Tuesday, July 21, 2009

“Ruksa” kwa watumishi wa umma kushiriki siasa-3“Ruksa” kwa watumishi wa umma kushiriki siasa-3

Na John Mnyika


Makala zilizotangulia zimedokeza wakina nani ni watumishi wa umma na ushiriki wao katika siasa katika vipindi vilivyotangulia; wakati wa mfumo wa chama kimoja 1965 mpaka 1992 na kipindi cha awali cha mfumo wa vyama vingi 1992 mpaka 2000. Makala hii inalenga kuanza kufanya mapitio ya kuhusu maadili ya watumishi wa umma katika mfumo wa vyama vingi vya siasa kuanzia mwaka 2000 na tunapoelekea katika chaguzi za mwaka 2009 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Ikumbukwe kuwa utumishi wa umma katika nchi yetu unaongozwa na Sheria ya Utumishi Serikalini namba 16 ya mwaka 1989 na Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma Toleo la 1994 pamoja na marekebisho yake. Kifungu cha 4(1) cha Sheria hiyo kinampa mamlaka Mkuu wa Utumishi wa Umma, ambaye ni Katibu Mkuu kiongozi kutoa waraka kuhusu taratibu mbalimbali za utumishi wa umma.

Chini ya Mamlaka hayo, Katibu Mkuu Kiongozi wakati huo akiwa Martem Y.C. Lumbanga tarehe 26 Juni, 2000 alitoa Waraka wa Mkuu wa Utumishi wa Umma na. 1 wa mwaka 2000 wenye kumb. Na. SHC/C.180/2/113. Waraka huu ulihusu maadili ya Watumishi wa Umma katika mfumo wa vyama vingi vya siasa. Waraka huo ulianza kutumika kuanzia Julai 2000 na ulifuta waraka wa mwaka 1992.

Katika waraka huo serikali imeamua kwamba hakutakuwa na makundi mawili ya watumishi kama ilivyokuwa hapo awali, bali watumishi wote wa umma sasa watatawaliwa na masharti yanayofanana. Katika waraka huo serikali pia imeamua kuanisha utaratibu utakaozingatiwa na watumishi wa umma watakaoamua kugombea ubunge kupitia viti maalumu, pamoja na wale walioteuliwa na Rais kwa mujibu wa katiba kuwa wabunge.

Pia mnamo tarehe 22 Aprili mwaka 2002 Mkuu wa Utumishi alitoa Rekebisho Na. 1 lenye kumb. Na. SHC/C.180/2/152 kwa lengo la kuboresha baadhi ya masharti yaliyotolewa na waraka wa mwaka 2000. Marekebisho hayo yalihusu wagombea udiwani, wagombea ubunge wa viti maalum, ubunge wa kuteuliwa na Rais katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wagombea Ubunge katika Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Hizi ni nyaraka ambazo si za siri za serikali, ni nyaraka za wazi anazopaswa kupatiwa kila mtumishi wa umma mara anapoajiriwa. Hata hivyo, watumishi wengi wa umma, hawafahamu kuhusu nyaraka hizi na hivyo kuwafanya kutotambua haki, wajibu na mipaka waliyonayo kuhusu ushiriki wao katika siasa ikiwemo za vyama.

Katika mazingira hayo ndipo zipozushwa hisia finyu kuwa watumishi wa umma hawaruhusiwi kushiriki kwenye siasa ama mawazo potofu kwamba watumishi wa umma wanajibika kushiriki kwenye siasa kupitia chama kinachotawala pekee. Hii ni changamoto kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais(Utumishi wa Umma), Hawa Ghasia, kuweza kutumia njia zote kuhakikisha waraka huu unafahamika kwa watumishi wa umma na wadau wengine wa siasa wakiwemo wananchi.

Kila mtumishi wa umma ni muhimu akahakikisha anafahamu waraka huu ambao madhumuni yake ni kuweka utaratibu ambao pamoja na masharti yake, unazingatia umuhimu wa kuendelea kuwa watumishi wa umma nafasi ya kutumia haki ya kikatiba ya kushiriki kwenye siasa. Kwa mtizamo wa serikali, waraka huo unalenga pia kuweka mipaka ili kuepuka madhara yanayoweza kuathiri utendaji wa shughuli za umma.

Kabla ya kufanya mapitio kuhusu yanayoruhusiwa na yasiyoruhusiwa kufanywa na watumishi wa umma katika ushiriki kwenye siasa ni vyema tukapitia kwanza misingi ya utumishi wa umma kwa kadiri ya katiba, sheria, kanuni na taratibu mbalimbali. Hii ni misingi ambayo mataifa mbalimbali wanaitumia katika kuongoza maadili ya watumishi wa umma.

Ikumbukwe kwamba watumishi wa umma ni waajiriwa wote kamili wa serikali na taasisi zake. Hii inajumuisha Rais, Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa halmashauri na Mashirika ya umma, watendaji wa kata nk. Orodha hii inahusisha pia waajiriwa wa kawaida wa serikali mathalani walimu wa shule za umma, watumishi wa sekta ya afya wa serikali, maofisa wote waajiriwa wa halmashauri/serikali za mitaa nk. Watumishi wa umma ni pamoja pia watumishi wa mihimili mingine ya serikali kama mahakama kwa maana ya majaji na mahakimu na Bunge kwa maana ya wabunge na watumishi wa bunge. Watumishi wa umma ni pamoja na wafanyakazi wa vyombo vya ulinzi na usalama wakiwemo askari wa majeshi mbalimbali.

Hawa wote wanapaswa kutekeleza wajibu wao kama watumishi wa umma bila kufanya upendeleo wala ubaguzi wa chama chochote cha siasa. Wanapaswa kuwa na utii kwa serikali ya chama kinachotawala kwa kutekeleza kwa dhati na kwa ufanisi sera za serikali. Wanapaswa kutoshiriki katika mambo ya siasa yanayozuia utendaji mzuri katika vyombo vya umma(hii haimaanishi kwamba hawaruhusiwi kujiunga na vyama au kushiriki kwenye siasa). Maadili yanawahitaji kutoa huduma kwa misingi ya haki na kufanya kazi kwa hekima na uadilifu. Pia wanawajibika kutunza siri za serikali, serikali za mitaa na taasisi za mashirika ya umma. Na kwa ujumla wanapaswa kuheshimu maadili ya taaluma. Maadili hayo yamefafanuliwa vizuri katika kijitabu cha Maadili ya Utendaji katika utumishi wa umma, Tanzania kilichotolewa na Idara Kuu ya Utumishi Serikalini, mwaka 1998.

Tunaweza kufanya tathmini na kujaza kurasa nyingi za mifano ya ambavyo maadili hayo yamekuwa yakikiukwa na watumishi wa umma wa ngazi mbalimbali kuanzia ya juu kabisa katika taifa mpaka ngazi ya chini. Kuanzia mwaka 2000 waraka huo ulipotolewa taifa limeshuhudia baadhi ya watumishi wa umma wakishiriki katika kufanya ubaguzi na upendeleo wa chama cha siasa, hususani kinachotawala. Imekuwa ni kawaida kusikia wananchi wakiambiwa na watumishi wa umma kwamba mkichagua upinzani mtanyimwa maendeleo ama watumishi wa umma wakilazimishwa kuunga mkono chama kinachotawala kwa vitisho vya kuondolewa katika utumishi wa umma. Aidha ziara za kiserikali za watumishi wa umma zimekuwa zikiingiza masuala ya kisiasa yenye kubagua na kubomoa vyama vingine. Ukiukwaji huu wa maadili umekuwa ukifumbiwa macho na Mkuu wa Utumishi wa Umma, ambaye ni Katibu Mkuu kiongozi.

Aidha suala la utii na kutekeleza sera za chama kinachotawala limezua mzozo baina ya serikali kuu na serikali za mitaa katika maeneo ambayo vyama vinavoongoza ni tofauti. Mathalani, wakati CCM ni chama tawala katika serikali kuu; katika halmashauri ya Karatu, CHADEMA ni chama kiongozi. Sasa kwa kuwa CCM ni chama cha upinzani katika halmashauri hiyo, watumishi wa umma katika halmashauri wanapaswa kuwa na utii kwa serikali ya chama kinachotawala kwa kutekeleza kwa dhati na kwa ufanisi sera za serikali hiyo ya CHADEMA. Hii ni katika masuala ambayo yako chini ya utekelezaji wa halmashauri chini ya mfumo wa mgawanyo wa madaraka baina ya serikali kuu na serikali za mitaa. Watumishi hao watafuata maelekezo ya serikali kuu katika masuala yanayosimamia kiutekelezaji na serikali kuu pekee.

Pamoja na kuwa maadili yanawahitaji watumishi wa umma kutoa huduma kwa misingi ya haki na kufanya kazi kwa hekima na uadilifu katika kipindi hiki umeshuhudiwa ufisadi mkubwa na/ama matumizi mabaya ya madaraka kuanzia uongozi wa juu kabisa wa taifa mpaka ngazi za chini za utumishi wa umma. Badala ya kuwa na utamaduni wa uwajibikaji pamekuwa na mazoea ya ufisadi kwa kisingizio cha ‘kila mbuzi kula kwa kadiri ya urefu wa kamba yake’. Wakati katika kada za juu za utumishi wa umma, hali hii ikichangiwa na ubinafsi katika kada za chini hali hii imechagiwa na mishahara/maslahi duni ya watumishi wa umma. Asili ya yote haya ikiwa ni mmomonyoko wa maadili kwa ujumla wake katika taifa. Mambo haya yanataathira kubwa katika ushiriki wa watumishi wa umma katika siasa na hivyo kuzalisha mfumo mpya wa ushiriki wa watumishi wa umma kwenye siasa wa ‘nipe nikupe’ au ‘ambao ni hatari kwa mwelekeo wa taifa.

Katika mazingira haya ya uozo wa kimaadili ndipo walipozuka baadhi ya watumishi wa umma wenye uzalendo ambao wameamua ‘kukiuka’ maadili ya kutunza ‘siri’ za serikali na kuanza kuvujisha nyaraka za kiserikali za ‘kifisadi’. Ni wazi, hakuna maadili ya utumishi wa umma yanayomtaka mtumishi wa umma kutunza siri ya serikali hata kama ikiwa ni siri ya wizi; kwani ni kosa la jinai kuficha wizi. Suala hili limezua zogo hivi karibuni bungeni mlengwa mkuu wa kuonyooshewa vidole akiwa ni Mbunge wa Karatu, Dr Wilbroad Slaa kutokana na kuwa mstari wa mbele kuzitumia nyaraka kama hizo katika mapambano ya kupinga ufisadi na kutetea rasilimali za Taifa. Ni vyema watanzania wakakumbuka kuwa ni ushiriki wa namna hiyo wa watumishi wa umma wazalendo ndio uliowezesha Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Kaskazini kuibua kashfa ya Buzwagi, na baadaye ikafuatiwa na Dr Slaa kusoma Orodha ya Mafisadi pale Mwembe Yanga Septemba 15 mwaka 2007. Matukio yaliyofuata baada ya hapo yakiwemo ya kuzomewa kwa watumishi wengine wa umma waliokuwa wakizunguka mikoani kukanusha tuhuma hizo za ufisadi kwa kizingizio cha kutetea uzuri wa bajeti ndio yaliyosukuma kuundwa kwa Kamati ya Bomani kuhusu Madini, Kamati Teule ya Bunge Kuhusu Richmond, Kamati Kazi(Task Force) kuhusu fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje(EPA). Kutokana na hayo taifa limeshuhudia baadhi ya watumishi wa umma wakijiuzulu, na wengine wakipelekwa mahakamani. Hata hivyo, iliweke wazi kwamba safari bado ni ndefu hivyo ushiriki wa watumishi wa umma katika siasa ni jambo linalohitaji mjadala endelevu. Hivyo katika makala ijayo tutafanya mapitio ya mambo ambayo yanaruhusiwa kufanywa kwa uwazi kabisa na watumishi wa umma wanaopenda kushiriki kwenye siasa.

Mwandishi wa Makala hii ni Mkurugenzi wa Mambo ya Nje(CHADEMA) anapatikana kupitia 0754694553, mnyika@chadema.net na http://mnyika.blogspot.com
No comments: