Tuesday, February 14, 2012

DAWASCO kutozingatia ratiba ya mgawo wa maji

Mbunge wa Ubungo, John Mnyika ametoa mwito wa Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASCO) kutoa taarifa kwa umma kuhusu kutozingatiwa kwa ratiba ya mgawo wa maji katika Jiji la Dar es salaam hali ambayo imesababisha kero ya maji katika maeneo mbalimbali ya jimbo la Ubungo.

Mnyika ametoa mwito huo kupitia kwenye barua yake kwa DAWASCO aliyoiwasilisha leo tarehe 14 Februari 2012 na kutoa rai kwa madiwani wa CCM na CHADEMA katika Jimbo la Ubungo kuwasilisha taarifa za hali ya maji katika kata zao kufuatia malalamiko ya wananchi.

Itakumbukwa kwamba tarehe 5 mwezi Septemba 2011 Mbunge Mnyika alifanya mkutano na Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASCO akiwa na baadhi ya wakazi wa kata mbalimbali kuhusu hali ya upatikanaji wa maji katika Jimbo la Ubungo.

Kufuatia mkutano huo DAWASCO ilichukua hatua mbalimbali ambazo ziliboresha mgawo wa maji katika maeneo kadhaa ya Jimbo la Ubungo katika kipindi cha mwishoni mwezi Septamba mpaka katikati ya mwezi Disemba mwaka 2011.


Hata hivyo, kuanzia mwishoni mwa mwezi Disemba 2011 mara baada ya maafa ya mafuriko katika Mkoa wa Dar es salaam mpaka sasa katikati ya mwezi Februari 2012 mbunge Mnyika amepokea malalamiko mbalimbali toka kwa wananchi kuwa hali ya upatikanaji wa maji katika kata mbalimbali za Jimbo la Ubungo sio nzuri kama ilivyokuwa baada ya maandamano.

Aidha, mbunge Mnyika amehitaji maelezo na vielelezo kuhusu maeneo ambayo hakuna miundombinu ya maji kabisa au miundombinu iliyopo haijawahi kutoa maji kwa kipindi kirefu kwa ajili ya kutaka hatua za ziada kutoka kwa DAWASA na Wizara ya Maji.

Imetolewa tarehe 14 Februari 2012 na:

Aziz Himbuka

Katibu Msaidizi

Ofisi ya Mbunge Ubungo

1 comment:

Anonymous said...

tatizo la maji sehemu nyingi za ubungo ni mbaya sana sababu maji yanaweza kutoka hata baada ya wiki tatu na yakitoka yanakatika baada ya saa moja. inabidi suluhisho lipatikane