Sunday, August 12, 2012

Kauli ya awali kufuatia madai ya kizushi na kijinga ya CCM kuwa CHADEMA imepewa mabilioni na nchi za nje

Katika mitandao ya kijamii kumesambazwa habari zikimnukuu msemaji wa CCM kutoa madai mbalimbali ya uzushi katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu CHADEMA baada ya CHADEMA kuendelea kutekeleza mikakati na mipango yake ya kuwaunganisha watanzania kupitia falsafa ya ‘nguvu ya umma’ katika kuchangia vuguvugu la mabadiliko (M4C) katika maeneo mbalimbali nchini. Nitatoa tamko kamili na kueleza hatua za ziada baada ya kupata taarifa iliyotolewa kwa ukamilifu, hata hivyo kuhusu madai yaliyokwisha sambazwa kwenye mitandao ya kijamii na CCM nachukua fursa hii kutoa kauli ya awali kama ifuatavyo:


Kuibuka huku kwa CCM na kufanya propaganda chafu ni ishara ya kwamba CCM inaumizwa na namna ambavyo watanzania wanajitokeza kuunga mkono CHADEMA kwa hali na mali hivyo CCM sasa inatapatapa kujaribu kudhibiti wimbi la mabadiliko kwa kutumia siasa chafu. Mwenyekiti wa CCM Rais Jakaya Kikwete anapaswa kueleza watanzania iwapo mikakati hiyo michafu ina baraka zake na za serikali anayoiongoza kwa kurejea pia madai yaliyotolewa na Waziri wa Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu) Steven Wassira kuwa CHADEMA itasambaratishwa katika kipindi cha mwaka mmoja kwa mbinu mbalimbali.

CCM kwa kuwa imekuwa na kawaida ya kufanya usanii kuhalalisha fedha haramu kama ilivyofanya kwenye chaguzi zilizopita baada ya viongozi waandamizi wa CCM na makada wake kuchota fedha za chafu kifisadi kama zile za kutoka kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) na vyanzo vingine vichafu na kuzisafisha kupitia harambee za hadaa zilizofanywa na CCM kwa nyakati mbalimbali; inataka kuichafua CHADEMA inayopata fedha kutoka vyanzo halali kwa njia za wazi ili kukatisha tamaa umma wa watanzania unaochangia vuguvugu la mabadiliko.

Viongozi wa CCM wameamua kujidanganya, kuidanganya Serikali yao na kujaribu kuwapotosha watanzania lakini CHADEMA inatambua kwamba watu wachache wanaweza kudanganyika kwa muda mchache lakini si watu wote wakati wote; na kwamba watanzania wa leo kwa uwingi wao hawawezi kudanganyika na uzushi wa kijinga wa CCM.

Ni ukweli ulio wazi kwamba CHADEMA imekuwa ikifanya harambee kwa uwazi kwa nyakati mbalimbali katika kumbi na katika mikutano ya hadhara ikiwemo ya vijijini ambapo michango hutolewa kwa uwazi, aidha michango kwa njia ya simu inaweza kufuatiliwa na kuthibitisha bila shaka yoyote kwamba watanzania wameamua kuchangia mabadiliko ya kweli.

Madai ya CCM kuwa CHADEMA imepokea au itapokea mabilioni ya shilingi kutoka mataifa ya nje ni ya uzushi na narudia kwa mara nyingine tena kuitaka CCM itaje majina ya serikali, taasisi ama makampuni ya nje ambayo CCM inadai kwamba CHADEMA imepokea mabilioni ya shilingi katika siku za karibuni au inatarajia kupokea.

Badala ya CCM kuisingizia CHADEMA ilipaswa CCM ieleze watanzania orodha ya vigogo wa Serikali inayoongozwa na wanachama waandamizi wa CCM ambao wanaelezwa kuwa na akaunti nchini Uswisi na nchi zingine wakituhumiwa kupewa fedha za kifisadi kutoka kwa makampuni ya utafutaji wa mafuta, gesi asili pamoja na uchimbaji wa madini.

CCM ilipaswa ieleze watanzania sababu za kuendelea kusuasua kujivua magamba ya ufisadi kinyume na maazimio ya CCM yaliyofikiwa baada ya msukumo wa CHADEMA kutaja orodha ya mafisadi kwa kuwa kati ya mafisadi hao ni pamoja na viongozi wa CCM walioiingiza nchi katika mikataba mibovu.

Ikumbukwe kwamba madai haya si mapya kutolewa na CCM, yaliwahi kutolewa na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Sophia Simba mara baada ya uchaguzi mkuu wa 2010 akidai kuwa CHADEMA imepokea fedha kutoka mataifa ya ulaya kwa ajili ya kufanya maandamano ya kuiondoa CCM madarakani.

Itakumbukwa kwamba wakati huo nilimtaka ataje nchi hizo na kueleza kusudio la kumchukulia hatua zaidi na kwa upande mwingine niliyataka mataifa hayo ya Ulaya yatoe kauli kuhusu madai hayo. Izingatiwe kwamba mataifa hayo yalikanusha madai hayo ya CCM na Sophia Simba mwenyewe alikana kuwa hakuna madai hayo dhidi ya CHADEMA.

Nimeelezwa kuwa CCM imetoa madai mengine ya uzushi kuwa CHADEMA inapewa mabilioni toka nje kwa kuwa nchi imegundua rasilimali za mafuta na gesi na kudai kuwa fedha hizo ni kwa ajili ya kuiweka nchi rehani.

Madai haya yaliwahi kutolewa pia na Katibu wa CCM wa Fedha na Uchumi Mwigulu Nchemba na nikamtaka Waziri wa Mambo ya Nje Benard Membe kutaja nchi hizo na mikataba hiyo hata hivyo mpaka sasa hakuna kiongozi yoyote wa CCM na Serikali aliyejitokeza kutaja CHADEMA imepokea au itapokea mabilioni kutoka nchi gani na kwa mikataba gani.

CCM inatoa madai hayo kuhamisha mjadala baada ya CHADEMA wa uongozi bora, sera makini, mikakati sahihi na oganizesheni thabiti kuwa mstari wa mbele katika kutetea rasilimali za taifa na watanzania kutambua kwamba taifa letu litaepushwa kutumbukia kwenye laana ya rasilimali kwa kuiondoa CCM madarakani katika chaguzi za mwaka 2014 na 2015 na kuichagua CHADEMA.

CCM na Serikali yake ndiyo imekuwa kinara wa kupokea fedha kutoka nje kwa kisingizio cha misaada na kuingia mikataba mibovu na mataifa ya nje pamoja na makampuni ya kigeni na kuachia mianya ya uporaji wa rasilimali za nchi na CHADEMA imeanika hali hii kwenye orodha ya mafisadi kwa kutaja majina ya viongozi waliohusika kwenye mikataba ya madini na tutaendelea kufanya hivyo hata katika masuala ya mafuta na gesi ambayo tayari vigogo wa Serikali inayoongozwa na CCM wameshaanza kuingia mikataba mibovu na kuingiziwa fedha katika akaunti zao za nje ya nchi.

Hivyo, badala ya CCM kutoa madai ya uzushi kuhusu CHADEMA kuingia mikataba na serikali au makampuni ya nje, CCM ieleze watanzania imechukua hatua gani mpaka sasa juu ya viongozi na wanachama wake waliongia mikataba mibovu kwenye rasilimali muhimu nchini ikiwemo madini, mafuta, gesi na maliasili zingine za taifa letu na kutoa mikataba hiyo hadharani ili watanzania waweze kuchukua hatua za kufanya mabadiliko ya kweli.

Hivi karibuni Rais Kikwete ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM alisema kwamba serikali inayoongozwa na CCM haitarudia makosa ya kuachia mianya ya ufisadi kwenye gesi; hivyo CCM ilipaswa wakati huu kuwaomba radhi watanzania kwa ufisadi uliofanyika kwenye madini na rasilimali nyingine na kuishukuru CHADEMA kwa kuendelea kuwaunganisha watanzania wakati wote kusimamia mabadiliko ya kweli.

CCM badala ya kutishia kuwa ina mikataba inayoihusu CHADEMA ingetoa mikataba hiyo na hali hii ya CCM inayoongoza Serikali kudai CHADEMA kufanya mikakati, mipango na shughuli iliyo kinyume cha sheria bila vyombo vya dola kuchukua hatua ni ishara ya CCM kukiri wazi kuwa chama legelege chenye serikali legelege kimeshindwa kuongoza nchi na badala yake kimejikita katika propaganda chafu.

CHADEMA tangu kuanzishwa kwake imekuwa na makubaliano ya ushirikiano (MOU) bila masharti yoyote na vyama rafiki vya ndani ya Afrika na duniani na makubaliano hayo yamekuwa yakifikiwa kwa uwazi ikiwa ni sehemu ya CHADEMA kuwa na mtandao wa kimataifa na hayajawahi kuhusisha wala hayatawahi kuhusisha CHADEMA kusaidiwa mabilioni ya shilingi kwa ajili ya kufanya kazi zake kama inavyodaiwa na CCM.

CHADEMA kimekuwa chama kiongozi kwa nyakati mbalimbali kueleza viwango cha matumizi yake ya fedha na vyanzo vya fedha husika huku kikitegemea kwa kiwango kikubwa michango ya wanachama na wapenzi wa chama hapa nchini pamoja na kutumia kwa ufanisi ruzuku inayotolewa kwa vyama vya siasa.

CCM imekuwa na kawaida ya kutoa madai ya uzushi wakati mwingine yakiambatana na kutoa nyaraka za kughushi inazodai kuwa ni za CHADEMA. Ikumbukwe kwamba wakati wa uchaguzi wa mdogo wa Igunga, CCM ilitoa madai ya uzushi kuwa CHADEMA inafadhiliwa na nchi za nje ikiwemo kupewa mafunzo ya ugaidi na kudai kuwa tayari magaidi wameingizwa na CHADEMA toka nje katika uchaguzi huo; hata hivyo katika mwenendo wa kesi ya uchaguzi ya Igunga Katibu Mkuu wa CCM Wilson Mukama aliyetoa madai hayo alitoa ushahidi mahakamani kwamba CHADEMA haijawahi kuleta magaidi bali kauli hizo za CCM zilikuwa ni za siasa za uchaguzi.

Hivi karibuni, CCM imeghushi waraka mwingine na kuusambaza kile ilichodai kuwa ni maazimio ya kamati kuu ya CHADEMA ya kupanga migomo ya walimu, madaktari na mipango mingine ya kuhujumu serikali; hata hivyo waraka huo ulidhihirika wazi kuwa ni wa kughushi.

Mikakati yote hiyo michafu hupangwa na CCM mara kwa mara wakati ambapo CHADEMA inaanza operesheni Sangara na mikakati mingine ya kuleta mabadiliko nchini na kujipanga kuiondoa CCM madarakani kama ilivyo sasa ambapo CHADEMA inaendelea na operesheni katika mkoa wa Morogoro hivyo watanzania wanapaswa kuipuuza CCM na kuendelea kujiunga CHADEMA na kuchangia mabadiliko kwa hali na mali mpaka kieleweke.

John Mnyika (Mb)

Mkurugenzi wa Habari na Uenezi

12/08/2012- Dodoma

12 comments:

Unknown said...
This comment has been removed by the author.
Anonymous said...

Hawa wajinga wana bahati, tungekuwa na hela kweli wangelia

Anonymous said...

Ingekuwa ni halali kuuwa 2ngewachicha.they ars all dickhead

http://kadulyu.wordpress.com said...

Mh. Inaskitisha madai ya namna hii kutoka kwa cma makini kama CCM. Nilisema wakati fulani kwamba inabidi jamii yetu kwa ujumla tuukubali mfumo wa vyama vingi kwa dhati. Na kwamba kutakuwa na mawazo mbadala kila wakati, na si dhambi kutoutiana kisiasa.

Kama CDM inachangiwa fedha na nchi za kigeni kinyume cha sheria watoe ushahidi ili nasi wananchi tufahamu. La sivyo tutajua hizi ni siasa za maji taka na ni aibu kufanywa na chama makini kama CCM? Nnauye anatakiwa afahamu kuwa mtamko yasiyo na mshiko yanakiweka chama chake mahali pabaya zaidi. Hata wale tusio na chama tunaona mambo yanyotamkwa na chama hiki kikongwe ni ya ajabu ajabu!

Anonymous said...

Nimemsikiliza vuvuzela nape na nikaona hana point, Kwani yeye anataka kusema kuwa chama chake kinatetea rasilimali za watanzania kweli wakati magamba(ccm) ndo mafisadi papa. Nitaendelea kuchangia M4C mwanzo mwisho.

Anonymous said...

Nape anataka kuwapotezea muda CDM, achaneni naye kwani hana jipya na akisemacho naona nikuweweseka kwani kwa ujumla CDM mko makini na hakika mbele ya chama cha Nape CDM ni tishio! Kwahiyo Nape lazima aweweseke.

Kama ni nchi hii kuibiwa na watu wa nchi za nje basi imeibiwa sana chini ya ccm, Nape amefanya nini? Kama nchi iko katika hali mbaya, basi ni sasa ambapo ccm inatawala! Nape amefanya nini? Asitubabaishe kwani hayo yote tunayaona na tunajua kabisa kuwa sasa tunaihitaji ukombozi kwani tumenyonywa kiasi cha kutosha, tumeonewa kiasi cha kutosha, na tumedharauliwa sana kiasi cha kutosha. Hayo yote yamekuwa yakifanyika kwasababu ya ukiritimba aw chama kimoja, nacho ni ccm!

Nawapongeza CDM kwa yote mnayoyafanya kuipigania nchi isije kila za ikaisha.

Anonymous said...

Inanisikitisha sana kuona kijana kama Nape anakaa chini na kutunga uongo, halafu bila aibu anautoa hadharani. Nyinyi magamba hamna hata hofu ya Mungu aonaye sirini?

Anonymous said...

Nape amekurupuka na wataleta maneno mengi upande wetu.Mh.hapa hakati tamaa mtu nadhani tuboleshe zaidi M4C.kingine Mh.tusaidie sisi wafanyakazi Tanesco hatulipwi overtime zetu sasa ni mwaka wa pili,hawa ccm wanatuumiza sana

Anonymous said...

Nape ni reflection ya serikali ya CCM. Upeo wao ni mdogo na hawajuwi maana halisi ya kushika dola. CHADEMA inawezaje kuingia mikataba ya mafuta na gesi wakati dola ipo na isichukuwe atua! Nape anapaswa kujuwa upeo wa watanzania ni mkubwa kuliko anavyofikiria yeye, kutoa uongo wa kijinga nikujiumbua yeye na CCM yake. CCM endeleeni kuvimbi.sha vitambi bila kutumia ubongo mutaumbuka

Anonymous said...

Nilishuhudia Nape akitoa shutuma dhidi ya CHADEMA kuhusu kupokea mabilioni ya fedha kutoka nje ya nchi kupitia station moja ya tv, watu wote niliokuwa nao waliguna na kucheka wakisema ama kweli CCM wameishiwa. So please Mnyika do not waste time to respond to allegations which do not exist. Kaza kamba maji yamewafika shingoni wanatapatapa hao.

Anonymous said...

Mh. Mnyika, J.J., uliahidi kuleta kauli yako ya pili kufuatia madai ya kizushi na kijinga ya CCM kuwa CHADEMA imepewa mabilioni na nchi za nje. Nina kiu ya kukusikia zaidi katika hiyo kauli yako ya pili maana hawa watu sasa wanataka kutuchezea! Naamini kauli yako ya pili bila shaka itakuwa ni ya kuzidi kuwashindilia na ili wakome tabia yao ya kutudharau kama wanavyofanya kule bungeni.

Nakumbushia tu Mh.

Anonymous said...

OUT OF TOPIC

MNYIKA HIVI UMESIKIA BARRICK GOLD INAUZA MAKAMPUNI YAKE YOOTE MANNE YA DHAHABU KWA WACHINA ? NAMAANISHA BULYANHULU, NORTHMARA, BUZWAGI NA TULAWAKA , JE HAPO KAMA SERIKALI MNASEMAJE? KAMA MNAVYOWAJUA WACHINA WALIVYO HADI WAFAGIAJI WATAKUWA WACHINA , VIPI SWALA LA AJIRA HAPA KWETU ? KUMBUKA NI MAMIA YA WATANZANIA WANAYAFANYIA KAZI MAKAMPUNI HAYA HEBU FUATILIA