Sunday, February 5, 2012

Kutoka Bungeni: Mgomo wa Madaktari; bado hakijaeleweka

Nashukuru kwamba walau tofauti na tarehe 02/02/2012 ambapo Naibu Spika Ndugai alipotosha muongozo nilioomba akadai kuwa ni hoja isiyoungwa mkono na kuipuuza; tarehe 03/02/2012 amezingatia muongozo nilioomba na kutoa mwelekeo ambao umeongeza msukumo katika bunge kufanya kazi yake ya kuisimamia serikali.

Hata hivyo, bado muongozo uliotolewa haujitoshelezi kwa kuwa jukumu hilo kwa kamati ya huduma za bunge halikuelezwa bayana limeanza lini na litamalizika lini. Vyanzo kadhaa vimeeleza kwamba taarifa ya kamati husika itawasilishwa kwenye mkutano ujao wa bunge (Mkutano wa Saba), suala ambalo halipaswi kukubaliwa. Kutokana na uzito na udharura wa mgogoro huu ni muhimu taarifa ya awali ya kamati iliyopewa jukumu ikawasilishwa katika mkutano huu wa sita unaoendelea ili hatua za haraka zikachukuliwa katika kushughulikia madai ya madaktari na kupata taarifa ya kweli kuhusu athari za mgogoro na mgomo ulioendelea ikiwemo vifo vilivyotokea.

Aidha, Kamati husika ingepewa hadidu rejea za wazi ikiwemo ya kufanya kazi ya usulushi na upatanishi katika mgogoro ambao umetokea baina ya madaktari na serikali na pia kuwezesha bunge kusimamia ipasavyo na kwa haraka serikali katika kushughulikia madai ya wafanyakazi.

Kwa upande mwingine, kwa kuwa imebainika wazi kwamba kuna uzembe na udhaifu miongozi mwa watendaji wakuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii wakiongozwa na Waziri wa Wizara husika ambaye amefikia hatua hata ya kutoa taarifa ya kulidanganya bunge; ni vizuri baada ya Kamati husika kusikiliza pande zote mbili Waziri na watendaji husika walazimishwe kujiuzulu ili hatua za kushughulikia madai ya madaktari na kuboresha huduma za afya katika hospitali za umma zitekelezwe na wateule wengine wenye uwezo na dhamira ya kweli ya kushughulikia matatizo yaliyojitokeza.


Itakumbukwa kwamba Juzi (03/02/2012) kabla ya kusomwa kwa kauli ya serikali kuhusu mgomo wa madaktari niliomba muongozo wa Spika kwa mujibu wa kanuni ya 5 ambayo inamtaka Spika kuendesha bunge kwa kuzingatia kanuni na pale ambapo kanuni hazijaelekeza kutumia sheria, katiba, maamuzi yaliyopita ya bunge na mila na desturi za kibunge. Nilitumia kanuni hiyo kutaka Naibu Spika Job Ndugai atoe muongozo ili kuwezesha badala ya kufuata masharti ya kanuni ya 49 pekee ambayo inasema kauli ya serikali ni ya jambo linaloihusu serikali na lisilozua mjadala afuate katiba ya nchi na maamuzi mengine ya bunge ili maudhui ya kauli hiyo ya serikali yaweze kujadiliwa na bunge.

Nilinukuu ibara ya 63 (2) ya katiba ambayo inasema mamlaka ya bunge ni kuisimamia serikali na kwamba katika suala la mgomo wa madaktari ni muhimu bunge likachukua wajibu huo kwa sababu kauli itakayotolewa inahusu serikali wakati mgomo wenyewe unaathari kwa wananachi hivyo wabunge kama wawakilishi wa wananchi wanapaswa kupewa fursa ya kuisimamia serikali katika suala hilo linalohitaji hatua za dharura. Aidha, nilieleza kwamba kauli ya serikali inaihusu serikali ambayo katika mgogoro na madaktari na yenyewe ni mtuhumiwa hususani Wizara ya Afya na Ustawi wa jamii ambayo Waziri na watendaji wake wameonyesha udhaifu katika kushughulikia mgogoro na madai ya madaktari hivyo bunge linapaswa kujadili ili kuweza kuwawajibisha.

Baada ya kauli ya Serikali Naibu Spika Job Ndugai alitoa muongozo ambao alieleza kwamba ni kweli kauli za mawaziri hazijadili lakini akaelekeza kwamba kauli hiyo ipelekwe kwenye Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii ili ichukue hatua ‘haraka iwezekanavyo’ na hatimaye kuleta taarifa bungeni. Katika maelezo yake alieleza kwamba kuna haja ya kanuni za bunge kubadilishwa lakini pia alieleza kwamba kuna watendaji wa serikali wamelalamikiwa kuhusu suala la mgomo wa madaktari.

Tayari imeeelezwa kwenye vyombo vya habari kwamba Kamati husika ya Bunge itakutana na madaktari kesho (06/02/2012) na kwamba madaktari kwa upande wao nao wameonyesha nia ya kukutana na kamati hiyo.

Kama tulivyoanza awali, tutaendelea kufuatilia suala hili hatua kwa hatua mpaka kieleweke.

John Mnyika (Mb)
Bungeni-Dodoma (05/02/2012)

2 comments:

Peasant Child said...

John Tatizo sio waziri tatizo ni mfumo nzima wa serikali na chama tawala. Maana waziri anategemea hela kutoka serikalini kuboresha maslahi ya madaktari lakini serikali nzima ambayo waziri anafanyia kazi haina nia ya kuboresha maslahi ya madaktari na watumishi wegine wa umma. Kibaya zaidi kwa nchi yetu waziri anamua kuendelea kushikilia kiti chake cha uwaziri hata kama anaona hawezi kutekeleza majukumu yake kwa sababu ya maslahi yake binafsi. Ndiyo maana hapa Tanzania sijawahi kusikia mtu ambaye amewahi kukataa uwaziri mpaka afukuzwe na rais au amepata tuhuma akajiuzulu. Waziri lazima akomaa maana mabosi wake wanaponda raha kwanini yeye aachie.Wananchi tungepaswa kuaandamana kuishinikiza serikali, lakini tumekaa kimya!

Kelkaf said...

Peasant Child umesema ukweli saana na kama alivyowahi kusema Godbless Lema kuwa "kuna watu wanahitaji ukombozi wa kifikra", na nnadhani baadhi ya wahitaji wa ukombozi huu ni viongozi kama hawa.Lakini kuna vitu vinaitwa uzalendo,utu na uadilifu (k)wako binafsi na kwa watu unaowatumikia na ninatia mashaka sana uzalendo,utu na uadilifu wa kiongozi wa aina hii kwake binafsi na kwa watanzania wote.