Friday, March 2, 2012

DAWASCO kufuata ratiba ya mgawo, ndani ya wiki moja DAWASA, EWURA na TANESCO nao wachukue hatua

Kazi ya mbunge ni kuwakilisha wananchi na kuisimamia serikali na vyombo vyake kuwezesha maendeleo. Naomba niwape mrejesho kwa muktasari; Machi Mosi tulikuwa pamoja na DAWASCO kwenye kata za Sinza, Makurumla, Mburahati, Msigani, Mabibo, Saranga, Kwembe na Makuburi tukifanya kazi za kuboresha upatikanaji wa maji katika Jimbo la Ubungo.

Itakumbukwa kwamba Septemba 2011 baada ya kwenda DAWASCO na wananchi maji yalianza kupatikana kwa kuzingatia ratiba ya mgawo kwenye maeneo zaidi ambayo hapo awali yalikuwa hayapati mgawo; hata hivyo mara baada ya mafuriko ya Disemba kisingizio cha kuharibika kwa miundombinu kikafanya ratiba husika kutokuzingatiwa kwa mwezi mzima wa Januari na mwezi Februari; hali ambayo ilirejesha kwa kiwango kikubwa pia biashara ya kinyemela ya maji.

Baada ya kuchukua hatua ikiwemo kuiandikia DAWASCO tarehe 14 na hatimaye kuwapa muda siku tatu kutoa majibu kwa umma DAWASCO ilieleza kuwa pamoja na mafuriko ratiba ya mgawo kwenye maeneo kadhaa ya Dar es salaam ilishindwa kuzingatiwa kutopata umeme wa uhakika kwenye mitambo yao ya Ruvu na pia kuharibika kwa pampu moja Ruvu Juu.

Tuliendelea kufuatilia kwa karibu suala hilo na hatimaye DAWASCO ilikamilisha matengenezo ya pampu husika hata hivyo bado kuna maeneo ambayo yalishindwa kupata mgawo kutokana hujuma katika miundombinu zikiwemo za mitandao haramu ya maji katika maeneo mbalimbali.


Kwa kazi iliyofanyika mgawo wa maji umeanza kuzingatiwa kwenye kata mbalimabali, Machi Mosi nilikutana na Wazee, wanawake na vijana kwenye eneo la ofisi ya kata ya Makuburi na waliwaeleza kwamba maji yameanza kutokana mara baada ya ziara niliyofanya, nimepokea pia taarifa kutoka Ubungo Msewe (isipokuwa Golani) kuwa sasa wameanza kupata mgawo wa maji, Kibamba Maji kwa ajili ya majaribio ya mradi wa BTC kwenda Kibwegere na Hondogo yatatolewa kwenye siku ya mgawo wa eneo husika; ofisi ya mbunge Ubungo inaendelea kufanya tathmini katika maeneo mbalimbali kujua kama ratiba ya mgawo wa maji inaendelea kuzingatiwa.

Aidha, kwa kazi ambayo tumeifanya siku hiyo tumeona bayana kwamba mtandao wa biashara haramu ya maji unaohusisha kujiunganisha mabomba ya maji kinyemela nao ni chanzo kingine cha hali iliyojitokeza, natumeona mota hizo maeneo ya kata ya Makurumla hususani mtaa wa Kagera, Makuburi kwenye nyumba yenye matanki yaliyounganishwa chini chini kwa ajili ya biashara ya maji na Kata ya Saranga eneo la Kimara B ambapo mtandao wa maji ulitolewa toka kwenye maeneo ya wananchi na kupelekwa nje ya makazi ya watu kwenye mtandao wa wafanyabiashara wakubwa wa maji. Mitandao hiyo imeanza kukatwa na majalada yamefunguliwa polisi kwa ajili ya wahusika kuchukuliwa hatua za kijinai. Hali hii inashamiri kutokana pia na vishoka na tumekubaliana kwamba kuanzia sasa yoyote anayekwenda kugusa bomba la DAWASA lazima kwamba aripoti kwenye serikali za mitaa na pia popote anapofanya kazi hizo lazima awe na kitambulisho cha DAWASCO na pia kadi ya kazi (job card) yenye saini ya meneja wa eneo ya kueleza aina ya kazi na ruhusa iliyotolewa kuifanya. Iwapo mwananchi yoyote akibaini anayekwenda kinyume na haya ashughulikiwe kama wanavyoshughulikiwa wahalifu wengine.

Katika kazi tulizofanya Machi Mosi, imeonekana bayana kwamba bado yapo maeneo ambayo mtandao wa mabomba ya wachina hautoi maji kutokana na msukumo mdogo na matatizo ya mfumo mzima, kama ilivyo katika majimbo mbalimbali ya Dar es salaam, mathalani Malambamawili, kwa Msuguri, Makoka, nk. Aidha, yapo maeneo ambayo hayakufikiwa kabisa kwenye awamu ya kwanza ya utandazaji wa mabomba husika mathalani ya Msingwa, Mbezi Msumi nk.

Haya ni masuala yanayohusu mwenye mali na miundombinu ambaye ni DAWASA, zaidi ya DAWASCO ambaye ni mwendeshaji. (Maji DSM ni kama duka, kuna mwenye bidhaa ambaye anawajibika kujaza duka lake ili wateja wasikose-DAWASA na muuza duka ambaye ana kazi ya kuuza duka lenye bidhaa chache-DAWASCO malalamiko mengi ya wateja yanamuangikia yeye). Kuhusu maeneo hayo, nimeamua kuongeza msukumo wa ziada niliunza kwa upande wa DAWASCO kuharakisha uwekaji wa miundombinu na kuongeza vyanzo, nimetoa kauli ya kuwataka watoe taarifa kwa umma katika kipindi kisichozidi wiki moja kuhusu hatua ambazo watachukua.

Kwenye kazi tuliyofanya Machi Mosi nao wanapaswa kuweka kipaumbele katika kuhakikisha umeme unakuwepo na wa ubora wa kutosha katika maeneo ya uzalishaji na usafirishaji wa maji; pamoja na kuwataka kueleza wamejipanga vipi kupunguza mgawo wa umeme wenye kuathiri ratiba ya mgawo wa maji, nimewataka pia kueleza hatua ambazo zimechukuliwa kuongeza transfoma yenye nguvu zaidi Kwembe ili kuwezesha pampu ya kusukuma maji Kwembe ambapo mabomba ya maji yameshawekwa kwa ajili ya kusukuma maji kikwazo cha sasa kikiwa ni nguvu ya umeme, aidha wachukue hatua za haraka kukamilisha kuweka umeme maeneo ya pembezoni kama Kimara King’ongo ambapo nguzo zimewekwa kwa miezi mingi kwa ajili ya kwenda kwenye miradi ya maji ambayo iko tayari ikisubiri umeme pekee wananchi waweze kupata huduma ya maji.

Kwa upande mwingine, kuna changamoto kubwa ya ubora na bei ya maji jijini Dar es salaam katika sekta binafsi; bei ya maji iko juu sana hali ambayo inashawishi biashara haramu yenye kuhusisha hujuma katika miundombinu ya maji na ufisadi wenye kuharibu ratiba ya mgawo wa maji ili kupanua soko kinyemela. EWURA ina wajibu kama ilivyo kwenye mafuta na umeme kusimamia sekta ya maji siyo ya umma tu hata binafsi, hata hivyo kwa sasa inasimamia zaidi bei na ubora kwa upande wa mamlaka za umma. Hivyo, nimewataka ndani ya wiki moja watoe kauli kuhusu hatua iliyofikiwa katika kuandaa kanuni za usimamizi wa sekta binafsi ya maji juu ya mfumo wa bei elekezi na viwango vya ubora kama ambavyo mamlaka husika iliahidi kwenye Kongamano la Maji Ubungo mwaka 2011.

Masuala haya yote yanahusu marekebisho ya kimfumo ambayo imekuwa dhaifu kwa kipindi cha takribani miaka 35 chini ya utawala wa CCM, nitaendelea kutimiza wajibu wa kibunge wa kuzisimamia mamlaka husika, ili matatizo ya maji yaliyodumu chini ya uongozi uliopita kwa miaka 50 toka uhuru sasa yapungue katika kipindi cha miaka 5.

Na jana kwenye mkutano na waandishi wa habari nimeeleza bayana kwamba nitakwenda hatua kwa hatua, mamlaka husika zisipochukua hatua kwa haraka nitaelekeza nguvu kwenye Wizara Maji, nayo isipochukua hatua za haraka nitaelekeza nguvu kwa Rais Kikwete ambaye mamlaka zote hizo zinafanya kazi kwa niaba yake, serikali ikiendelea kuwa legelege ikiwemo kushindwa kutimiza ahadi zake yenyewe kwenye suala hili muhimu kwa uhai wa wananchi wa Jimbo la Ubungo na Jiji la Dar es salaam nitaelekeza nguvu kwa wenye mamlaka na madaraka yote; wananchi ambao tunalipa kodi na pia mikopo ya miradi ya maji inaendelea kukopwa kwa jina la nchi yetu wakati utekelezaji ukiwa unasuasua. Taarifa zaidi tutazitoa baada ya kazi tunayoendelea kuifanya. Tuendelee kushauriana na kushirikiana mpaka kieleweke; Maslahi ya Umma Kwanza.

3 comments:

Phiemon Kilibata said...

Asante Mhe. Mbunge. nimesoma kwa makini taarifa yako. Kuna sehemu umesema maeneo ya Msewe yameanza kupata maji iosipokuwa Golani. Umeishia hapo bila kutupa ufafanuzi wa kiufundi uliosababisha hali hiyo. Mimi ni mkazi wa Matete-Golani ambae nimeguswa ndiyo maana naendelea kukusumbua. Nazidi kukupongeza kwa kazi nzuri.
kilibata@iit-tz.com

Anonymous said...

Ndg Phiemon na mi nilikuwa nimemuuliza Mh Mbunge pia swala hilo hilo la Golani kwenye post iliyopita sasa sijui kama anaangalia kwa sababu sikuona amejibu, hili eneo la golani ndo kwenye hujuma kubwa wananchi wanaulziwa maji kwa bei ya juu bila kujua hata ubora wa maji yenyewe (ubora wa maji yanayouzwa kwa wananchi ulitakiwqa uangaliwe pia labda kwa kutoa elimu)Mimi nasikitika sana hili swala la maji katika eneo hili lingeweza kutatuliwa endapo viongozi wa serikali za mitaa wangewajibika, nachelea kusema kwamba kuna baadhi ya viongozi wa serikali za mitaa wanahusika kuwahujumu wananchi kwa kiasi kikubwa sana kwa ajili ya maslahi yao wenyewe. Bomba la wachina limeenda maeneo hayo lkn hatua za kujua kwa nini halitoi maji na kwa nini lilidivage kuelekea maeneo mengine badala ya kwenda kwa wananchi

Anonymous said...

Hongera sana Mh.Mnyika kwa ufuatiliaji wa huduma muhimu kwa wananchi wako.

Ila nakushauri sana kuzipima kauli za uongozi wa dawasco maana ni wababaishaji. Matatizo ya kuharibika kwa pampu huko Ruvu Juu ni mchezo wao wa kujitafutia mahela tu. Nasikia sana meneja wa Ruvu Juu amekimbia kwa wizi alioufanya kupitia kuunga maji ya wizi huko Mlandizi. Sasa kama meneja anaunga maji ya wizi unatarajia sisi wateja wa dar es salaam tutapataje maji?

Uongozi wa dawasco kuanzia mkuu wao ni mafisadi