Thursday, March 29, 2012

Mnyika: Mpango wa Dharura wa Umeme


Utekelezaji wa Mpango wa dharura wa umeme unasuasua kutokana ombwe la uongozi katika serikali inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete hususan udhaifu wa kiuratibu ulioonyeshwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda na uzembe wa kiutendaji wa Wizara ya Nishati na Madini.

Izingatiwe kwamba kwa nyakati mbalimbali kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni Freeman Mbowe na Waziri Kivuli wa Nishati na Madini kwa nyakati mbalimbali tulieleza umuhimu wa serikali kuchukulia dharura ya umeme kwa uzito wake na kuunda chombo maalum kitakachohusisha wadau na kupewa msukumo na uongozi mkuu wa nchi katika kupanga na kutekeleza mkakati wa taifa wa kuondoa janga hili linalojirudia.

Hata hivyo, Waziri Mkuu Pinda mara zote alikataa mapendekezo hayo huku akisema kwamba serikali iwajibike iwapo itashindwa kutekeleza mpango huo kwa wakati. Kwa upande wake Waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja naye alieleza bungeni kuwa baada ya mpango huo kupita na kuwa na uhakika wa fedha kutoka Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na mabenki binafsi miradi hiyo yote itatekelezwa kwa wakati.

Kutokana na mipango hiyo kutotekelezwa kwa wakati Waziri Mkuu Pinda na Waziri Ngeleja kukiri kwamba walitoa taarifa potofu kwa bunge na kwa umma ilibidi hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kurekebisha mwelekeo wa mambo katika utekelezaji wa Mpango wa dharura wa umeme.
Izingatiwe kuwa matatizo ya sasa ni matokeo ya udhaifu wa kisera na kiutendaji kuanzia wakati wa Rais wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi na baadaye kwa Rais awamu ya tatu Benjamin Mkapa ambapo TANESCO iliwekwa kwenye orodha ya mashirika ya kubinafsishwa na hivyo serikali kuacha kuwekeza kikamilifu katika uzalishaji wa umeme pamoja na matengenezo ya miundombinu ya usafirishaji na usambazaji. Aidha, ni katika kipindi hicho hicho kuliibuka matatizo pia ya ufisadi kwenye uwekezaji katika sekta ya nishati kama ya IPTL, Kiwira, Net Group Solution nk. Awamu ya nne ya Rais Kikwete nayo ikaongeza zaidi mzigo kwa TANESCO kupitia miradi mingine ya kifisadi kama ya Richmond/Dowans na mengine.

Izingatiwe kwamba udhaifu huu wa mahitaji ya umeme wa dharura mwaka 2006 ulizaa kashfa ya kampuni ya kufua ya Richmond ambayo ilisababisha Waziri Mkuu wa wakati huo Edward Lowassa kuhusishwa na kulazimika kujiuzulu mwaka 2008.

Kati ya maazimio ya mwaka huo 2008 ilikuwa ni pamoja na serikali kuwekeza katika miradi mipya ya uzalishaji wa umeme hata hivyo toka wakati huo mpaka sasa maazimio hayo hayakutekelezwa kwa ukamilifu hali ambayo imeliingiza taifa katika dharura nyingine ya umeme.

Pamoja na kuwa na mpango wa gharama kubwa wa dharura ambayo unahusisha kwa sehemu kubwa suluhisho la muda mfupi la kukodi mitambo, bado utekelezaji wa mpango wenyewe nao unasuasua hali inayodhihirisha kuendelea kwa uzembe na udhaifu katika serikali.

Mpango wa Dharura uliwasilishwa bungeni tarehe 13 Agosti 2011, ahadi ya serikali ilikuwa kuongeza MW 572 ifikapo mwezi Disemba 2011. Serikali ieleze ukweli wananchi kuwa kiwango hicho mpaka sasa Mwezi Machi 2012 hakijafikiwa; mitambo ya dharura iliyofungwa mpaka sasa ni yenye uwezo wa MW 342.

