Tuesday, July 21, 2009

‘Ruksa’ kwa watumishi wa umma kushiriki siasa-1



‘Ruksa’ kwa watumishi wa umma kushiriki siasa-1


Na John Mnyika

Kati ya maswali na masuala ambayo watumishi wengi wa umma wamekuwa wakijiuliza ama kuyatakakari baada ya kuanza kwa mfumo wa vyama vingi ni haki, wajibu na mipaka yao katika kujihusisha na siasa zikiwemo za vyama. Aidha majibu mepesi ya maswali hayo yamekuwa ni hisia finyu kuwa watumishi wote wa umma hawapaswi kujihusisha na vyama vya siasa. Ama kwa kwa upande mwingine yamekuwepo pia mawazo potofu kwamba watumishi wa umma wanapaswa kujihusisha na chama kinachotawala pekee na hawapaswi kabisa kujihusisha na vyama vya upinzani. Makala hii itachambua suala hili mintaarafu Waraka wa Mkuu wa Utumishi wa Umma kuhusu maadili ya watumishi wa umma katika mfumo wa vyama vingi kwa kurejea pia sheria na kanuni zinazohusika.

Utumishi wa umma katika nchi yetu unaongozwa na Sheria ya Utumishi Serikalini namba 16 ya mwaka 1989 na Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma Toleo la 1994 pamoja na marekebisho yake. Kwa madhumuni ya makala hii Neno Mtumishi wa Umma lina maana kama iliyoanishwa katika Kanuni za kudumu za utumishi kifungu Na. A.1(66) ambacho kinatafsiri mtumishi wa umma kama mtu yoyote anayeshikilia ofisi ya umma ambayo imepewa mamlaka ama inatekeleza wajibu wenye asili ya umma, iwe chini ya utawala wa moja kwa moja wa Rais au la. Na inajumuisha maofisa walio chini ya Serikali za Mitaa ama Mashirika ya umma; lakini haijumuishi wanaoshikilia nafasi hizo kwa sehemu ya muda wa ziada(Part Time basis).

Kwa mantiki hiyo, tafsiri hii inafanya wafanyakazi wote wa serikali na taasisi zake kuwa ni watumishi wa umma. Hii inajumuisha Rais, Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa halmashauri na Mashirika ya umma, watendaji wa kata nk. Orodha hii inahusisha pia waajiriwa wa kawaida wa serikali mathalani walimu wa shule za umma, watumishi wa sekta ya afya wa serikali, maofisa wote waajiriwa wa halmashauri/serikali za mitaa nk. Watumishi wa umma ni pamoja pia watumishi wa mihimili mingine ya serikali kama mahakama kwa maana ya majaji na mahakimu na Bunge kwa maana ya wabunge na watumishi wa bunge. Watumishi wa umma ni pamoja na wafanyakazi wa vyombo vya ulinzi na usalama wakiwemo askari wa majeshi mbalimbali. Ukiitafakari orodha hii ndefu utaona kwamba jambo hili linahusu watu wengi; hivyo suala la ushiriki wao katika siasa katika mfumo wa vyama vingi linapaswa kutafakariwa na kujadiliwa na umma.

Uzoefu katika nchi mbalimbali duniani unaonyesha kuwa ziko njia mbalimbali za watumishi wa umma kuweza kujihusisha na vyama vya siasa. Njia iliyozoeleka zaidi ni ile ya kushiriki katika kupiga kura ama kuweza kushiriki katika kupigiwa kura kwa maana ya kugombea. Kushiriki katika kupiga kura kunaweza kuwa ni katika kupiga kura za kuchagua viongozi wa umma wa kiserikali ama kupiga kura katika kuchagua viongozi wa ndani ya chama. Kwa upande wa kugombea nayo inaweza ikawa katika chaguzi za kiserikali ama kugombea katika nafasi za uongozi za ndani ya chama cha siasa. Katika hali hiyo, njia nyingine ya watumishi wa umma kujihusisha na vyama vya siasa ni kwa kuwa wanachama wa vyama hivyo. Aidha katika nchi ambazo demokrasia imeendelea, ushiriki wa watumishi wa umma katika vyama vya siasa na siasa kwa ujumla unahusisha ushiriki wao katika kupiga kura kuhusu masuala mbalimbali(issue voting) mathalani kura za maoni(referendum). Pia, watumishi wa umma wanaweza kujihusisha kwa kutoa maoni na mitazamo yao kuhusu masuala mbalimbali ya kisiasa na yanayohusu vyama vya siasa kwa kutumia njia mbalimbali.

Kuanzia mwaka 1965 hadi 1992 Tanzania ilipokuwa na mfumo wa siasa wa chama kimoja kundi lote hili la watumishi wa serikali na vyombo vyake siyo tu waliruhusiwa bali ilionekana ni wajibu wao kushiriki katika mambo ya kisiasa. Shughuli nyingi za kiserikali na za kisiasa zilikwenda kwa pamoja na palikuwepo na maingiliano makubwa kati ya sehemu hizi mbili katika shughuli zote za kiutendaji, kiuongozi na kiitikadi.

Na kwa kweli suala hili lilianza mara baada ya uhuru kabla hata ya nchi kutangaza kuingia katika mfumo wa chama kimoja. Mathalani, baada ya Maasi ya Jeshi ya mwaka 1964 uamuzi wa Rais wa Kwanza Hayati Mwalimu Nyerere wa kulisuka upya jeshi ambalo lilirithiwa toka kwa mkoloni, kuunda jeshi la wananchi wa Tanzania ulihusisha fungamano la kipekee baina ya Jeshi na Chama tawala. Wakati ule, sehemu kubwa ya wanajeshi ilichaguliwa kutoka vijana wa chama TANU. Hodhi hii iliendelezwa zaidi chini ya mfumo wa chama kushika hatamu ambao ulioweka mahusiano ya karibu baina ya chama kinachotawala na serikali ikiwemo vyombo vyake vya dola. Ni fungamano hili kati ya watumishi wa umma wa kada zote, na chama ndio uliofanya chama kinachotawala kuwa chama dola; suala lenye athari mpaka hivi sasa hususani katika nyakati za uchaguzi.

Mapendekezo ya Tume ya Nyalali ya mwaka 1991 na marekebisho ya Katiba ya mwaka 1992 kuingia katika mfumo wa vyama vingi na marekebisho ya sheria yaliyofuata yameweza kupunguza kwa kiasi hali hiyo. Lakini bado fungamano kati ya chama tawala na serikali ikiwemo vyombo vya dola linahitaji kujadiliwa ili mabadiliko ya kweli yaweze kufanyika. Mabadiliko hayo ya kikatiba, kisheria na kimitazamo yatawezesha kuwa na tunu za kitaifa, misingi kamili ya haki za raia, mifumo ya uwajibakaji wa viongozi na uwanja sawa wa kisiasa. Mabadiliko hayo yatawezesha pia kujenga taasisi za kitaifa, uongozi bora na dira ya pamoja yenye kuunganisha nguvu za umma katika kupambana na ufisadi, kutetea rasilimali na kusimamia fikra mbadala zenye kujenga taifa lenye kutoa fursa kwa wote. Taifa wananchi wanaweza kuneemeka na uwezo ambao wamejaliwa wao na nchi kwa ujumla.

Wakati tunapoanza kutafakari namna ambayo watumishi wa umma wanavyoweza kujihusisha na vyama vya siasa kwa sasa na kuwa wakala wa mabadiliko wanayotaka kuyaona, ni muhimu kama taifa tukakumbuka ushiriki wao katika wakati uliopita na taathira yake katika demokrasia katika wakati huu. Hii itawezesha kuchukua maamuzi thabiti ya kuweka mwelekeo mwafaka wenye kujenga katika mafanikio ya zamani na wakati huo huo kutibu majeraha ya kisiasa, kijamii na kiuchumi yaliyotokana na hodhi ya chama kimoja ambayo sasa taifa linadhamiria kuondokana nao.

Mwandishi wa Makala hii ni Mkurugenzi wa Mambo ya Nje(CHADEMA) anapatikana kupitia 0754694553, mnyika@chadema.net na http://mnyika.blogspot.com





1 comment:

Fredy Mhenzi said...

Hi,mhemiwa! Tunashukuru sana kwa mwanga uliotupa katika mada hii.Tunaomba upige hatua zaidi mbele kutueleza jinsi gani mtumishi wa umma anaweza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kama vile udiwani,ubunge,m/kiti serikali za mtaa n.k.Asante na God bless u. Mhenzi Junior