Thursday, December 22, 2011

Hatua kuhusu maafa katika Jimbo la Ubungo

Jana na leo nimeshiriki katika jitihada za uokoaji na nimetembelea maeneo mbalimbali katika Jimbo la Ubungo kwa ajili ya kuchukua hatua za kibunge kufuatia maafa ambayo yamejitokeza kutokana na mvua na mafuriko yanayoendelea.

Kama sehemu ya kazi ya mbunge ya uwakilishi na kuisimamia serikali nimekuwa nikiwasiliana mara kwa mara na mamlaka zinazohusika na naomba kitengo cha maafa kuongeza nguvu zaidi katika kushughulikia matatizo yaliyojitokeza. Ingawa kuna udhaifu mkubwa katika mfumo wetu mzima wa kukabiliana na maafa na dharura kwa ujumla, hata hivyo huu si wakati wa kulaumiana bali kuunganisha nguvu katika kuchukua hatua za haraka.

Aidha, natoa pole kwa wananchi wote waliofiwa au kuathirika kutokana na maafa yanayoendelea na kuwasihi waishi kwa tahadhari lakini wawe na utulivu katika kipindi hiki kigumu. Pia, natoa mwito kwa wadau wengine wote ikiwemo mashirika ya misaada ya kinadamu kutembelea katika maeneo ya maafa kuona hali halisi na kuchukua hatua zinazostahili kuunga mkono jitihada ambazo tunaendelea nazo hivi sasa.

Maeneo ambayo nimetembelea nyumba za wananchi na miundombinu ni pamoja na kata ya Ubungo (maeneo ya Ubungo Kisiwani na Msewe), Kata ya Sinza (Maeneo ya Sinza D na Sinza E) kata ya Mabibo (Maeneo ya Mabibo farasi na Loyola) na Manzese (maeneo ya Uzuri na Chakula Bora).Aidha nimefuatilia kupitia kwa madiwani na watendaji wengine taarifa za maeneo mengine yaliyokumbwa na maafa ya kata za Kimara, Makuburi, Mbezi na Goba na wakati wote nimekuwa nikitoa taarifa kwa mamlaka zote zinazohusika na kuwezesha hatua mbalimbali hususani za uokoaji kuweza kuchukuliwa.

Natoa taarifa hii nikiwa njiani nikiendelea kutembelea maeneo mengine ili maafa haya yanayoendelea yaweze kuchukuliwa kwa udharura na uzito unaostahili na wananchi na mamlaka zote zinazohusika.

Kutokana na maafa haya wapo wananchi ambao makazi yao yameharibiwa kabisa na wanahitaji maeneo ya dharura ya kuweza kuishi pamoja na kupata mahitaji ya kibinadamu hasa baadhi ya kaya za eneo la Ubungo Kisiwani (Nyuma ya Land Mark Hotel) na baadhi ya kaya za eneo la Manzese (Uzuri na Chakula Bora). Manispaa ya Kinondoni inapaswa kutangaza eneo maalum kwa ajili ya huduma husika kuweza kupatikana kwa wahanga kama jambo la dharura.

Aidha, miundombinu ya maeneo mbalimbali imeharibiwa hali ambayo inahitaji njia mbadala za wananchi kuweza kuvuka mito na mikondo ya maji katika maeneo husika bila kuhatarisha maeneo yao. Baadhi ya madaraja yaliyoharibiwa ni pamoja na daraja la Msewe, madaraja ya Kilungule, daraja la Mabibo Farasi na daraja linalounganisha kata ya Mbezi Louis na Goba.

Pamoja na kuunga mkono agizo la mkuu wa mkoa kuwataka wanaoishi katika mabonde kuchukua tahadhari ya kukaa mbali na maeneo yao wakati huu wa mvua kubwa, nimebaini katika ziara niliyofanya kwamba maafa ya sasa yanagusa watu wengi zaidi ya waishio katika mabonde.

Hivyo, ni vizuri serikali ikatambua kwa dharura maeneo yote ambayo yako hatarini kufikiwa na maafuriko hata kama yako mbali na mabonde na kuweza kutoa tahadhari mahususi kwa wananchi na kuwaeleza utaratibu mbadala wa makazi ya dharura.
Pia, yapo maeneo ambayo uwezekano wa kukumbwa na mafuriko zaidi ni mkubwa pamoja na kuwa mbali na eneo la mto kutokana na kuziba kwa njia za mto kwa sababu mbalimbali ikiwemo matatizo katika ujenzi na mipango miji lakini pia kutokana na uchafu. Hivyo, hatua za dharura zinahitajika katika kusafisha, kupunguza kifusi na kuweka kingo ili kuwezesha maji kuweza kupita wakati huu wa dharura. Hatua hii ihusishe mito mbalimbali iliyoko jimbo la Ubungo ikiwemo mto ng’ombe katika kata na maeneo mbalimbali.

Pamoja na matatizo ya mipango miji ya ujenzi holela, udhaifu katika usafishaji wa mito pamoja na uchafuzi wa mazingira inaelekea maafa ya sasa yamechangiwa pia na mvua kubwa kutokana na mabadiliko ya tabia nchi. Hivyo, suala hili linapaswa kuchukuliwa kwa uzito wa kitaifa ili kukabiliana na athari za sasa na madhara makubwa zaidi yanayotarajiwa siku za usoni.

Hatua zinazochukuliwa mpaka hivi sasa bado hazilingani na ukubwa wa tatizo kwa kuwa kwa sehemu kubwa zinahusisha serikali katika ngazi ya mkoa, wilaya na manispaa mbalimbali za jiji la Dar es salaam katika maafa yenye uzito wa kitaifa yanayohitaji vyombo vyote vinavyohusika na maafa na wananchi kwa ujumla kuweza kuunganisha nguvu katika kuchukua hatua stahiki.

Nimewahimiza madiwani, watendaji wa kata, wenyeviti wa mitaa na watendaji wa mitaa kuweza kufanya tathmini katika maeneo yao na kutoa taarifa za dharura kwa ajili ya kuwezesha hatua kuchukuliwa kwa wakati.

Nitatoa taarifa kwa umma kuhusu masuala mengine yanayohusu misaada ya kibinadamu katika Jimbo la Ubungo baada ya kukutana na kamati ya maafa ya wilaya ya Kinondoni. Tumevitaarifu vyombo vya dola kuhusu vifo ambavyo vimetokea mpaka hivi sasa na naamini watatoa taarifa kwa umma. Aidha, mara baada ya kukamilisha kuchukua hatua za kushughulikia dharura ya maafa nitatoa taarifa ya kina zaidi ya athari za hali hii pamoja na madhara ya hatua kutokuchuliwa kwa wakati toka maamuzi yalipofanyika baada ya maafa yaliyotokana na mvua za El Nino miaka michache iliyopita.

John Mnyika-Mbunge wa Jimbo la Ubungo

PS: Taarifa hii niliitoa jana tarehe 21 Disemba 2011. Jana hiyo hiyo jioni tulikaa kikao cha Kamati ya Maafa ya Wilaya. Kutokana na kuwa na haraka ya kuelekea kwenye maeneo ya maafa sitaweza kuandika kwa kina maazimio tuliyoyafikia. Hata hivyo, tayari tumeshaanza utekelezaji wa kushirikiana na mamlaka mbalimbali kuhusu athari za kibinadamu na pia kuhusu miundombinu. Ofisi ya mbunge ubungo imeshawasiliana na madiwani, watendaji wa mitaa, wenyeviti na watendaji kwa ajili ya kuwajulisha hatua mbalimbali ambazo wanaendelea kuzichukua.

Leo ninashiriki katika kazi za maafa katika maeneo mbalimbali: Mosi, nitaungana na wenzetu wa jimbo la Kinondoni kwa ajili ya kutoa misaada ya kinadamu kwa wahanga wa maafa wa Hananasif, Magomeni Sunna, Tandale na Kigogo. Pili; nitakuwa na ziara ya jimbo la Ubungo kwa ajili ya kutoa misaada ya kibinadamu kwa wahanga wa Mbezi/Saranga (Kibanda cha Mkaa) na pia nitatembelea maeneo yaliyoathirika ya Kimara Kilungule na kwa Msuguri (eneo la Msingwa). Aidha, nitashiriki maziko ya mahanga waliofariki jana kutokana na maafa ya maafuriko katika kata ya Mburahati na pia walioangukiwa na ukuta kutokana na mvua katika eneo la Kilungule. Aidha, napenda kurudia tena kusisitiza kwamba huu si wakati wa kulaumiana bali kuunganisha nguvu katika kukabiliana na athari za maafuriko haya; hata hivyo baada ya maafa haya nitarejea katika kumbukumbu mbalimbali za kibunge na za vikao vya jiji na manispaa kuhoji sababu za hatua kutokuchukuliwa kwa wakati wa ukamilifu hata baada ya kutoa tahadhari mbalimbali na kutaka hatua kuchukuliwa kwa nyakati mbalimbali toka niingie katika utumishi wa umma ili hatua za uwajibikaji ziweze kufuata.

6 comments:

bongole3 said...

pole kwa maafa haya yaliyotukumba watanzania wote, mimi nipo hapa hapa jijini Mlimani University, hali ya maeneo hayo uliyotaja sio siri ni kama ulivoweka wazi na ni matumaini yangu mamlaka husika zipo kwa ajili ya utekelezaji! nakutakia kazi njema na utekelezaji mwema wa majukumu yako USISAHAU LILE SUALA LA CHUO NA TAARIFA UIPOST KAMA ILIVOKUA KWA HII.

Anonymous said...

Pamoja tunaweza na pole sana kwa maafa hayo kwani ni kilio cha Watanzania wote tunazidimshukuru Mungu kwa wale wakazi waishio nyuma ya landmark hotel hata maeneo ya ubungo maziwa baadhi ya wakazi waishio maeneo hayo wamekumbwa na maafa hayo huku baadhi ya vitu vyao kuharibika kutokana na mvua hiyo ya siku chache zilizopita....Mnyika uzidi kuwa na moyo huo huo Mungu azidi kunyoosha mkono wako na azidi kukuona ktk kazi zako za kila siku za kulijenga Taifa uzidi kuwa na moyo huo huo wa kujitolea kwa taifa likuzungukalo..na uzidi kuwa mfano wa kuigwa hata kwa wale viongozi wengine waliopo madarakani...Tuko pamoja ktk kusaidia wale waliokumbwa na mahafa haya yaliyotokana na mvua za siku chache zilizopita hapa Jijini Dar...Jacqueline Moshi

Anonymous said...

Shukran kwa kuonyesha kutujali watu wa jimbo lako. Naomba sinza iwe na sewage system ambayo inaeleweka. Imekua ni kutiririka maji taka kila kukicha hovyo kwa vile hakuna utaratibu mzuri. Sidhan kama tunahitaji serikali katika hili. Tuchangie,tulimalize. Tuamua tunaweza. Natamani kuiona sinza tofauti na hii uliyoirithi kutoka ccm. Asante sana

Mdauwabunju said...

Kazi nzuri Mh Mnyika. Ila naona kama usemavyo, bado wahusika wanalichukulia hili swala la janga na maafa kimzaha mzaha, itabidi wabadilike tu.
Huu ndio ule wakati wa kusema, inatosha, kwa wale waliokuwa wanaishi pembezoni ya mito na mabonde.
Nchi yetu ni kubwa mno, najua hao wananchi watasita kwenda maeneo mapya kwa kisingizio cha miundo mbinu na n.k. Ila hawana njia, itabidi tu wakubaliane nasi.
Kudos Mh Mnyika

Anonymous said...

Pole kwa maafa yalitukmba. Sisi ni wakaazi wa mbezi eneo la Saranga Temboni. Kero(1) yahusu wachimba mchanga katika bonde la eneo maarufu kwa Mangi.Watu hawa wamefanya lile bonde kama ajira yao. Mwenyekiti wa serekali ya Mtaa aliwahi kukemea bila mafanikio, wanaamka saa 7.30 usiku. Wamesababisha hata daraja letu tulilo jenga la mda kwenda na maji sasa hivi, mvua zikinyesha hatu wezi kuvuka kwenda popote.

Anonymous said...

Ndugu Mheshimiwa.
kwanza tunakupa pole kwa kazi ngumu ya ujeni wa Taifa.Nimesoma nimeona sehemunyingi za maafa ulizo tembelea,inaonyesha wazi kwajinsi unavyo jali Watukatikajimbo lako,tunakuomba na sisi Wakaaziwa Mbezi Temboni Mtaa wa Saranga ujekutembelea uonela bonde letu lilivyo haribika, hata barabara yetu imeharibika vibaya sana. lilebonde kuna watu kumi hivi,wanachimba mchanga kwenyebondehilila barabara na kuwauzia watu wa malori, bila kujalikuwa udongo niwakichanga ukiloa maji sehemu ambayo imechimbwa mchanga hatakama nyumba yako ilikua mbali ule ufa tokea Mheshimi kwa pamoja tunakuomba, sisi wakaazi Wasaranga ni watu wahali ya chini na wengine tupo ambao hata shule ya msingi hatukenda ndio maana unakuta tunaharibu mazingira yetu wenyewe bila kujua. Tunaomba utufikishie huu ujumbe kwa Mwenyekiti wa serekali ya Mtaa kwasababu alisha wahi kuwa kataza lakini bado wana leta zarau nakusema hatuchimbi kwako.Wanaume wanauza kwa malori na
kuna wanawake kama watano nao nitishio kwa maneo ya watu wale ambao hawajahamia wanaamka hata saa nane usiku mpaka saa kuminamoja asubuhi,Mheshimiwa wanaotuletea zaidi mmomonyoko wa ardhi hata kwa majina wanajulikana kwavile wamefanya mchanga niajira yao mvua ikinyesha tu kidogo utaona watu na viroba kujakuchimba kwenye mitaa yawenzao. Wako katika ujezi wa Taifa.