Hata hivyo iliyofungwa nayo haina uhakika wa kuwa na uwezo wa kuendeshwa wakati wote uliopangwa kwa kuwa mpaka TANESCO inadaiwa na makampuni ya kufua umeme wa dharura shilingi Bilioni 105 huku ikiwa na madeni mengine kiasi cha shilingi Bilioni 164 na hivyo kufanya jumla ya madeni ya TANESCO kufikia Bilioni 269.

Mashaka yanakuwa makubwa zaidi kwa kuwa mpaka sasa TANESCO haijapata mkopo wa Bilioni 408 kutoka katika mabenki uliopaswa kutumika kuendeshea mitambo ya dharura ya IPTL, Symbion, Aggreko na kulipia madeni mengine kutokana na kutokamilisha masharti muhimu ikiwemo ya kupata dhamana kutoka kwenye serikali.

Kuchelewa kwa dhamana hiyo ni udhaifu katika utendaji ambao ulipaswa kushughulikiwa na uongozi mkuu wa nchi kwa kuweka pamoja mamlaka zote zinazohusika ikiwemo Wizara ya Fedha, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wizara ya Nishati na Madini ili kufanya maamuzi ya pamoja ya dharura.

Hali hii inadhihirisha kwa mara nyingine tena udhaifu wa Baraza la Mawaziri ambalo Mwenyekiti wake ni Rais Jakaya Kikwete ambalo tumesisitiza mara kadhaa kuwa linapaswa kufanyiwa mabadiliko kwa kuwa linaingiza nchi katika migogoro ya kiuchumi, kisiasa na kijamii mara kwa mara toka liundwe.

Aidha, Wakati umefika sasa wa kufanya mabadiliko makubwa zaidi kimuundo na kiuongozi katika Wizara ya Nishati na Madini kwa kuwa inashindwa kuhimili mahitaji ya sasa ya sekta nyeti inazozishughulikia za umeme, mafuta, madini na gesi asilia.

Ikumbukwe kuwa Tarehe 8 Disemba 2011 Wizara ya Nishati na Madini ilitoa Taarifa kwa Umma kuhusu Maendeleo ya Sekta ya Nishati na Madini. Kufuatia taarifa hiyo tarehe 14 Disemba 2011 nilitoa tamko la kueleza kushangazwa na ukimya wa serikali mpaka hivi sasa kuhusu haja ya kutoa kwa taarifa kwa umma kuhusu utekelezaji wa mpango wa dharura wa umeme na maendeleo ya sekta ya nishati ambayo inakabiliwa na changamoto nyingi kwa sasa zenye kuathiri uchumi wa nchi na maisha ya wananchi. Iwapo Wizara ingekuchukua hatua thabiti toka wakati huo, hali ya utekelezaji wa Mpango wa dharura wa umeme usingefikia kukwama na kuchelewa kwa kiwango cha sasa.

Kuanzia mkutano wa tano wa bunge ulionza tarehe 8 Novemba 2011 ilitarajiwa kwamba serikali ingetoa taarifa bungeni kwa mujibu wa ibara ya 63 (2) na (3) ya katiba kuhusu mpango wa dharura wa umeme na maendeleo ya sekta ya nishati; hata hivyo suala hilo halikuingizwa kwenye ratiba ya bunge. Baada ya taarifa kutokutolewa bungeni nilitarajia serikali ingetoa taarifa kwa umma lakini serikali haikufanya hivyo hata katika Mkutano wa Sita wa Bunge uliomalizika tarehe 10 Februari 2012.

Ikumbukwe kwamba Mpango wa Dharura ulipowasilishwa bungeni tarehe 13 Agosti 2011 serikali ilieleza kuwa imepanga kuongeza MW 572 ifikapo mwezi Disemba 2011. Kati ya hizo, MW 150 ilikuwa zizalishwe kupitia makubaliano baina ya Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na TANESCO; ilitarajiwa kuzalishwe MW 50 Septemba, MW 50 Oktoba na MW 50 Novemba 2011.

Kimsingi, kauli iliyotolewa bungeni kuwa mitambo ilikuwa imepatikana haikuwa ya kweli hivyo ahadi ya kupata umeme huo ilikuwa hewa. Mpaka sasa hakuna hata MW moja ambayo imezalishwa kwa ushirikiano kati ya NSSF na TANESCO. Ujumbe ulipotumwa Marekani kwenda kuona mitambo iliyokuwa inaelezwa kwamba ipo haikukuta mitambo yoyote, walikuta kampuni ambayo haikuwa na uwezo kama ilivyokuwa kwa Richmond Development LLC; timu hiyo ya wataalamu ilibidi kwenda Ufaransa nako ikakosa mitambo ya dharura. Hivyo, fedha nyingi za umma zimetumika kufuatilia ahadi hewa na umeme mpaka sasa haujapatikana.

Ikumbukwe kwamba mpango mwingine wa muda mfupi ulioelezwa bungeni tarehe 13 Agosti 2011 ni mradi wa kununua mitambo ya MW 100 wa Jacobsen wa gesi asili ambao awali ulikuwa ukamilike 2009/2010 lakini kutokana uzembe ndani ya serikali mradi huo haukukamilika mpaka mwaka 2011. Kuchelewa kwa kununuliwa na kufungwa kwa mitambo hii ambayo ilikuwa ifungwe pale Ubungo ndiko kuliongeza makali ya mgawo wa umeme kuanzia mwishoni mwa 2010 mpaka mwanzoni mwa mwaka 2011.

Baada ya kuchelewa kwa mradi huu serikali ikakubaliana na mkandarasi kuwa mradi huo ukamilike Juni 2012. Kutokana na ahadi ya MW 150 za dharura toka NSSF kuthibitika kuwa ni hewa, serikali ikarudi tena mezani kufanya majadiliano na mkandarasi wa mradi wa Jacobsen ili kuharakisha utekelezaji uzinduliwe mwezi Disemba 2011 wakati wa ‘sherehe’ za uhuru. Hata hivyo, wataalamu hawakumueleza tena ukweli Rais Jakaya Kikwete kwa kuwa matarajio waliyompa ya kuzindua mradi huo wakati wa sherehe za uhuru nayo yamethibitika kuwa hewa kwa kuwa sherehe zimepita bila umeme wa nyongeza. Katika hali ya kukosa maneno, Rais Kikwete alilazimika kurudia mara kwa mara kwamba asingetoa hotuba ndefu uwanja wa taifa kwenye maadhimisho tarehe 9 Disemba katika siku ambayo wananchi walitarajia mkuu wa nchi azungumze masuala makubwa ya kitaifa ikiwemo suala la umeme.

Kwa upande mwingine, udhaifu wa kutokutekeleza mipango ya uzalishaji wa gesi na makaa ya mawe kwa wakati umesababisha utegemezi mkubwa kwenye matumizi ya mafuta katika mitambo ya kuzalisha umeme wa dharura. Zaidi ya nusu ya umeme unaozalishwa nchini hivi sasa ambao ni sawa na takribani MW 660 unazalishwa kwa kutumia dizeli, mafuta ya ndege na mafuta mazito hali ambayo imeongeza mahitaji makubwa ya uagizaji wa mafuta toka nje ya nchi. Hii imesababisha mahitaji makubwa ya fedha za kigeni kwa ajili ya kuagiza mafuta na hivyo kuchangia katika kuporomoka kwa thamani ya shilingi. Aidha, ongezeko kubwa la uagizaji toka nje limeathiri urari wa biashara na hivyo kuchangia katika mfumuko wa bei. Hivyo, watanzania hivi sasa wanabeba mzigo wa kupanda kwa bei za bidhaa na gharama za maisha kwa ujumla kutokana na ufisadi kwenye mikataba, ubadhirifu katika matumizi, uzembe katika uongozi na upungufu katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya serikali kwenye sekta ya nishati.

Pamoja na kuwa ahadi za mpango wa dharura bado hazijatekelezwa kwa ukamilifu wake serikali inaendelea kutumia zaidi ya bilioni 2 kila siku kama gharama za mafuta ya kuzalishia umeme suala ambalo linahitaji kufanyiwa uchunguzi wa kina kuhusu vyanzo vya fedha hizo na uhalali wa matumizi ya miradi ya Aggreko International, Symbion Power LLC na IPTL.


Nilionya bungeni kuhusu gharama kubwa za mpango wa dharura wa umeme na kupendekeza vyanzo mbadala vya fedha ambavyo serikali ilivipuuza. Uamuzi wa kukopa katika mabenki ya biashara kwa ajili ya kugharamia mpango wa dharura wa umeme tayari umeshaanza kuathiri Shirika la Umeme (TANESCO), serikali na utaathiri maisha ya wananchi.

Ikumbukwe kwamba tarehe 15 Julai 2011 nilieleza bungeni vyanzo mbadala vya kuongeza fedha katika bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini bila kuathiri kwa kiwango kikubwa maisha ya wananchi na uchumi wa nchi kwa ujumla. Tarehe 18 Julai 2011 Waziri Mkuu Mizengo Pinda alikubaliana na mapendekezo yetu na hivyo wakati anatoa hoja ya kuahirisha majumuisho ya mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini akaahidi kwenda kukata fedha kwenye posho na matumizi mengine yasiyokuwa ya lazima katika bajeti ya serikali ili kuelekeza fedha kwenye mradi wa dharura wa umeme.

Hata hivyo, tarehe 13 Agosti 2011 Serikali ikageuka na kuleta mpango wa dharura tofauti ambao ulijikita katika serikali kuidhamini TANESCO kwenda kukopa kwenye mabenki ya kibiashara zaidi ya bilioni 400. Siku hiyo nilirudia kumsomea Waziri Mkuu kumbukumbu ya Bunge (Hansard) ya ahadi yake ya tarehe 18 Julai 2011 ambayo haikuitimiza, inaelekea serikali ilitoa ahadi hewa ndio maana haikutaka kabisa kubadili msimamo.

Kusuasua kwa mabenki kutoa mikapo na serikali yenyewe kuchelewa kutoa dhamana kunatokana na mzigo mkubwa wa gharama za uendeshaji unaobebwa na TANESCO ikiwemo kutokana na mikataba ya kifisadi na uzembe wa kutowekeza kwenye sekta hii muhimu kwa wakati hali inaleta kusitasita katika utoaji wa fedha kwa hofu ya mikopo kutokulipika kwa wakati.

Katika hali hii hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa za kuitaka Wizara ya Nishati na Madini kutoa taarifa ya kina kwa umma juu ya hali halisi ya utekelezaji wa mpango wa dharura wa umeme na kudhibiti mianya ya ubadhirifu ambayo imeanza kujitokeza kwa kuzingatia pia mapendekezo ambayo tuliyatoa bungeni.



John Mnyika (Mb)


Waziri Kivuli wa Nishati na Madini


28 Machi 2012

1 comment:

Simbeye said...

I have read your analysis on the state of power in our country. I personally appreciate your effort via your party of the follow-up you have been making; probably we should not be thinking of urging our corrupt ministers and incompetent civil servants to work out the current power problem. Iam of the view that the whole system is corrupt no changes can be made. People should be sensitized on the weaknesses of their leaders via CCM so that a strong party which is people centered for this case CHADEMA to take over. All in all I appreciate your efforts; please keep on working as a team. Tupo pamoja mheshimiwa.