Thursday, March 6, 2014

Taarifa kwa Umma: “Kuendelea kwa ‘Kashfa ya IPTL’ mpaka hivi sasa ni matokeo ya udhaifu wa Rais Kikwete, uzembe wa uongozi wa Bunge, ufisadi wa baadhi ya viongozi wa CCM na uongo wa Waziri Muhongo”.

Kwa nyakati mbalimbali kati ya tarehe 27 Februari 2014 na tarehe 5 Machi 2014 vyombo mbalimbali vya habari vimeandika habari na kuchapisha matangazo juu ya TANESCO na IPTL.

Umma uzingatie kwamba ‘kashfa ya IPTL’ ni ya miaka mingi katika taifa letu na inaendelea mpaka hivi sasa kutokana na udhaifu, uzembe, ufisadi na uongo unaotawala. 

Kumbukumbu zangu zinanionyesha kwamba wakati wa kuanzishwa kwake IPTL ilikuwa ni ubia wa kampuni mbili; Mechmar Corporation ya Malysia Bhd na VIPEM ya Tanzania. 

Udhaifu wa Rais unaendeleza ‘kashfa ya IPTL’:

Mwaka 1994 IPTL ilikutana na aliyekuwa Waziri wa Maji, Nishati na Madini wakati huo Jakaya Kikwete na aliyekuwa Mkurugenzi wa TANESCO wakati huo Simon Mhaville. 

Mara baada ya mazungumzo hayo IPTL ilianza kupigiwa chapuo kuingia mikataba na TANESCO pamoja na kudaiwa kutokuwa na uwezo. 

Mara baada ya kuchaguliwa Urais mwaka 2005 Rais Kikwete aliahidi kuupatia ufumbuzi mgogoro kati ya TANESCO na IPTL na washirika wake uliokuwa umegubikwa pia na madai ya ufisadi mkubwa. 

Huu ni mwaka 2014 ‘kashfa ya IPTL’ inaendelea hivyo Rais Kikwete anapaswa kulieleza taifa sababu za kuendelea kwa hali hiyo na hatua ambazo unakusudia kuchukua kuondoa udhaifu huo.

Uzembe wa uongozi wa Bunge unakwaza uwajibikaji ‘kashfa ya IPTL’

Mwaka 2008 kufuatia ‘kashfa ya Richmond’ Bunge liliazimia katika Azimio Na. 3, kwamba “Mkataba kati ya TANESCO na Richmond Development Company LLC (uliorithiwa na Dowans Holdings S.A.) na ile kati ya TANESCO na IPTL, SONGAS, AGGREKO na Alstom Power Rentals, ipitiwe upya mapema iwezekanavyo kama ambavyo Mikataba ya Madini ilivyopitiwa upya na Serikali”. 

Uongozi wa Bunge la tisa wa Spika Samuel Sitta ulizembea na kufunga mjadala kuhusu ‘kashfa ya Richmond’ huku maazimio ya msingi yakiwa hajatekelezwa. Uongozi wa Bunge la kumi wa Spika Anna Makinda ukaendeleza uzembe huo hata tulipohoji Bungeni kwa nyakati mbalimbali 2011, 2012 na 2013 kutaka Serikali itakiwe kuwasilisha bungeni taarifa za utekelezaji wa maazimio ya Bunge kuhusu kashfa za Richmond, IPTL na nyingine nyingi katika sekta ya nishati.

Iwapo Azimio hili lingetekelezwa kwa ukamilifu wake, gharama za uzalishaji TANESCO na serikali kwa ujumla zinazotokana na matatizo katika mikataba zingepungua na hivyo kupunguza kuwaongezea mizigo ya bei ya umeme mara kwa mara watanzania. Hivyo, kauli za hatua ambazo wanakusudia kuchukua kuondoa uzembe huo za Waheshimiwa Sitta (katika Baraza la Mawaziri) na Makinda (Katika Uongozi wa Bunge) zinahitajika kuepusha madhara zaidi kwa nchi na wananchi.

Uongo wa Waziri Muhongo umechelewesha hatua bungeni

Katika Hotuba niliyotoa Bungeni tarehe 22 Mei 2013 kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa Nishati na Madini nilieleza kwa kirefu kuhusu kashfa hizo na hatimaye nikaeleza kwa niaba ya wenzangu kwamba “Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali ieleze kwanini mpaka sasa haijatekeleza maazimio hayo na bunge liweke muda wa ukomo wa kutekeleza Maazimio yote ya Bunge yaliyokuwa yamesalia katika sakata hili la Richmond ili mara moja na daima sakata hili la Richmond limalizwe na kufungwa baada ya maazimio yote kutekelezwa kwa ukamilifu. Ikiwa maazimio ya mwaka 2008 utekelezaji wake haujakamilika mpaka mwaka 2013 kwa miaka mitano, nini kitalihakikishia taifa kwamba maazimio mengine mapya yaliyopitishwa 2011 na 2012 yatatekelezwa kwa wakati na kwa ukamilifu?”

Aidha, nikaendelea mbele kueleza kwamba “matumizi mabaya ya rasilimali za umma hayako katika mikataba ya kukodi mitambo ya umeme tu, bali katika ununuzi wa huduma za kisheria. Hivyo, narudia kutoa mwito kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali aeleze ni kiasi cha fedha kilichotumika kwenye kuendesha kesi za Dowans na IPTL mpaka sasa na hatua zilizochukuliwa dhidi ya mawakili wa TANESCO na makampuni binafsi yanayotuhumiwa kusababisha mzigo mkubwa wa gharama za kesi ambazo serikali inashindwa kwa nyakati mbalimbali”.

Katika Hotuba hiyo bungeni nilikumbusha pia kwamba, “mwaka 2011 Benki ya Standard Hong-Kong ambayo ni mdeni mkuu katika sakata la IPTL ilifungua kesi ya madai katika mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi (ICSID case Na. ARB/10/20) inayodai kiasi cha dola za Kimarekani milioni 225, pamoja na riba katika kuendesha kesi hiyo. Kampuni ya uwakili ya Mkono (inayomilikiwa na Nimrod Mkono Mbunge wa CCM) ilipewa zabuni ya kuitetea Serikali katika shauri hilo, na kwa kujiamini iliishauri Serikali kuwa kesi hiyo tutashinda pamoja na wanasheria wengine kuwa na maoni kinzani kuhusu suala hilo. Kampuni ya Mkono imekuwa ikiishauri Serikali isifanye usuluhishi nje ya mahakama ya ICSID wakati wadai kupitia kwa Mfilisi wa Mali na Madeni za IPTL (RITA) wanakubali kusuluhishwa nje ya mahakama. Je, mpaka lini Serikali itaendelea kuingia gharama hizo na ni kiasi gani Serikali imelipa kwa kampuni hiyo na zingine mpaka hivi sasa?”. 

Tarehe 25 Mei 2013 badala ya Waziri Muhongo kutoa majibu ya ukweli hatua ziweze kuchukuliwa mapema kulinusuru taifa na mzigo wa madai akatoa majibu ya uongo kwamba “sasa hivi tunaongelea uchumi na maendeleo na ndiyo maana ukinitajia hapa mlolongo wa kesi ukategemea nikapukue mafaili Wizarani, nadhani kuwa kwanza ni mbunge wa kuteuliwa na nikapewa uwaziri nadhani hawakunituma pale kupekua mafaili”.

Matokeo ya uongo huo ni Bunge kucheleweshwa kuingilia kati kabla ya hukumu iliyotolewa tarehe 12 Februari 2014 ya kesi iliyofunguliwa na Benki ya Standard Chartered (SCB) Hong Kong dhidi ya TANESCO kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Utatuzi wa Migogoro ya Kibiashara (ICSID) iliyopo nchini Uingereza.

Kwa kuzingatia kuwa hukumu hiyo imetoa miezi mitatu kwa pande mbili kukubaliana nje ya mahakama hadi Mei 2014; Waziri Muhongo anapaswa kujitokeza mbele ya umma kufuta kauli yake ya uongo aliyoitoa bungeni. 

Waziri Muhongo atumie fursa hiyo kueleza pia hatua ambazo yeye na wenzake katika Serikali wanakusudia kuchukua kuhakikisha kwamba mazungumzo yanayoendelea kwa siri hivi sasa kuhusu taratibu za kukokotoa gharama halisi hayabebeshi mzigo kwa nchi na wananchi. 

Waziri Muhongo akiendelea kusema uongo kuhusu ‘kashfa ya IPTL’ na zingine nitawataja kwa majina vigogo wa Serikali na CCM walionyuma ya kashfa hizo ili waweze kuhojiwa kwa umma. 

Nitachukua hatua hiyo kwa kuzingatia kwamba madaraka na mamlaka ni ya wananchi, Serikali inafanya kazi kwa niaba ya wananchi; hivyo pale ambapo Serikali inachelewa kuchukua hatua kutokana na udhaifu, uzembe, ufisadi au uongo ni muhimu wananchi wakashiriki kutaka uwajibikaji.

John Mnyika (Mb)
05/03/2014

1 comment:

Anonymous said...

Je unajua Jimboni kwako hakuna maji kwa muda wa wiki ya pili sasa? Je unadhani hik ni muimu kwa wapiga kra wako zaidi ya kutatua tatizo la maji. Maji ni tatizo katika jimbo hili.