Tuesday, September 10, 2013

Mnyika: Serikali imalize tatizo la maji

na Abdallah Khamis

MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika, ameitaka serikali kuhamisha nguvu na kasi zilizotumika katika ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara kuelekea jijini Dar es Salaam na kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi hususan katika Jimbo la Ubungo.

Mnyika alitoa kauli hiyo juzi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Kimara, Mtaa wa Mavurunza na kusisitiza hakuna suala muhimu kama maji kwa wananchi na kwamba kunahitajika ufumbuzi wa muda mfupi na mrefu, ikibidi kwa hali ya dharura.

Alisema kama serikali inaweza kutumia muda mfupi kujenga na kutandaza bomba hilo kwa nini ishindwe kufanya hivyo kwa mabomba ya maji, ambayo ni uhai wa wananchi.

“Tunaendelea kupambana kuhakikisha tatizo la maji tunalipunguza na kuliondoa kabisa, ninachowaomba ni sauti zenu na mshikamano wenu, suala hili ni uhai wa watu, kama maji ni tatizo maana yake uhai wa binadamu uko shakani,” alisema Mnyika.

Aliongeza kuwa ni wakati muafaka kuharakisha ujenzi wa bomba la Ruvu Juu, kutoka Mlandizi hadi Kimara kwa kugawanya majukumu yatakayomuwezesha mkandarasi mwingine kuanzia sehemu nyingine ya mradi huo na kisha waungane katika kumalizia kazi hiyo.

Alisema kuwa utatuzi mwingine kama moja ya suluhisho la muda mfupi wakati wananchi wakisubiri suluhisho la muda mrefu, ni serikali kuunganisha mifumo ya maji ya Ruvu Juu na Ruvu Chini ili iweze kusaidiana pale ambapo mfumo mmoja unakuwa na upungufu wa maji au tatizo lolote kubwa.

Mbunge huyo aliwakumbusha wakazi wa Kimara Mavurunza kuwa eneo hilo ndipo Rais Jakaya Kikwete alitoa ahadi ya kumaliza tatizo la maji jijini Dar es Salaam.

Chanzo: TanzaniaDaima Jumanne Septemba 10, 2013 Toleo Na. 3203 ISSN 0856 9760  http://freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=53721

No comments: