Thursday, March 3, 2011

TAMKO LA AWALI KUHUSU KUBOMOLEWA KWA SOKO LA URAFIKI

Tarehe 2 Machi 2011 nikiwa mkoani Kagera kwenye maandamano ya kitaifa ya kupinga kupanda kwa gharama za maisha, kupanda kwa bei na mgawo wa umeme, , kutaka uchaguzi wa Meya wa Arusha, kutaka waziri wa ulinzi awajibike kutokana na milipuko na mabomu ya Gongo la Mboto na kupinga malipo ya fidia kwa kampuni ya Dowans yenye mitambo yake katika jimbo la Ubungo- masuala ambayo yanagusa maisha ya watanzania wakiwemo wakazi wenzangu wa jimbo la Ubungo; nimepokea taarifa za kuvunjwa kwa Soko la Wafanyabiashara wa mitumba Urafiki maarufu kama “Big Brother” usiku wa kati ya saa 6 na 7 wa kuamkia siku hiyo.

Awali ya yote ieleweke wazi kuwa kwa nafasi ya yangu ya ubunge wa Ubungo naunga mkono uamuzi wa upanuzi wa Barabara ya Morogoro kwa ajili ya njia ya mabasi ya haraka mkoani Dar es salaam (DART) kwa kuwa ni kati ya masuala ambayo niliyaweka mstari wa mbele kwenye miundombinu na kwa miaka kadhaa nimekuwa nikiilaumu serikali kwa uzembe wa kuchelewesha utekelezaji wa mradi husika.

Hata hivyo, nalaani hatua ya serikali kutokuwa makini katika utendaji wake kwenye utekelezaji wa miradi na hatimaye kusababisha migogoro isiyokuwa ya lazima na madhara katika mali za watu kama ilivyokuwa kwenye uvunjaji wa soko la mitumba la Urafiki maarufu kama Big Brother.

Ni muhimu umma wa watanzania ukafahamu kuwa wafanyabiashara wa eneo la Urafiki Big Brother hawakuvamia eneo husika bali walihamishiwa na manispaa ya Kinondoni toka eneo la Manzese Darajani na kutengewa eneo husika kwa ajili ya mabanda yao ya biashara ya mitumba. Hivyo, uamuzi wowote wa kuwahamisha ulipaswa kuambatana na maandalizi thabiti ya eneo mbadala la kufanyia biashara zao ama sivyo serikali inakuwa imeingia katika kashfa ya kuondoa watu wake kwa ajira zao bila sababu za msingi.

Pia, serikali makini inapaswa kutoa taarifa za ukweli na kwa wakati kwa wananchi wake katika hatua zote za utekelezaji wa miradi katika masuala yanayowagusa wananchi. Kimsingi, katika suala la uvunjaji wa soko la Mitumba la Urafiki maarufu kama Big Brother serikali imeshiriki kutoa taarifa za uongo kwa wananchi na pia waliotumwa kutekeleza zoezi husika wanatuhumiwa kufanya wizi. Pia, hatua za kuwaondoa kwa notisi ya siku chache ni kuweka mazingira ya hasara na kuwakosesha ajira na hivyo kuchangia katika kuongeza umasikini hususani kwa wanawake na vijana.

Ni muhimu wananchi wakafahamu kwamba tarehe 1 Februari mwaka 2011 tulifanya ziara ya kukagua miradi ya Barabara mkoani Dar es salaam na kati ya miradi ambayo tuliikagua ni ya Barabara hiyo ya Morogoro kuhusiana na mradi wa mabasi yaendayo haraka (DART) na kati ya maeneo tuliyotembelea ni hilo la soko la mitumba Urafiki maarufu kama Big Brother.

Tukiwa kwenye eneo hilo mbele ya baadhi ya wafanyabiashara hao ndogondogo wakiongozwa na Mwenyekiti wa Soko hilo Iddi Toatoa maofisa wa mradi wa mabasi ya haraka (DART) waliulizwa kwa mujibu wa mipango ya mradi wao ni jambo gani linahitajika kufanyika katika eneo hilo ili mradi utekelezwe kwa haraka. Ilielezwa kwamba kinachohitajika ni kusogezwa kwa nguzo moja ya umeme ambayo itahusishwa kuondolewa kwa muda kwa vibanda vichache kuwezesha nguzo hiyo kuhamishwa na kwamba biashara ya mitumba katika eneo hilo ingeendelea kama kawaida.

Maelezo hayo yalitolewa mbele ya Afisa Tawala wa Manispaa ya Kinondoni Ndugu Benard ambaye alikuwa akimwakilisha mkuu wa Wilaya Jordan Rugimbana na mbele yangu pamoja na maofisa wengine wa mamlaka mbalimbali wakiwakilisha manispaa, wakala wa barabara (TANROADS).

Katika mazungumzo hayo ilielezwa kwamba Afisa Tawala Manispaa ya Kinondoni atatoa taarifa kwa mkuu wa wilaya na pia Mkurugenzi wa Manispaa ili hatimaye manispaa ambayo ndiyo wameingia makubaliano na wafanyabiashara wa eneo husika kuweza kufanya taratibu ili kazi husika iweze kufanyika.

Taarifa hiyo ya ukaguzi wa miradi ikiwemo kuhusu eneo husika ilitolewa kwenye kikao cha bodi ya barabara cha tarehe 2 Februari 2011 ambacho mimi ni mjumbe. Katika vikao hivyo, hakukutolewa maelezo ya kwamba soko zima litavunjwa badala yake kilichoelezwa ni uhamishaji wa nguzo. Na wakati wote manispaa imekuwa ikisisiza kwamba kwa wafanyabiashara wataothirika watapatiwa maeneo mbadala ya kufanyia biashara zao.

Toka tarehe hiyo, serikali haikutangaza kwa umma hatua mbadala na kuwezesha wafanyabiashara hao kwenda maeneo mbadala mpaka nilipotaarifiwa siku ya tarehe 2 Machi 2011 baada ya kuvunjiwa kuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni alitoa ilani yenye tarehe 14 Februari 2011 iliyosainiwa kwa niaba yake na L.B.KIMOI kuwataarifu watu wote waliojenga mabanda yao yaliyopo ndani ya hifadhi ya barabara ya Morogoro kwenye soko la mitumba la Urafiki kuwa wabomoe na kuondoa mali zao kwa muda wa siku tatu kuanzia tarehe ya ilani tajwa; kwa wengi wa wafanyabiashara hao ilani hiyo ilifika ikiwa imechelewa. Nimeelezwa kwamba kutokana na kuchelewa huko wafanyabiashara hao waliuandikia barua mkurugenzi wa manispaa ya tarehe 1 Machi 2011 wakiomba kupatiwa maeneo mbadala ili waweze kuhamia huko.

Wakati hatua hizo zikiendelea usiku wa siku hiyo hiyo ndipo uvunjaji ukafanyika ambapo wafanyabiashara wanatuhumu kuharibiwa na kuibiwa mali zao na mgambo wa manispaa ambao ndio waliotumwa kutekeleza zoezi husika.

Kutokana na hali hiyo kupitia taarifa hii ya awali natoa matamko yafuatayo:
Mosi; Serikali ikutane na wafanyabiashara hao walioathirika kubaini athari walizozipata na kuwapatia eneo mbadala la biashara kwa kushughulikia mapendekezo yaliyoko kwenye barua yao ya tarehe 1 Machi 2011 ambayo baadhi yake yako ndani kabisa ya uwezo wa manispaa.

Pili; Manispaa ifanye uchunguzi kuhusu vitendo vya uwizi vinavyoelezwa kufanywa na mgambo waliotuma kufanya zoezi husika na kueleza sababu za zoezi hilo kufanyika usiku. Serikali inastahili kuchukua hatua na kutoa fidia ya uwizi huo.

Nne; tarehe 2 Machi 2011 baada ya tukio hilo nilimtuma Diwani wa Kata ya Ubungo Boniface Jacob kufanya mazungumzo ya awali na wafanyabiashara husika pamoja na kuhamasisha utulivu wakati hatua zikiendelea kuchukuliwa, kati ya mambo ambayo yalijitokeza katika mazungumzo yao ni hoja ya wafanyabiashara kutaka kufanya maandamano na haja ya kuchukua hatua za kisheria. Nimepokea mapendekezo hayo na tutafanya maamuzi ya pamoja nikirejea.

Tatu; Katika muktadha huo naitisha Mkutano na wafanyabiashara husika pamoja na watanzania wengine ambao wanatarajiwa kuathiriwa na upanuzi wa barabara ya Morogoro kwa ajili ya mradi wa mabasi yaendayo haraka (DART) ili kupeana taarifa na kukubaliana kuchukua hatua mbalimbali. Mkutano huo utafanyika eneo la Kimara Baruti uwanja wa Central kuanzia saa 4 asubuhi mpaka saa 7 Mchana siku ya jumamosi ya tarehe 5 Machi 2011 ambapo nitakuwa nimerejea jimboni Ubungo. Tamko langu kamili nitalitoa baada ya mkutano huo.

Iwapo Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni hawatatoa taarifa ya kujitosheleza kuhusu suala husika ikiwemo kukutana na waathirika wa bomoa bomoa hiyo kabla au kupitia mkutano huo basi tutajibika kupeleka suala husika kwa mamlaka ya juu zaidi katika hatua ya sasa ikiwa ni kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye pia ni msimamizi wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na kuunganisha nguvu ya umma ili suluhisho la mapema liweze kupatikana.

Wenu katika utumishi wa umma,

John Mnyika
Mbunge-Jimbo la Ubungo
03/03/2011-Kagera

No comments: