Saturday, March 31, 2012

Turekebishe kwanza kanuni ndipo tufanye Uchaguzi wa Bunge la Afrika Mashariki!

Siku chache zilizopita tarehe 28 Machi 2012 niliwasilisha kwa katibu wa bunge mapendekezo ya mabadiliko katika Kanuni za Kudumu za Bunge Nyongeza ya Tatu (The East African Legislative Assembly Election Rules) kwa mujibu wa kifungu cha 3 fasili ya 3 (a) ya kanuni husika za bunge toleo la mwaka 2007.

Malengo ya mapendekezo niliyowasilisha ni: Mosi, kupanua wigo na kuboresha mchakato wa upatikanaji wa wajumbe wa kuwakilisha vyama vya upinzani na kambi rasmi ya upinzani bungeni. Pili; kuwezesha uwepo wa uwakilishi wa vijana katika bunge la Afrika Mashariki. Tatu; kupanua wigo na kuboresha mchakato wa upatikanaji wa wajumbe kwa kuzingatia jinsia. Nne; kuanza mchakato wa kufanyia marekebisho kanuni za bunge la Tanzania za uchaguzi wa Afrika Mashariki kwa kuzingatia maudhui ya muswada wa sheria ya uchaguzi wa Afrika Mashariki wa mwaka 2011 uliopitishwa na Bunge la Afrika Mashariki.

Marekebisho hayo yatawezesha kuzingatiwa kadiri iwezekanavyo uwakilishi wa kambi na pande zote (shades of opionion), makundi maalum na uendelevu na kumbukumbu ya kitaasisi (continuity and institutional memory) katika wakati huu ambapo uchaguzi husika una umuhimu wa pekee ambapo jumuiya ya Afrika Mashariki ipo katika soko la pamoja na majadiliano ya kuwa na sarafu moja yanaendelea hali ambazo zina athari kwa nchi na wananchi kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Naelewa kwamba Katibu wa Bunge alitoa Taarifa kwa Umma tarehe 12 Machi 2012 kwamba, Uchaguzi wa wajumbe tisa (9) watakaoiwakilisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki utafanywa na Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, wakati wa Mkutano wake wa Saba utakaofanyika Dodoma, kuanzia tarehe 10 hadi 20 Aprili, 2012.

Hata hivyo izingatiwe kuwa kabla ya tangazo hilo nilishawasilisha barua kwa Katibu wa Bunge tarehe 8 Februari 2012 ya kutaka kufanyike kwa mabadiliko katika kanuni za kudumu za Bunge Nyongeza ya Tatu (The East African Legislative Assembly Election Rules) zinazosimamia uchaguzi husika.

Kutokana na barua hiyo kutokujibiwa mpaka mkutano wa sita wa bunge ulipomalizika tarehe 10 Februari 2012, siku chache baada ya mkutano huo nilitoa mwito kwa Spika wa Bunge Anna Makinda kuwezesha marekebisho ya msingi ya kanuni zinazosimamia uchaguzi husika kabla ya katibu wa bunge kutoa tangazo la uchaguzi tajwa.

Aidha, Nilitoa rai Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Samuel Sitta kutoa kwa umma na kwa vyama vya siasa muswada wa sheria ya uchaguzi wa Afrika Mashariki wa mwaka 2011 uliopitishwa na Bunge la Afrika Mashariki na kumshauri Rais Jakaya Kikwete kusaini sheria husika ili iwe msingi wa marekebisho yanayopaswa kufanyika kabla ya uchaguzi husika kufanyika nchini.

Nilichukua hatua hizo ili mihimili miwili ya nchi yaani bunge na serikali kutoa uongozi thabiti wenye kuwezesha Tanzania kupata wabunge wanaokubalika na umma wa Bunge la Afrika Mashariki katika uchaguzi.

Hata hivyo, hatua husika hazikuchukuliwa kwa wakati mpaka mwezi Machi ambapo tangazo la uchaguzi lilitolewa na majibu ya barua ya mwezi Februari kupewa mwezi Machi kuwa naweza kuwasilisha mapendekezo ya marekebisho ya kanuni husika.

Kutokana na majibu hayo, pamoja na kuwa tangazo la uchaguzi limeshatolewa na baadhi ya vyama vimeanza kutoa mapendekezo ya wagombea kwenye vyama vyao naamini bado Spika na Katibu wa Bunge watawezesha marekebisho husika kufanywa na bunge kabla ya siku ya uchaguzi ambayo ni tarehe 17 Aprili 2012.

Marekebisho hayo yatawezekana kufanyika iwapo Katibu wa Bunge ataamua kusogeza mbele tarehe ya uteuzi wa wagombea ambayo imetangazwa kuwa ni tarehe 10 Aprili 2012 na pia iwapo Kamati ya Kanuni itakutana mapema iwezakanavyo kabla ya mkutano saba wa bunge na kutumia mamlaka ya kibunge kwa mujibu wa vipengele 3(3)(a) na (b) vya Nyongeza ya Nane chini ya Kanuni ya 115 ya Kanuni za Kudumu za Bunge toleo la 2007 kuanza mchakato wa kufanya marekebisho ya msingi katika kanuni za uchaguzi.


John Mnyika (Mb)

31/03/2012

No comments: