Monday, March 24, 2014

Kuhusu Kituo Kipya cha Daladala Ubungo, Uendelezaji wa Kiwanja na. 2005/2/2 Sinza (Former Simu 2000) na fursa kwa Wafanyabiashara Ndogo Ndogo

Leo 25 Machi 2014 Ofisi ya Mbunge wa Jimbo Ubungo itafanya kazi ya kufuatilia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Manispaa ya Kinondoni na Kamati ya Wafanyabiashara ndogo ndogo kuhusu utekelezaji wa mapendekezo niliyotoa tulipofanya ziara ya kikazi katika Stendi mpya ya Daladala ya Ubungo tarehe 6 Januari 2014.

Aidha, Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Ubungo itatumia nafasi hiyo kufuatilia kwa mamlaka mbalimbali juu ya masuala ambayo mbunge aliyahoji jimboni na bungeni kuhusu wafanyabiashara ndogo ndogo na wazalishaji wadogo ambayo yako katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Ikumbukwe kwamba tarehe 6 Januari 2014 nilipofanya ziara ya kikazi ya kufuatilia ujenzi wa Kituo kipya cha daladala katika Kiwanja na. 2005/2/2 Kitalu C Sinza eneo ambalo zamani lilikuwa chini ya “Simu 2000” uendelezaji ulikuwa umefanyika katika ekari nne.

Katika ziara hiyo niliambatana na watendaji mbalimbali wa Serikali na mamlaka zingine ambapo niliwaeleza haja ya kuharakisha kutenga eneo la wafanyabiashara ndogo ndogo na wazalishaji wadogo katika ekari nane ambazo mpaka wakati huo zilikuwa hazijaanza kuendelezwa ili kuongeza fursa za ajira hususani kwa vijana na wanawake.

Msingi wa mapendekezo hayo ni hatua ambazo nilishaanza kuzichukua kwa nyakati mbalimbali mwaka 2011, 2012 na 2013 katika kuwawakilisha na kuisimamia Serikali (Rejea: http://mnyika.blogspot.com/2012/04/mkutano-wangu-na-wamachinga-wa-ubungo.html au http://mnyika.blogspot.com/2013/03/mnyika-ataka-kauli-ya-rais-kikwete.html )

Pia, kwa kuzingatia kwamba mpaka sasa bilioni 1 na milioni 82 zimechatolewa kumlipa mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi, choo na eneo la daladala; nilitaka kazi iharakishwe pia ya kujenga miundombinu mingine muhimu.

Naamini mpo wadau mnaotumia kituo cha sasa cha Daladala cha Ubungo (Eneo la Mataa) kinachotarajiwa kuvunjwa na mpo watumiaji watarajiwa wa Kituo Kipya kitakachokuwa katika kata ya Sinza.

Kwa kuwa leo nitakuwa pia kwenye kazi nyingine ya kuwawakilisha wananchi kwenye Bunge Maalum la Katiba hapa Dodoma, natoa taarifa hii kwenu ili wadau wa masuala hayo muweze kumpa ushirikiano Katibu Msaidizi 0784379542/0715379542 ambaye atafanya ufuatiliaji Dar Es Salaam kwa niaba ya Ofisi ya Mbunge Jimbo la Ubungo.

AMUA: Maslahi ya Umma Kwanza, 
John Mnyika (Mb)

No comments: