Wednesday, March 26, 2014

Mnyika: Dawasco toeni taarifa mtambo wa Ruvu

26/03/2014 | Posted by Shehe Semtawa

MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika, ameitaka Kampuni ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasco), kutoa taarifa kwa umma kuhusu kuchelewa kukamilika matengenezo ya mtambo wa Ruvu Juu, kunakosababisha upungufu wa maji katika maeneo ya jiji hilo.

Akizungumza kwa njia ya simu na Tanzania Daima Jumatano jana, Mnyika alisema baada ya kutokea tatizo hilo aliwasiliana na Dawasco ili kujua hatua walizochukua.

Alisema maelezo waliyompatia ni kuanza kwa matengenezo, hivyo hatua ya kuchelewa kukamilika kwa matengenezo hayo ilipaswa Dawasco kutoa taarifa kupitia vyombo vya habari, matangazo ikiwemo tovuti yake.

“Natambua kwamba yapo matengenezo madogo yamefanyika, hivyo baadhi ya maeneo kuanza kupata maji lakini pungufu ya kiwango cha mgawo uliokuwa ukitolewa kabla,” alisema.

Mnyika alibainisha kuwa kuharibika kwa pampu hiyo kumesababisha ongezeko la uhaba wa maji kwa muda wa wiki tatu katika maeneo ambayo yalikuwa yanapata maji kutokana na utaratibu wa mgawo wa kawaida.

Aliyataja maeneo yalioathirika kutokana na tatizo hilo ni Kibamba, Kwembe, Mbezi, Saranga, Kimara, Ubungo, Makuburi na maeneo mengine.

Chanzo: http://www.freemedia.co.tz/daima/mnyika-dawasco-toeni-taarifa-mtambo-wa-ruvu/

No comments: