwa na maudhui kadhaa yasiyozingatia katiba ya nchi, sheria mbalimbali za nchi, kanuni za kudumu za bunge, maamuzi ya awali ya maspika wa Bunge pamoja na mila na desturi za mabunge mengine yenye utaratibu wa kibunge unaofanana na utaratibu wa bunge letu.

Hata hivyo kwa kuzingatia kuwa rufaa huchukua muda kusikilizwa nilitaka niombe muongozo wake kabla ya Mkutano wa Bunge kuahirishwa kwa kuwa katika uamuzi wake hakueleza hatma ya Kamati ya Nishati na Madini ilivyovunjwa, hivyo Spika anapaswa bado kueleza kwa umma iwapo kamati hiyo inarejeshwa au inaundwa kamati nyingine au kuelekeza kamati nyingine ya kudumu ya Bunge inayopaswa kuisimamia Serikali wakati huu ambapo nchi inakabiliwa na matatizo mengi kwenye sekta za nishati na madini yenye athari kwa maisha ya wananchi wakiwemo wa Jimbo la Ubungo.

Kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa Nishati na Madini nasisitiza kwamba Spika anapaswa kurejea barua yangu ya toka mapema Oktoba ambayo mpaka sasa haijapatiwa majibu, hoja niliyoiwasilisha bungeni na kuungwa mkono ya jambo lililohusu haki za bunge  na miongozo niliyoomba bungeni kuhusu masuala ya nishati kwa nyakati mbalimbali katika mkutano wa Bunge uliomalizika  na kutoa kauli kwa umma.

Kwa kuwa katika uamuzi wake Spika wa Bunge ameeleza kwamba Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter  Muhongo na Katibu Mkuu wake Eliackim Maswi wametoa maelezo yasiyokuwa kweli kwa nyakati mbalimbali uwepo wa kamati ya bunge kwa ajili ya kuisimamia Wizara hiyo kwa niaba ya bunge ni suala linalohitaji uamuzi wa haraka.

Aidha, katika uamuzi wake Spika zaidi ya kutoa onyo kali kwa Katibu Mkuu na Wabunge hakutoa onyo kwa Waziri wa Nishati na Madini wala hakueleza chochote  iwapo alipokea ushauri kutoka kwa Kamati Ndogo ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuhusu ukiukwaji wa kanuni uliofanywa na Spika mwenyewe bungeni wakati wa kadhia nzima.

Kwa mujibu wa Kanuni za Bunge Spika anaweza kutoa taarifa bungeni wakati wowote  na taarifa yake haijadiliwi hivyo sehemu kubwa ya taarifa ya tarehe 9 Novemba 2012 ilikuwa ni maelezo kuanzia sehemu ya kwanza mpaka sehemu ya pili.

Uamuzi wa Spika unapatikana sehemu ya tatu ya maelekezo hususan kifungu cha 6.12 ya kwamba “tuhuma husika hazikuweza kuthibitishwa” na baadaye kufuatiwa na uamuzi wa Spika kuhusu watoa tuhuma katika vipengele (a), (b), (c) na (d).

Nakusudia kukata rufaa ili taarifa kamili ya Kamati Ndogo ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge iweze kuwasilishwa kwa ukamilifu wake kwenye kamati husika ya kudumu ya Bunge na hatimaye taarifa kamili kuwasilishwa na kujadiliwa bungeni ili ‘mbivu na mbovu’ zijulikane na masuala yanayohitaji kufanyiwa uchunguzi wa ziada na vyombo vingine vya nje ya Bunge yaendelee kwa hatua zaidi badala ya uamuzi huu wa ‘funika kombe’.

Yapo masuala ya ziada ambayo binafsi niliyaeleza mbele ya kamati ndogo chini ya kiapo ambayo sitakiwi kuyaeleza nje ya bunge kwa mujibu wa kanuni na sheria husika , hata hivyo taarifa kamili ikiingia bungeni kutakuwa na uhuru wa majadiliano kwa mujibu Kwa Ibara ya 100 ya Katiba ya Nchi.

Aidha, nitaka rufaa kwa kuwa kiwango cha ‘adhabu’ kilichotolewa kwenye uamuzi wa Spika hakilingani na ‘makosa’ ambayo yameelezwa kuwa na  uzito wenye kuathiri “kwa kiasi kikubwa hadhi ya Bunge kama taasisi na heshima ya wabunge waliohusishwa”.

Spika amefanya uamuzi wake chini ya Kanuni ya 5(1) na 72 (1) lakini hakuzingatia kuwa kanuni ya 72 (3) inaeleza kuwa iwapo mbunge ameshindwa kuthibitisha ukweli Spika amepewa fursa ya kumsimamisha mbunge huyo kuhudhuria vikao vya Bunge visivyozidi vitano.

Aidha nitakata rufaa kwa kuwa waliodaiwa kutoa kutoa tuhuma bila ushahidi walipaswa kujieleza kwa tuhuma hizo kabla ya kuhukumiwa kwa misingi ya kanuni za haki ya asili zilizopo pia katika katiba ya Nchi na kwa kuzingatia matakwa ya kanuni za kudumu za Bunge; hata hivyo Spika amefikia uamuzi wa moja kwa moja wa kutoa adhabu ya ‘onyo kali’ kinyume na masharti ya kanuni ya 5 (1).

Ikumbukwe kwamba Spika katika maelezo yake amesisitiza kuwa Kamati Ndogo ilipewa hadidu rejea moja tu, “Kuchunguza na kumshauri Spika iwapo tuhuma kwa baadhi ya wabunge na wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini kujihusisha na vitendo vya rushwa ni za kweli au hapana”, baada ya kuchunguza kwa mujibu wa hadidu rejea hiyo na kuwasilisha ripoti yake Spika alipaswa kama kuna ukiukwaji mpya wa kanuni uliobainika kutokana na uchunguzi huo kuanzisha mchakato wa adhabu.

Binafsi niliitwa kwa maandishi kuisaidia kamati ndogo katika uchunguzi wake kutokana na maoni niliyowasilisha bungeni ya kwamba  “….Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inafahamu kwamba kuna kampeni kubwa inafanywa ndani na nje ya Bunge ili uamuzi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati ubatilishwe kwa maslahi ya Makampuni yaliyokosa zabuni kuiuzia TANESCO mafuta ya kuendesha mitambo ya kufua umeme…”.

Sijawahi kuandikiwa au kuitwa popote kutakiwa kujieleza kwa ‘kuisemea tuhuma bungeni bila ya kufanya utafiti kupata ukweli’ na maelezo hayo niliyoyatoa bungeni hayakukiuka kanuni yoyote ya bunge kama ambavyo nitathibitisha wakati nitakapokata rufaa.

Kwa upande mwingine nitakata rufaa kwa kuwa adhabu aliyopewa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Eliakim Maswi hailingani na ukubwa wa makosa anayodaiwa kuyafanya, ikiwa ni kweli amevunja haki za bunge kwa kuzusha tuhuma za uongo dhidi ya wabunge kwa ajili ya kujihami dhidi ya baadhi ya wajumbe wa kamati ya Bunge ya Nishati na Madini waliokuwa wanahoji kuhusu utendaji wa Wizara yake.
Kwa kosa hilo ikiwa maelezo ya Spika kuhusu matokeo ya uchunguzi wa Kamati ni sahihi anapaswa kufunguliwa mashtaka kwa mujibu wa Sheria ya Kinga, Madaraka na Haki za Bunge na kupewa adhabu ya zaidi ya onyo ikiwemo hata faini au kifungo au walau kutakiwa kuwajibika.

Kadhalika kwa Spika ameeleza kuwa mbinu aliyotumia ni pamoja na kutaka kuwalipa fedha wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini shilingi milioni mbili kwa kila mjumbe madai haya ni ya jaribio la kufanya ufisadi wa fedha na matumizi mabaya ya madaraka kama ilivyokuwa kwenye kashfa ya Katibu Mkuu aliyemtangulia David Jairo hivyo Spika alipaswa kupendekeza kwa mamlaka ya uteuzi wake kuchukua hatua za kinidhamu na kisheria.

Uamuzi wa Spika ‘kufunika kombe’ hauna tofauti na maamuzi yaliyotangulia ambayo yamesababisha mpaka sasa Serikali haijawasilisha bungeni ripoti ya utekelezaji wa maazimio ya Bunge kufuatia uchunguzi uliofanywa na kamati teule ya Bunge.

Ni vizuri ikakumbukwa kwamba katika hotuba yangu bungeni kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni tarehe 27 Julai 2012 nilisisitiza kwamba  “ili ukweli wa kina uweze kujulikana Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza kuwa bunge liazimie kuunda Kamati Teule ya Bunge kuchunguza masuala yote ya ukiukwaji wa sheria, matumizi mabaya ya madaraka na tuhuma za ufisadi katika utekelezaji wa mpango wa dharura wa umeme na ununuzi wa mafuta wa ajili ya mitambo ya umeme.

Uchunguzi huo uhusishe pia mkaguzi mkuu kufanya ukaguzi wa kiuchunguzi (Forensic Audit) kwa malipo yaliyofanywa na makampuni ya BP (Sasa PUMA Energy), Oryx na Camel Oil ili kubaini iwapo kuna vigogo zaidi wa serikali waliojinufaisha kwa kisingizio cha dharura ya umeme. Izingatiwe kwamba masharti ya ibara ya 27(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inamtaka kila mtu “… kutunza vizuri mali ya Mamlaka ya Nchi na ya pamoja (na) kupiga vita aina zote za uharibifu na ubadhirifu….”.

Mchakato huu ungewezesha kupata ukweli wa ziada kibunge kuliko utaratibu uliotumiwa na Kamati Ndogo na Spika.

Nitaeleza masuala ya ziada nitakayoyakatia rufaa na kauli yangu kuhusu maelezo na uamuzi wa Spika juu ya Waziri na Waziri Kivuli wa Nishati na Madini.

John Mnyika (Mb)
10/11/2012

No comments: