Friday, November 23, 2012

SIRI HADHARANI KUWEZESHA HATUA ZA ZIADA ZA KISHERIA KUCHUKULIWA DHIDI YA MHANDO NA WENZAKE

Nimeamua kuchukua hatua ya kuiweka hadharani ripoti hii ya SIRI ya ndani ya Shirika la Umeme (TANESCO) ya maoni ya kisheria juu ya ukaguzi maalum uliofanywa na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi niliyoitoa tarehe 1 Novemba 2012.

Kwa mujibu wa nyaraka hii ni wazi aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme (TANESCO) William Mhando amefanya makosa mengi yanayohitaji hatua za ziada za kisheria ikiwemo ya mgongano wa maslahi, utovu wa uaminifu, kushindwa kutangaza maslahi na matumizi mabaya ya ofisi; matendo ambayo ni ya kifisadi.

Makosa hayo na mengine ni kinyume cha sheria mbalimbali za nchi ikiwemo Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, Sheria ya Ununuzi wa Umma na sheria nyingine.

Hivyo, kwa kuwa Bodi imekataa kuwa haitachukua hatua za zaidi za kisheria juu yake natoa kauli ya ziada kwamba mamlaka zingine zinazohusika zichambue Taarifa hii sanjari na Taarifa ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) na kuchukua hatua za kisheria zilizochini ya mamlaka hizo.

Mamlaka hizo ni pamoja na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Sekretariati ya Maadili ya Umma zote kila moja kwa nafasi yake zichunguze ukiukwaji wa sheria katika masuala yaliyo kwenye majukumu yao na kuchukua hatua za ziada.

Aidha, wakati mamlaka na taasisi hizo zikiendelea kuchukua hatua za kisheria naitaka kwa mara nyingine bodi ieleze hatua ilizochukua dhidi ya watendaji wengine wa TANESCO walioshirikiana naye kwa namna moja au nyingine na iwapo bodi hiyo haitachukua hatua za haraka, ukiondoa majina ya maafisa watatu waliosimamishwa mpaka sasa nitataja majina ya ziada ya maofisa wengine waliohusika na kutaka Rais Jakaya Kikwete kuingilia kati kwa mamlaka yake ya kikatiba na kuchukua hatua ikiwemo dhidi ya bodi yenyewe.

Ikumbukwe kwamba kufuatia kufukuzwa kazi kwa Mhando kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa Nishati na Madini tarehe 1 Novemba 2012 nilitoa kauli ya awali kwamba hatua hiyo pekee haitoshi bali Serikali irejee katika hotuba niliyotoa tarehe 27 Julai 2012 bungeni kwa niaba ya kambi rasmi ya upinzani na kuchukua hatua zaidi za kuwezesha Mhando na wenzake kufikishwa mahakamani.

Aidha, pamoja na hatua za ziada nilitaka bodi ya TANESCO kueleza hatua ilizochukua dhidi ya watendaji wengine wa TANESCO walioshirikiana naye kwa namna moja au nyingine na iwapo bodi hiyo haitachukua hatua za haraka niliahidi kuiweka hadharani taarifa ya kamati iliyoundwa na bodi hiyo kuchambua taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kueleza hatua ambazo zinapaswa kuchukuliwa na Rais Jakaya Kikwete dhidi ya Bodi yenyewe.

Kufuatia kauli yangu hiyo tarehe 3 na 7 Novemba 2012 Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Jenerali Mstaafu Robert Mboma alinukuliwa baadhi ya vyombo vya habari akisema kwamba aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo William Mhando hawezi kushitakiwa mahakamani kwa sababu kosa alilofanya la kuingia kwenye mikataba yenye mgongano wa kimaslahi ni kosa la kiuadilifu.

Mwenyekiti wa Bodi ametaja kosa moja tu la mgongano wa kimaslahi wakati ambapo yapo makosa mengine na naamini kauli yake imetokana na ushauri wa kwenye kipengele cha 36 na 37 cha nyaraka niliyoambatanisha; maoni ambayo bodi ilipaswa kuyachukulia kwa tahadhari na kutaka mamlaka na vyombo vya uchunguzi kuendelea na hatua zao za ziada kuwezesha hatua za kisheria kuchukuliwa.

Aidha alieleza kwamba kuhusu maofisa wengine watatu waliosimamishwa sambamba na Mhando bodi yake inasubiri taarifa ya ukaguzi unaofanywa na Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) ili kubaini kama wana makosa wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria na kuahidi kwamba uchunguzi dhidi yao ungekamilika ndani ya wiki moja na kueleza kuwa hatma yao ingejulikana tarehe 16 Novemba 2012 ahadi ambayo mpaka leo tarehe 23 Novemba 2012 haijaitekeleza.

Katika muktadha huo kwa kuwa suala hili tayari limeshatolewa kauli kwenye vyombo vya habari kwa nyakati mbalimbali na Wizara ya Nishati na Madini pamoja na TANESCO, mawasiliano ya kawaida ya kiofisi na kuendelea kuficha taarifa za siri kama hii hakutalisaidia taifa kujinusuru kwa haraka na ufisadi. Hivyo, kusambaza taarifa hii hadharani na kutaka majibu ya wazi toka kwa mamlaka zote zinazohusika kutawezesha hatua za haraka kuchukuliwa kwa maslahi ya umma.

Wenu katika uwakilishi wa wananchi, 



John Mnyika (Mb) Waziri Kivuli wa Nishati na Madini.

1 comment:

Anonymous said...

Naona link ya mwanzo haikuwa Ripoti yenyewe, lakini sasa umerekebisha. Akhsante mheshimiwa.