Thursday, June 3, 2010

Mnyika achukua fomu ya kugombea Ubunge Ubungo

MKURUGENZI wa Mambo ya Nje wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bw. John Mnyika amechukua rasmi fomu ya kugombea Ubunge katika Jimbo la Ubungo.

Akichukua fomu hiyo Dar es Salaam jana, Bw. Mnyika aliwataka wananchi kuwapuuza wanasiasa walioshindwa kuongoza nchi na kuitumbukiza kwenye mfumuko wa bei na kuzorotesha maendeleo ya jamii na kuwaachia mafisadi kufuja fedha za umma.

Bw. Mnyika alisema ameamua kuchukua fomu ya CHADEMA kwa kuwa ni chama mbadala na tumaini jipya la Watanzania chini ya falsafa yake ya Nguvu ya Umma.

"Leo nimekuja kuchukua fomu sitatoa hotuba, nitazungumza kwa kirefu siku nitakaporudisha fomu, leo natoa tu rai kwa wananchi wa ubungo na Tanzania kwa ujumla kuwapuuza wanasiasa walioshindwa kuongoza nchi na kuitumbukiza katika mfumuko wa bei na kuzorotesha huduma za jamii huku mafisadi wakiendelea kufuja fedha ya umma," alisema Bw. Mnyika.

Aidha aliwataka wananachi kupuuza kauli ya Rais Jakaya Kikwete kuhusu takrima akidai kuwa ni za kubariki rushwa kwa kisingizio cha takrima.

Bw. Mnyika alisema kauli ya Rais Kikwete ya kuwa wagombea wanaweza kutoa pombe kwa wananchi, kauli ambayo imetafsiriwa kuwa ni kuchochea rushwa kwenye uchaguzi na suala ambalo rais asipolikanusha, itathibitisha kuwa hakuwa na dhamira ya kweli ya kudhibiti matumizi makubwa ya fedha kwenye uchaguzi.

Aidha alisema kauli hiyo isipokanushwa itakuwa ni ishara ya kutoheshimu utawala wa sheria.

Aliongeza kuwa nia yake nyingine ya kuchukua fomu ya kuwania ubunge katika jimbo hilo ili kupata fursa ya kushiriki kikamilifu katika kuliletea mabadiliko ya kweli jimbo hilo pamoja na Tanzania kwa ujumla kupitia siasa safi na uongozi wenye utawala bora.

Mwanasiasa huyo amewataka Watanzania wengine kujitokeza kugombea kwenye jimbo hilo katika nafasi za udiwani ili Manispaa ya Kinondoni iendeshwe na vyama mbalimbali tofauti ilivyo sasa ambapo Dar es Salaam inaongozwa na CCM.

Bw. Mnyika alichukua fomu hiyo katika Ofisi za CHADEMA Jimbo la Ubungo kutoka kwa Katibu wa Jimbo hilo, Bw. Nasor Balozi.

Chanzo: Majira 17 Mei 2010-http://majira.co.tz/index.php?option=com_content&view=article&id=199:mnyika-achukua-fomu-kugombea-ubungo&catid=1:latest-news&Itemid=18

4 comments:

Anonymous said...

Mnyika umechukua fomu ubungo, lakini usiharibu chama kwenye majimbo mengine ya dar,unaonekana kuharibu chama kwenye baadhi ya majimbo ya dar hasa segerea na kigamboni.Tunakuomba uwachie watu wa segerea na kigamboni kazi ya kuteua mbunge usiwapangie!!!!! wala usiingilie mchakato ndani ya haya majimbo kwa usalama wa chama chenu!

Anonymous said...

Mnyika ameingilia vipi uteuzi kwenye majimbo ya Segerea na Kigamboni? Hebu tupe maelezo zaidi

Anonymous said...

kwanza ametengeneza mpasuko ambao ni hatari kwa chama.Kuzungumza na kikundi cha watu kutoka katika kata iliyoko kwenye jimbo mfano jimbo la segerea kuwa mgombea aliyeko ni weak thats why jimbo halipewi kipaumbele pamoja na jimbo la ukonga.Let me tell u one thing mnyika..siasa unayoitaka kuifanya sio nzuri,kujulikana kwako ubungo ni sababu uligombea 2005,lakini uchaguzi wa serikali za mtaa hukupata hata kiti kimoja ,hao unaodai ni dhaifu wamepata mitaa,waache nao watajulikana wakishagombea!naipenda chadema bt kuna watu kama wewe humo wanakatisha tamaa.ur very selfish mnyika!

John Mnyika said...

Nimesoma maoni ya anonymous wawili, naomba ieleweke kwamba madai yanayotolewa hapa hayana ukweli wowote. Ifahamike pia kuwa si kweli kwamba CHADEMA Ubungo haikushinda kiti chochote cha mtaa katika uchaguzi wa mwaka 2009. Nawatakia mjadala mwema