Saturday, February 11, 2012

Nilitaka bunge likae kama kamati ya mipango kuchukua hatua za kunusuru uchumi na kupunguza mfumuko wa bei

Katika kuendelea kutimiza wajibu wa kuisimamia serikali kushughulikia uchaifu wa uchumi wa nchi yetu wa urari tenge kutokana na kuagiza bidhaa nyingi toka nje na upungufu katika uzalishaji na usambazaji wa ndani na kupanda kwa gharama za maisha kwa wananchi nilihoji uongozi wa serikali na bunge sababu za bunge kutokukaa kama kamati ya mipango kama kanuni za bunge zinavyohitaji na badala yake kufanyiwa semina ya hali ya uchumi tarehe 8 Februari 2012.

Nilieleza bayana kwamba matarajio yangu katika mkutano huu wa sita wa bunge ilikuwa ni serikali kuwasilisha bungeni mpango wa haraka wa kunusuru uchumi wa nchi, kupunguza mfumuko wa bei na kudhibiti kuporomoka kwa thamani ya shilingi yetu ukilinganisha na sarafu nyingine badala ya semina ya hali ya uchumi ambapo mada zinaweza zikatolewa na wabunge wakatoa maoni mazuri lakini yasiingizwe katika utekelezaji ya kiserikali na bajeti ya taifa.

Kanuni ya 94 ya Kanuni za Kudumu za Bunge inaelekeza “Ili kutekeleza majukumu yaliyoanishwa katika ibara ya 63(3) (c) ya katiba, Bunge litakaa kama Kamati ya Mipango katika Mkutano wake wa Mwezi Februari ili kujadili na kushauri kuhusu mapendekezo ya Serikali katika mwaka wa fedha unaofuata”.

Pamoja na kuhoji ni lini mpango utaletwa na kujibiwa na Waziri wa Fedha Mustapha Mkullo na Spika wa Bunge Anna Makinda kuwa mpango utajadiliwa katika Mkutano wa Saba wa Bunge mwezi Aprili; nilitoa pia mawazo yangu kuhusu hatua ambazo zinapaswa kuchukuliwa na serikali kwa haraka kupunguza mfumuko wa bei nchini na kudhibiti kupanda kwa gharama za maisha kwa wananchi hali ambayo ni tishio kwa uchumi na usalama wa nchi na maisha ya wananchi kwa ujumla.


Nilihoji hali hiyo kwa sababu majibu ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Waziri wa Fedha Mustapha Mkullo kwa nyakati tofauti bungeni alhamisi tarehe 2 Februari 2012 yalionyesha kwamba serikali haina mkakati wa kunusuru uchumi wa nchi, kupunguza mfumuko wa beina kukabiliana na ongezeko la gharama za maisha kwa wananchi.

Dalili za hali hiyo ni kwamba hata Rais Jakaya Kikwete amekwepa kwenye ‘sherehe’ za CCM za tarehe 5 Februari 2012 kuzungumzia jinsi yeye na chama chake walivyotekeleza ahadi ya maisha bora kwa kila mtanzania ambayo sasa Waziri Pinda anakwepa serikali na chama hicho kuwajibika katika utekelezaji wake kama walivyoahidi.

Miezi zaidi ya miwili imepita toka Waziri wa Fedha Mustapha Mkullo atoe ahadi kwa niaba ya serikali kuwa mpango kabambe unatarajiwa kupitishwa kuboresha uchumi na kupunguza gharama za maisha; hivyo natoa mwito kwa Waziri Mkullo kueleza mpango huo umefikia wapi ili kunusuru maisha ya wananchi.

Itakumbukwa kwamba Tarehe 28 na 29 Oktoba 2011 Waziri wa Fedha Mustapha Mkullo alinukuliwa na vyanzo mbalimbali akieleza kwamba mpango kabambe unatarajiwa kupitishwa na baraza la mawaziri kuboresha uchumi na kupunguza gharama za maisha.

Kauli hiyo ya Waziri Mkullo aliitoa siku chache baada ya mkutano wangu na waandishi wa habari wa tarehe 23 Oktoba 2011 ambao nilitoa mwito kwa Rais Jakaya Kikwete kuitisha kikao cha dharura cha tume ya mipango na baraza la mawaziri kupanga mpango wa dharura na wa muda mrefu wa kupunguza gharama za maisha kwa wananchi kwa kudhibiti mfumuko wa bei pamoja na kuporomoka kwa shilingi ya Tanzania. Aidha, nilitoa mwito pia kwa bunge kuingilia kati kupitia kamati zake za kisekta na hatimaye kwa serikali kuwasilisha bungeni mpango wa kukabiliana na matatizo husika ya kiuchumi ambayo ni hatari kwa usalama wa nchi na maisha ya wananchi.

Serikali inapaswa kupeleka Mpango wa dharura wa kuimarisha uchumi na kupunguza gharama za maisha bungeni katika mkutano wa bunge unaoendelea hivi sasa badala ya kufanya semina tu ya wabunge kuhusu hali ya uchumi ya nchi.

Narudia tena kutahadharisha kwamba hali ngumu ya maisha kutokana mfumuko wa bei na kuporomoka kwa sarafu yetu ni tishio kwa uchumi na usalama wa nchi na maisha ya wananchi.

Ikumbukwe kwamba bidhaa zinazochangia kwa kiwango kikubwa mfumuko wa bei ni vyakula na nishati hususani matatizo ya umeme na gharama kubwa za mafuta na gesi asilia. Aidha, kuporomoka kwa thamani ya shilingi kunachangiwa na mahitaji makubwa ya dola miongoni mwa waagizaji wa bidhaa toka nje na urari hasi wa biashara kutokana na upungufu wa mauzo ya bidhaa zetu katika masoko ya kimataifa.

Pamoja na kuchukua hatua za dharura za kuchochea ongezeko la uzalishaji katika kilimo na viwanda na kuwezesha udhibiti wa bei ya bidhaa muhimu kukabiliana na kupanda kwa gharama za maisha kunakosababishwa na mfumuko wa bei na kuporomoka kwa sarafu ya Tanzania pamoja na; serikali inapaswa kuitumia sekta ya madini katika kunusuru uchumi wa taifa na maisha ya wananchi.

Izingatiwe kwamba mfumuko wa bei nchini pamoja na kusababishwa na kupungua kwa uzalishaji unachangiwa pia na nakisi ya bajeti pamoja na udhaifu katika matumizi ya serikali wakati kuporomoka kwa sarafu kunatokana pia na ongezeko la mahitaji ya fedha za kigeni kwa ajili ya ongezeko la uagizaji wa mafuta na malighafi nyingine toka nje.

Hatua tatu za kifedha ambazo zimechukuliwa na benki kuu katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita hazijaweza kuimarisha kikamilifu sarafu yetu badala yake; hali ambayo inahitaji hatua za ziada na za haraka kuchukuliwa na mamlaka zingine za kiserikali kwa kushirikiana na sekta binafsi.

Hatua hii iende sambamba na kupunguza matumizi ya anasa pamoja na kuvitumia vyanzo mbadala vya mapato vilivyoelezwa na kambi ya upinzani ili kupata fedha za nyongeza za kuingiza katika mpango wa dharura wa kudhibiti mfumuko wa bei na kuporomoka kwa shilingi. Hata hivyo, udhibiti wa ziada unahitajika katika kutekeleza mipango yote ya dharura ili kuepusha mianya ya ufisadi kama ilivyokuwa katika miradi ya kufua umeme IPTL, Alstorm Power Rentals, Richmond na fedha za kuchochea uchumi (Stimulus Package).

Imetolewa na Mbunge wa Jimbo la Ubungo na Waziri Kivuli wa Nishati na Madini.



No comments: