Saturday, November 24, 2012

Mnyika amlilia Odira Ongara


Na Mwandishi Wetu

Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika ametoa salamu za rambirambi kwa kifo cha Mzee Odira Elizaphan Hamathe Ongara na kumweleza Marehemu kuwa alikuwa mtu mwenye msimamo katika nafasi za uongozi na utumishi wa umma alizowahi kuzishikilia wakati wa marais watatu wa Tanzania; Nyerere, Mwinyi na Mkapa.

Mnyika alisema hayo jana (Novemba 23, 2012) wakati akihutubia waombolezaji waliojitokeza nyumbani kwa familia ya marehemu kata ya Kwembe, jimboni Ubungo. “ Nilipopata taarifa za msiba juzi, nilimtumia ujumbe mfupi wa maneno Eric (mtoto wa marehemu) akiwa Afrika Kusini kikazi kuwa asihuzunike, mzee amekwenda kupumzika baada ya kazi. Sasa majukumu yamebaki kwa vijana kwenda mbele zaidi. Na huu ni ujumbe wangu kwenu leo, tumuombee apumzike kwa amani lakini tukumbuke tunao wajibu wa kulitumikia Taifa letu na jamii yetu”.

Marehemu Odira Ongara pamoja na mambo mengine atakumbukwa kwa msimamo wake katika masuala mbalimbali nchini hususan misimamo yake katika kipindi cha utumishi serikalini.

Moja kati ya misimamo wa Mzee Ongara ambayo ni ya mfano na yenye kutoa fundisho kubwa hasa kwa watumishi wa umma katika nyadhifa mbalimbali za kiserikali na pia kisiasa ni pamoja na ule wakati wa sakata la ununuzi wa kivuko cha Kilombero akiwa Katibu Mkuu wizara ya miundo mbinu ambayo wakati kwa wakati huo ilihusika na masuala ya ujenzi na mawasiliano kati ya mwaka 1978 na 1986. Marehemu Ongara alipinga mpango wa ununuzi wa kivuko kilichotumika.

Katika kupinga hatua hiyo ya kununua kivuko kilichotumika, Marehemu Ongara alikataa kusaini nyaraka. Lakini hatimaye ununuzi huo uliidhinishwa na waziri wa wakati huo Mustapha Nyang’anyi. Kivuko hicho baadae kilikuja kuzama na kuua. Kivuko hicho kilizusha mjadala mkali hasa baada ya kuzama kwake na kuua ambapo marehemu Odira Ongara kwenye mkutano wake na vyombo vya habari alieleza wazi kuwa hakukubaliana na ununuzi huo na kuahidi kutoa nyaraka za kuonyesha aliyeidhinisha ununuzi wa kivuko hicho kilichokuwa kimekwisha kutumika. Lakini siku iliyofuata usiku wa siku aliyozungumza na waandishi wa habari wizara hiyo ikaungua moto na nyaraka mbalimbali zikateketea.

Baada ya tukio hilo, marehemu Ongara aliondolewa wizarani na kupelekwa mikoani kati ya mwaka 1986 mpaka 1996 ambapo alitumikia kama Mkurugenzi wa Maendeleo nafasi inayoshabiana na afisa tawala mikoa.

“Kwa heshima ya mzee wetu na kwa ushirikiano nanyi kwa niaba ya wananchi na marafiki, nitaambatana nanyi katika maziko kijiji cha Utegi”, alisema Mnyika.

Marehemu Odira Ongara alizaliwa mwaka 1946 na anatarajiwa kuzikwa siku ya jumapili tarehe 25 Novemba, 2012 wilayani Rorya. Marehemu amewahi kulitumikia taifa katika mikoa mbalimbali ikiwemo Morogoro, Pwani, Lindi, Tanga, Tabora na mingineyo. Aliwahi kuteuliwa pia wakati wa Hayati Mwalimu Nyerere kuwa Naibu Katibu Mkuu wa wizara ya Fedha. Marehemu alikuwa sehemu ya ujumbe uliotumika na Hayati Nyerere, Ufaransa kufanya majadaliano yaliyowezesha ujenzi wa uwanja wa kimataifa wa ndege wa Dar es Salaam. Marehemu alistaafu kazi katika utumishi wa umma mwaka 1996 akiwa Ofisi ya Waziri Mkuu, wakati huo akiwa na umri wa miaka 50.

No comments: