Tuesday, July 21, 2009

“Ruksa” kwa watumishi wa umma kushiriki siasa-2

“Ruksa” kwa watumishi wa umma kushiriki siasa-2


Na John Mnyika

Katika makala iliyopita tulijibu swali nani ni ‘mtumishi wa umma’, tukadokeza uzoefu kutoka mataifa mbalimbali kuhusu namna ambavyo watumishi wa umma wanaweza kushiriki katika siasa. Kadhalika, makala iligusia ushiriki wa watumishi wa umma katika siasa kuanzia mwaka 1965 mpaka 1992 wakati huo nchi ikiwa katika mfumo wa siasa wa chama kimoja. Katika makala hii tutaangalia ushiriki wa watumishi wa umma katika siasa katika kipindi cha awali cha mfumo wa vyama vingi kuanzia mwaka 1992 mpaka mwaka 2000.

Ni muhimu kusisitiza kuwa wakati tunatafakari namna ambayo watumishi wa umma wanavyoweza kujihusisha na vyama vya siasa kwa sasa na kuwa wakala wa mabadiliko wanayotaka kuyaona, ni muhimu kama taifa tukakumbuka ushiriki wao katika wakati uliopita na taathira yake katika demokrasia katika wakati huu. Hii itawezesha kuchukua maamuzi thabiti ya kuweka mwelekeo mwafaka wenye kujenga katika mafanikio ya zamani na wakati huo huo kutibu majeraha ya kisiasa, kijamii na kiuchumi yaliyotokana na hodhi ya chama kimoja ambao sasa taifa linadhamiria kuondokana nao.

Kufuatia mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yaliyofanyika Julai, 1992 na kuruhusu mfumo wa vyama vingi vya siasa kurejea Tanzania, Serikali ilitoa maelekezo ya jinsi watumishi wa umma watavyoshiriki katika mambo ya Siasa kupitia waraka wa Utumishi wa Umma Na. 1 wa mwaka 1992. Waraka huu uliotolewa wakati wa Urais wa Mzee Ali Hassan Mwinyi, maarufu kama “Ruksa”. Na wa kweli waraka huo ulitoa ruksa pana ya ushiriki wa watumishi wa umma katika siasa ukilinganisha na waraka uliofuatia ambao tutaurejea katika makala inayofuata.

Utaratibu uliotolewa na waraka huo uliwagawa watumishi wa umma katika makundi mawili na kuweka masharti ya namna watavyoshiriki katika siasa. Watumishi wa kundi “A” walijumuisha Watumishi wa ngazi za juu wa Serikalini, Serikali za Mitaa na Katika Mashirika ya Umma wanaoshughulikia uandaaji na usimamizi wa sera. Hawa walikuwa ni watumishi waandamizi kwenye madaraka kuanzia ngazi za mkurugenzi na kuendelea juu, Meneja Msaidizi na kuendelea juu na ngazi ya Mkurugenzi Mtendaji. Watumishi wa Kundi “B” walijumuisha watumishi wa ngazi za chini na kati ambao hawahusiki na maandalizi ya sera mbalimbali.

Chini ya waraka Na. 1 wa mwaka 1992 watumishi katika kundi “A” na “B” walipewa masharti kuhusu mambo wanayoruhusiwa kufanya na wasiyoruhusiwa kufanya kuhusu ushiriki wao katika siasa ikiwemo za vyama.

Waraka huu uliotoa mwanya wa watumishi wa umma kushiriki katika siasa hususani kupitia uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 na pia chaguzi za Serikali za Mitaa zilizofanyika katika ngazi za Mitaa, Vitongoji na Vijiji mwaka 1994 na 1999.

“Ruksa” iliyotolewa na waraka huo iliotoa uhuru wa watumishi wa umma kushiriki katika masuala ya siasa na kwa kiasi kikubwa watumishi wengi wa umma wakati huo walijitokeza kuunga mkono vyama vya siasa; hususani vya upinzani. Harakati hizo za watumishi wa umma kushiriki siasa wakati huo pamoja ni moja ya sababu zilizochangia upinzani kupata viti vingi bungeni katika uchaguzi wa mwaka 1995 ukilinganisha na chaguzi zote zilizofuata.

Hata hivyo, baada ya chaguzi hizo serikali ilionyesha dhahiri kutoridhishwa na hali hiyo na kueleza kwamba ‘ruksa’ hiyo ya watumishi wa umma kushiriki kwenye siasa ‘imeathiri maadili ya msingi ya utendaji kazi serikalini na vyombo vyake”.

Ilipofika mwanzoni mwa mwaka 2000, wakati taifa likiwa linajiandaa na uchaguzi mkuu wa pili chini ya mfumo wa vyama vingi serikali ya wakati huo chini ya Urais wa Benjamin Mkapa ilieleza kutoridhishwa na kiwango cha ‘ruksa’ ambayo watumishi wa umma wamepewa kushiriki katika siasa.

Serikali ikaeleza kwamba uhuru ambao watumishi wa umma wapewa kushiriki kwenye siasa unafanya baadhi yao kutotekeleza kwa dhati sera za chama tawala. Kadhalika serikali ikalalamika kwamba wapo watumishi wa umma wanaoikashifu serikali kufuatana na msimamo wa kisiasa. Pia yalikuwepo malalamiko ya pande zote kuhusu athari za kujihusisha na masuala ya siasa mahali pa kazi na wakati wa saa za kazi. Baadhi ya watumishi wa umma pia walilalamikiwa kwa kutoa huduma za kiutumishi kwa upendeleo unaotokana na msimamo wa kisiasa. Kwa upande mwingine, waliokuwepo pia watumishi wa serikali kuu waliojitokeza kugombea nafasi za uongozi/siasa katika serikali za mitaa jambo ambalo lilikwenda kinyume na dhana ya utenganishaji wa madaraka kati ya watungaji wa sera ambao ni viongozi wenye mwelekeo wa kisiasa na wale watekelezaji wa sera ambao kwa kawaida wanatakiwa kuwa watendaji.

Aidha palikuwepo na utata kuhusu mgawanyo wa watumishi katika makundi “A” na “B” kutokana na vigezo kutokuwa wazi na kutoeleweka vizuri hivyo wakati mwingine ulizua mkanganyiko juu ya mtumishi yupi yupo katika kundi lipi.

Kwa kiasi kikubwa baadhi ya kasoro zilichangiwa na ombwe na udhaifu iliokuwepo kwenye waraka wenyewe. Kwa mfano mbali na makundi ambayo nimeyadokeza hapo juu kuna makundi ya watumishi wa umma ambao hawakuorodheshwa kabisa katika waraka lakini kwa mujibu wa katiba wametajwa. Hawa ni watumishi ambao katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeeleza wazi kwamba hawaruhusiwi kuwa wanachama wa chama chochote cha siasa. Hawa ni watumishi wa umma ambao ruksa yao pekee ya kushiriki kwenye vyama vya siasa ni ya kupiga kura. Ni kundi la watumishi wa umma ambao hawaruhusiwi kushiriki katika shughuli zozote zingine za kisiasa isipokuwa kupiga kura tu. Ibara ya 147(3) na (4) ya Katiba imewataja Askari wa Jeshi la Wananchi(JWTZ), Jeshi la Kujenga Taifa(JKT), Polisi na Magereza. Pia Ibara ya 113A imewakataza majaji na mahakimu wa ngazi zote. Kadhalika Ibara 74(14) na (15) imewazuia wajumbe na watumishi wa Tume ya Uchaguzi na Wasimamizi wa Uchaguzi.

Kasoro nyingine ya waraka huo ilikuwa ni kutoyaraja makundi mengine ambayo pamoja ni kuwa hayajakatazwa na katiba kushiriki kwenye shughuli za kawaida za kisiasa lakini kwa mujibu wa kazi zao wanapaswa kushiriki kwa kupiga kura tu. Mathalani, watumishi wa idara ya usalama wa taifa, taasisi ya kuzuia rushwa(wakati huo), msajili wa vyama vya siasa, watumishi wa ofisi ya bunge na mawakili wa serikali.

Kutokana na hali hiyo, ilipofika Mwezi Juni mwaka 2000 serikali ilitangaza kufuta waraka wa Mkuu wa Utumishi wa Umma Na. 1 wa Mwaka 1992 na kutoa waraka mwingine kuhusu maadili ya watumishi wa umma katika mfumo wa vyama vingi vya siasa ambao tutaufanyia mapitio kuanzia makala inayofuata. Sababu kuu iliyopelekea serikali kufikia maamuzi hayo ni kile kilichoelezwa kuwa ni ‘vitendo vya watumishi wa umma vinavyokiuka maadili ya utumishi wa umma kwa kisingizio cha uhuru uliotolewa wa kushiriki katika mambo ya siasa’.

Hata hivyo kwa watetezi wa demokrasia na maendeleo waraka huo wa mwaka 1992 ulionekana kuwa na udhaifu wa msingi wa kimaudhui na kimaadili. Waraka huo haukuweza kuviruka viunzi vya kikatiba na kisheria ambavyo vilikuwepo ambavyo vimeendeleza fungamano kati watumishi wa umma, chama kinachotawala na serikali ikiwemo vyombo vya dola na hivyo kuathiri ushindani wa kisiasa. Ikumbukwe kwamba mapendekezo ya Tume ya Nyalali ya mwaka 1991 na marekebisho ya Katiba ya mwaka 1992 kuingia katika mfumo wa vyama vingi na marekebisho ya sheria yaliyofuata yameweza kupunguza kwa kiasi hali hiyo.

Lakini bado fungamano kati ya chama tawala na serikali ikiwemo vyombo vya dola linahitaji kuendelea kujadiliwa ili mabadiliko ya kweli yaweze kufanyika. Mabadiliko hayo ya kikatiba, kisheria na kimitazamo yatawezesha kuwa na tunu za kitaifa, misingi kamili ya haki za raia, mifumo ya uwajibakaji wa viongozi na uwanja sawa wa kisiasa. Mabadiliko hayo yatawezesha pia kujenga taasisi za kitaifa, uongozi bora na dira ya pamoja yenye kuunganisha nguvu za umma katika kupambana na ufisadi, kutetea rasilimali na kusimamia fikra mbadala zenye kujenga taifa lenye kutoa fursa kwa wote. Taifa wananchi wanaweza kuneemeka na uwezo ambao wamejaliwa wao na nchi kwa ujumla. Sehemu ya wananchi hao ambao ushiriki wao kwenye siasa unapaswa kuwa wa maana na wenye manufaa ni watumishi wa umma.


Mwandishi wa Makala hii ni Mkurugenzi wa Mambo ya Nje(CHADEMA) anapatikana kupitia 0754694553, mnyika@chadema.net na http://mnyika.blogspot.com

No comments: