Saturday, December 24, 2011

Majina mapya bila mfumo mpya hauwezi kutuhakikisha ufanisi wa tume wala kuwa na chaguzi huru na za haki

Kufuatia Rais Jakaya Kikwete kufanya uteuzi wa Mwenyekiti na Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, wadau mbalimbali wametaka maoni yangu kuhusu watu walioteuliwa. Kwa maoni yangu hatupaswi kutoa maoni kuhusu watu walioteuliwa kwa sababu matatizo ya tume yetu ya uchaguzi ni ya mfumo mzima. Hivyo, uteuzi wa mwenyekiti na mkurugenzi mpya wa tume ya uchaguzi hauwezi kuleta mabadiliko yoyote ya maana katika utendaji wa tume ya uchaguzi wala hauwezi kuisaidia tume hiyo kuweza kuaminika na umma. Majina mapya bila mfumo mpya hauwezi kutuhakikisha ufanisi wa tume wala kuwa na chaguzi huru na za haki.

Uteuzi huu mpya hauwezi kuhakikisha watanzania kuwa na chaguzi huru na haki katika chaguzi za marudio zinazotarajiwa kufanyika, wala hauwezi kuleta uchaguzi huru na haki wakati wa kura za maoni za kufanya maamuzi ya kuhalalisha katiba mpya wakati wa mchakato wa mabadiliko ya katiba kwa mujibu wa sheria ya mabadiliko ya katiba ya mwaka 2011.

Pia, uteuzi wa mwenyekiti na mkurugenzi mpya wa tume ya uchaguzi hautaweza kuhakikisha Tanzania inakuwa na uchaguzi huru na wa haki kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Hivyo, wananchi na wadau wote badala ya kupongeza uteuzi uliofanyika tunapaswa kuunganisha nguvu ya umma kuendelea kudai mabadiliko ya mfumo mzima wa uchaguzi ikiwemo utaratibu mzima unaoongoza uteuzi. Kwa sasa Rais Kikwete amepewa mamlaka makubwa ya uteuzi kwa mujibu wa katiba na mamlaka hayo ameyakuwa akiyatumia vibaya kufanya teuzi mbalimbali bila kuzingatia ridhaa ya umma na maslahi ya taifa kwa ujumla.



Uteuzi huu umedhihirisha mashaka ambayo wadau mbalimbali wamekuwa nayo juu ya mamlaka makubwa ya Rais katika mchakato wa mabadiliko ya katiba na pia katika masuala ya uchaguzi. Chini ya tume hii ya uchaguzi pamoja na uteuzi mpya uliofanyika maoni yatakusanywa na tume iliyoteuliwa na rais na katiba ikishatungwa na bunge la katiba itapitishwa kwa kupigiwa kura ambazo zitasimamiwa na tume hii hii ya uchaguzi ambayo imeteuliwa na Rais. Hivyo, tukiacha mfumo huu ukaendelea kama ulivyo tutapata katiba mpya kwa jina lakini katiba mbovu isiyokuwa na muafaka wa kitaifa kwa kuwa watanzania wengi hatuna imani na mfumo mzima wa sasa wa tume ya uchaguzi. Aidha, tume hii iliyoteuliwa na Rais ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM bila mapendekezo kutoka kwenye chombo chochote na bila uteuzi wake kuidhinishwa na chombo chochote itakwenda kusimamia uchaguzi katika mazingira yasiyokuwa huru na haki na hivyo kufanya uchakachuaji wa kura kama ilivyokuwa kwenye uchaguzi wa mwaka 2010. Katika mazingira haya, badala ya kutoa maoni kuhusu majina ya watu walioteuliwa tuitake serikali ifanye mabadiliko ya kikatiba na pia ifanye mabadiliko ya sheria ya uchaguzi ili mfumo mpya uwepo ambao utafanya uteuzi uweze kuwa wa kuamininiwa na wenye tija.

Ni muhimu tuijadili mifumo ya kisheria na kiuchaguzi kwa ajili ya uchaguzi na Muundo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Pamoja na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sheria mbalimbali zimekuwa zikisimamia uchaguzi hususani: Sheria ya Uchaguzi na. 1 ya mwaka 1985; Sheria ya Vyama vya siasa na. 5 ya mwaka 1992 na Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambazo zimetoa mamlaka kwa tume kusimamia na kuratibu uchaguzi ikiwemo kutoa maelekezo na taratibu mbalimbali.

Muundo wa Tume unatokana na Katiba Kifungu 74(1) kama ilivyofanyiwa marekebisho na Sheria na. 4 ya 1992 na Sheria na. 7 ya mwaka 1993; Tume inateuliwa na Rais(Katiba na Sheria husika zimeeleza sifa za wanaoweza kuteuliwa). Mkurugenzi wa Uchaguzi naye anateuliwa na Rais kwa mapendekezo ya Tume. Katiba kifungu 74 imebainisha majukumu ya Tume ya Uchaguzi. Wadau mbalimbali kwa nyakati tofauti wamekuwa wakidai tume huru ya uchaguzi wakati wa marekebisho ya 14 ya katiba yaliyofanyika karibu na uchaguzi mkuu wa 2005. Hata hivyo suala la muundo wa tume huru ya uchaguzi halikujadiliwa wala kuingizwa kama sehemu ya marekebisho hayo. Matokeo yake maandalizi ya chaguzi za 2005 na 2010 yalifanywa na tume ile ile ambayo ilisemwa kipindi chote kwamba haiko huru. Kamati mbalimbali ziliundwa na kufanya kazi kipindi cha uchaguzi pekee. Uteuzi huu wa Rais umeendeleza hali hiyo ambayo imekuwa ikilindwa kwa muda mrefu.

Marekebisho ya sheria ya uchaguzi yaliyofanyika mwaka 2010 hayakubadili misingi ya muundo wa tume ya uchaguzi badala yake yalitoa tu mamlaka ya kuteua wasimamizi wa uchaguzi kutokana na ofisi au sifa zao tofauti na ilivyo ambapo tume huteua wasimamizi wa uchaguzi kutokana na ofisi pekee. Upenyo wa tume kuachiwa kuamua kati ya vyeo na sifa unatoa mianya ya kuruhusu hujuma. Mathalani, katika uchaguzi wa serikali ya mitaa wa mwaka 2009 pamoja na kuwa haukusimamiwa na tume; kanuni za uchaguzi huo zilitaja kwamba wasimamizi wa uchaguzi wangeteuliwa kwa cheo au kwa sifa; matokeo yake idadi kubwa iliteuliwa kutokana na vyeo ndio maana uchaguzi husika kwa sehemu kubwa ulisimamiwa na watendaji wa serikali kwa nafasi zao. Hali hii ilidhihirika pia katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 ambapo chaguzi tume iliangalia vyeo na kuteua wakurugenzi na maafisa watendaji wa kata kusimamia uchaguzi badala ya uteuzi kuegemea zaidi katika sifa na kuepuka kuwateua watendaji wa serikali. Matokeo yake ilikuwa na uchakachuaji katika maeneo kadhaa na mivutano katika maeneo mbalimbali ya nchi wakati wa ujumlishaji wa kura na utangazaji wa matokeo.

Hivyo, badala ya kujadili majina ya watu walioteuliwa tuitake serikali kufanya mabadiliko ya kimfumo katika katiba na sheria kwa kuzingatia yafuatatayo: Pawepo na Sheria ya Tume ya Uchaguzi ili kuipa uhuru na mamlaka zaidi tume ya uchaguzi kama ilivyo katika nchi kadhaa za Kusini mwa Afrika.(Pendekezo hili limetolewa pia na Tume ya Uchaguzi na Vyombo mbalimbali vya Ufuatiliaji/Uangalizi wa uchaguzi).
Katiba na Sheria vifanyiwe mabadiliko/marekebisho ili kutoa uhuru na mamlaka ya Tume ya Uchaguzi wa Kuzingatia vigezo vya Kanuni/Matamko na Misingi mbalimbali ya Uchaguzi ya Kimataifa ambayo taifa letu limeridhia. Baadhi ya masuala mahususi ni pamoja na: Tume iwe nje ya mfumo wa kiutendaji wa kiserikali(Watendaji wa Serikali kama Wakurugenzi na Watendaji wa Kata wasiwe watumishi wa Tume ya uchaguzi hata wakati wa uchaguzi); Wajumbe wa Tume wachaguliwe kwa mashauriano na Wadau wengine vikiwemo vyama vya siasa na baadaye wathibitishwe na Bunge; mwenyekiti achaguliwe na wajumbe hao miongoni mwao badala ya kuteuliwa na Rais kama ilivyo sasa; Utumishi wa Wajumbe waandamizi wa Tume wa ulindwe(durability and security of tenure) kisheria na kikatiba kama walivyo majaji; Uwakilishi wa Tume uzingatie jinsia, uwakilishi wa kijamii na makundi rika; Tume ya Uchaguzi iwajibike kwa Bunge badala ya Kuwajibika kwa Serikali; Tume ya Uchaguzi iwe na Bajeti inayojitegemea itakayopitishwa moja kwa moja na Bunge. Kamati za Tume ziwe ni za kudumu; ziendelee na kazi hata baada ya uchaguzi. Vitengo vya TEKNOHAMA (ICT) na Elimu ya Uraia viwe sehemu ya vitengo vya kudumu vya Tume.

Tume ya Uchaguzi iwe na watendaji wa Kudumu katika ngazi mbalimbali; utaratibu wa kuwatumia maofisa wa serikali kama wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi usitishwe. Hii ihusishe kuwezesha bajeti ya Tume ya uchaguzi iwekewe fungu pekee kutoka katika mfuko mkuu wa fedha za umma(consolidated fund) badala ya kuwa sehemu ya bajeti za kawaida za wizara.Hivyo mjadala utakaowezesha kuunganisha nguvu za kidemokrasia na kimaadili ili kudai na kushawishi mabadiliko ya sheria za uchaguzi na mazingira ya kisiasa ikiwemo wenye kuboresha usimamizi wa uchaguzi ni muhimu uendelezwe hata baada ya Rais kuteua mwenyekiti na mkurugenzi mpya.

John Mnyika (Mb)

1 comment:

Francis Morris said...

Great analysis Mnyika, a transparent and independent election management body is what we highly need!