Friday, December 16, 2011

Taarifa ya Mkutano wa Kanda Maalum DSM

Taarifa inatolewa kwa viongozi, wanachama na wapenda demokrasia na maendeleo wa Jiji la Dar es salaam na Manispaa kuhusu Mkutano Mkuu wa CHADEMA wa Kanda Maalum Dar es salaam.

Mkutano huo utafanyika jumapili ya tarehe 18 Disemba 2011 kuanzia saa 4 kamili asubuhi katika Ukumbi wa Kilamuu ulioko Mbezi jijini Dar es salaam.

Washiriki wa mkutano huo ni viongozi wa chama wa Mikoa ya kichama ya Temeke, Ilala, Kinondoni na wajumbe wa mikutano mikuu ya majimbo yote ya jiji la Dar es salaam. Aidha, waalikwa katika mkutano huo ni pamoja na viongozi wa kuchaguliwa katika ngazi mbalimbali, viongozi wilaya, kata na wawakilishi wa matawi mbalimbali.

Taarifa zaidi kuhusu ushiriki wa wanachama na wapenda demokrasia na maendeleo katika mkutano husika zinatolewa katika ofisi mbalimbali za chama katika ngazi za mikoa, wilaya/majimbo ya kanda maalum ya Dar es salaam.

Ajenda za Mkutano huo ni waraka na. 1 na 2 wa chama wa mwaka 2011 kuhusu uchaguzi ndani ya chama na waraka na. 3 wa mwaka 2011 kuhusu Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011. Mgeni rasmi katika Mkutano huo ni Katibu Mkuu wa CHADEMA Dr Wilbroad Slaa ambaye pia atashiriki katika kutoa mada.

Mkutano huu ni sehemu ya utekelezaji wa malengo ya mpango mkakati wa CHADEMA wa mwaka 2011 mpaka 2016 ambapo umeweka mkazo kwa chama kufanya mikutano katika ngazi mbalimbali kwa ajili ya ujenzi wa chama pia kwa ajili ya kushughulikia masuala muhimu ya kitaifa.

Katika ajenda ya waraka namba 1 na 2 Mkutano utapokea na kujadili maelezo na maelekezo mbalimbali kuhusu maandalizi ya uchaguzi wa ndani ya chama katika ngazi mbalimbali.

Ajenda ya Waraka namba 3 ni sehemu ya utekelezaji wa azimio la Kamati Kuu la tarehe 20 Novemba 2011 ambayo iliwaagiza viongozi wote wa chama na wa kuchaguliwa wa ngazi zote nchi nzima kufanya mikutano ya ndani na ya hadhara kwa lengo la kuwaelimisha wananchi juu ya sheria ya Mabadiliko ya Katiba na madhara yake kwa mchakato wa kupata katiba mpya na bora kwa nchi yetu ili kuunganisha umma wa watanzania kuweza kufanya mabadiliko ya msingi. Kamati Kuu ilizingatia kwamba sheria husika ilisomwa na kujadiliwa kwa mara ya pili bila ya wananchi kushirikishwa kwa ukamilifu kutoa maoni yao na muswada kuboreshwa kwa kuzingatia makubaliano ya kitaifa kuhusu mchakato wa katiba mpya.

Aidha Kamati Kuu iliazimia kwamba CHADEMA itaendelea kutoa elimu kwa wanachama, wananchi na wadau wote juu ya ubovu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na juu ya haja ya kuwa na sheria itayoweka utaratibu bora zaidi wa kuunda Tume Shirikishi ya Katiba kwa lengo kukusanya maoni ya wananchi, kuandaa ripoti na rasimu ya katiba mpya, Bunge Maalum la Katiba na usimamizi wa kura ya maoni itayowezesha wananchi kufanya maamuzi kwa uhuru na kwa haki.

Ikumbukwe kwamba kwa mujibu wa waraka na. 4 wa mwaka 2007 chama kilielekeza kwamba Hoja ya Mabadiliko ya Katiba ya Nchi kuwa ya kudumu katika vikao vya kikatiba vya chama pamoja na mikutano na wananchi mpaka pale taifa letu litakapokuwa na katiba mpya.

Maandalizi ya Mkutano huo ni matokeo ya kikao cha pamoja cha viongozi wa Mikoa ya kichama, wilaya za kichama, na majimbo ya kiuchaguzi ya Kanda Maalum ya kichama ya Dar es Salaam.

John Mnyika (Mb)
Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Mikoa ya Kanda Maalu ya Dar es salaam
Na Mwenyekiti wa Mkoa wa Kichama wa Kinondoni.
16/12/2011

No comments: