Tuesday, May 24, 2011

Tamko kuhusu Umeme

TAMKO LA WAZIRI KIVULI (MSEMAJI WA KAMBI RASMI YA UPINZANI) WIZARA YA NISHATI NA MADINI JUU YA MASUALA, MATUKIO NA MWELEKEO WA SERIKALI KUHUSU UMEME KATIKA KIPINDI CHA MWEZI MEI

Utangulizi

Katika kipindi cha Mwezi Mei yameibuliwa masuala na wadau mbalimbali na zimetolewa kauli kadhaa na serikali kuhusu umeme.

Baadhi ya masuala na matukio hayo ni pamoja na kuanza kwa mgawo mkubwa wa umeme, kutokutekelezwa ipasavyo kwa hatua za dharura za kuongeza uzalishaji wa umeme, tuhuma za ufisadi katika sekta husika na masuala mengine kuhusu umeme yenye kuathiri uchumi wa taifa na maisha ya wananchi hususani wa kipato cha chini.

Kambi ya Upinzani inayoongozwa na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kupitia kwa Waziri Kivuli wa Nishati na Madini imekuwa ikifuatilia kwa karibu matukio na kauli hizo na kubaini kwamba serikali kupitia Wizara husika ya Nishati na Madini haijawajibika ipasavyo kuchukua hatua stahili au kutoa mwelekeo wenye matumaini kwa watanzania hususani katika masuala yafuatayo:

Kuhusu mgawo wa umeme unaotokana na upungufu wa gesi:

Nchi iko katika mgawo mkubwa hivi mpaka tarehe 26 Mei 2011 kwa kile kilichoelezwa ni kutokana na kampuni ya uzalishaji wa gesi asilia ya Songo Songo ya Pan African Energy Tanzania Limited ambayo imetangaza kutosambaza gesi katika kipindi hiki kwa ajili ya ukaguzi na ukarabati mkubwa wa mitambo ya gesi. Hali hii imetokana na mamlaka husika kutokuwajibika ipasavyo kwa kuwa matengenezo haya yalifahamika kwa serikali kuanzia mwishoni mwa mwaka 2010 na mwezi Februari 2011 suala hili lilijadiliwa ndani ya serikali lakini hatua stahili hazikuchukuliwa kwa wakati kufanya ufuatiliaji na udhibiti uliohitajika.

Kumekuwepo tuhuma za muda mrefu kwamba kampuni ya Pan African imekuwa haifanyi matengenezo ya ukamilifu na kwa wakati hata hivyo Wizara inayohusika haikueleza hatua ambazo zimechukuliwa hali ambayo imeongeza hitaji la matengenezo makubwa kwa wakati mmoja yaliyosababisha gesi kutokusambazwa na kuleta upungufu wa umeme wa kati ya MW 200 mpaka 359 katika kipindi husika. Kwa kuwa serikali ilifahamu mahitaji ya matengenezo hayo miezi mingi kabla ingeweza kuweka mfumo wa uhifadhi wa gesi kwa ajili ya kuepusha hasara ambayo inalikumba taifa hivi sasa. Aidha serikali imekuwa pia ikifahamu kuhusu tatizo lingine la kutopanuliwa ipasavyo kwa miundombinu ya kusafirisha gesi (re rating) kunakopaswa kufanywa na kampuni ya Pan African.

Hali hii ya utegemezi wa serikali kwenye sekta ya gesi kwa makampuni yenye mwelekeo wa udalali imesababisha hasara kwa serikali lakini ina mwelekeo pia wa kuhatarisha usalama wa nchi katika siku za usoni kama hatua stahili hazitachukuliwa; hivyo Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) inapaswa kuchunguza hali hiyo na kuchukua hatua stahili. Aidha Serikali inapaswa kupitia upya mikataba na makampuni ya Songas, Pan African na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) ili kuondoa migongano na kupunguza mzigo kwa taifa wakati gesi asilia ni mali asili ya watanzania sanjari na kupanua wigo wa usafirishaji wa gesi katika mwaka wa fedha 2011/2012.

Kuhusu kusuasua kwa hatua za dharura za kupunguza upungufu wa umeme:

Kwa upande mwingine, natahadharisha kwamba mgawo mkubwa na wa muda mrefu utalikumba taifa kuanzia mwezi Julai 2011 kutokana na hatua za dharura kutochukuliwa kwa wakati. Pamoja na Serikali kushikilia msimamo wa kukodi mitambo ya umeme wa MW 260 ambayo itatumika kwa kipindi cha miezi sita pekee kwa gharama za zaidi ya bilioni 400 badala ya kuweka mkazo katika kununua mitambo kama ambavyo imeshauriwa na wadau mbalimbali; Wizara ya Nishati na Madini haijawajibika kwa kiasi cha kutosha kuhakikisha nchi haikumbwi na mgawo katika kipindi husika.

Mchakato wa kutekeleza mpango wa dharura umecheleweshwa na hivyo kuna hatari ya mitambo hiyo kuwa tayari kutoa huduma mwezi Januari katika kipindi ambacho haihitajiki na kusababisha hasara kwa taifa kama ilivyokuwa kwa mitambo ya Richmond/Dowans.

Hivyo, serikali inapaswa kutangaza kusitisha mara moja mpango huo na kuelekeza fedha hizo za umma katika hatua za dharura za kununua mitambo ya kudumu; kinyume na hapo itathibitika kwamba kuna mazingira ya ufisadi katika mpango huo wenye kutaka kuongeza mzigo wa madeni kwa TANESCO na gharama za umeme kwa wananchi wa kawaida.
Izingatiwe kwamba madhara na hasara yote ambayo wananchi, sekta binafsi na serikali imekuwa ikipata kuanzia mwezi Februari mwaka 2011 mpaka Disemba 2012 kwa kipindi cha takribani mwaka mzima inatokana na kutokuwajibika kikamilifu kwa mamlaka husika kwa kuwa dharura ilifahamika toka mwaka 2008 na serikali ikapanga kwamba utekelezaji wa miradi ya MW 60 wa kutumia mafuta mazito Mwanza na Mradi wa MW 100 wa kutumia gesi asilia Ubungo, na wa MW 200 Kiwira ilipaswa kukamilika Februari 2011; hata hivyo kutokana na uzembe na ufisadi sasa miradi hiyo itakamilika 2012/2013.

Hivyo, serikali kupitia TANESCO na kwa kushirikiana na sekta binafsi iweke mazingira wezeshi ya kisheria, kikanuni na kibajeti msingi wa utekelezaji wa miradi ya Kiwira (MW 200), Somangafungu (MW 230), Mnazi Bay (MW 300), Kinyerezi (MW 240), maporomoko ya Ruhudji (MW 358) ili ianze kwa haraka zaidi kwa mwaka wa fedha 2011/2012 tofauti na kusubiria mpaka mwaka 2013/2014 kama serikali inavyopanga hivi sasa.

Kuhusu tuhuma za ufisadi katika manunuzi kwa ajili ya miradi ya umeme:

Mpaka sasa serikali haijawajibika ipasavyo kushughulikia tuhuma za ufisadi katika ununuzi wa mafuta mazito ambayo Waziri wa Nishati na Madini alieleza bungeni tarehe 6 Aprili 2011 kwamba zimetumika bilioni 46 kwa ajili ya kuendesha mitambo ya kufua umeme ya IPTL. Hata hivyo, mwezi Mei Wizara ya Nishati na Madini kupitia taarifa nyingine imesema kwamba fedha zilizotumika kwenye ununuzi wa mafuta katika kipindi husika ni bilioni 28; bila kueleza sababu za kutofautiana kwa maelezo ya waziri bungeni na haya yaliyotolewa sasa na Waziri. Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) ulishatoa tamko kwamba pamoja na RITA kusimamia IPTL hawana mamlaka, fedha hazipitii kwao na kwamba hata taratibu zote za manunuzi na maamuzi mazito hufanywa na serikali kuu. Wizara ya Nishati na Madini ilipaswa kutoa maelezo kuhusu tuhuma hizo na iwapo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imeanza kuzichunguza. Kutokana na hali hiyo, Kamati ya Nishati na Madini inapaswa ifanye uchunguzi maalum kama ilivyoombwa na Zitto Kabwe (Mb) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati za Hesabu za Mashirika ya Umma.

Pia pamekuwepo malalamiko mbalimbali kuhusu mazingira ya kupitishwa kwa zabuni za ununuzi wa nguzo, transforma na nyaya za umeme kwa kiwango kikubwa toka nje ya nchi huku viwanda vya ndani mathalani TANALEC ABB, East African Cables (hususani kampuni tanzu ya Tanzania Cables) na vingine vikididimia. Hali hii imesababisha pia kukwama kwa utekelezwaji wa miradi mbalimbali ya kusambaza umeme kutokana kwa kile kinachoelezwa kuwa ni vifaa kutokupatikana kwa wakati toka nje ya nchi.

Hitimisho:

Hivyo kutokana na hali hiyo; kama sehemu ya kutekeleza wajibu wa kibunge wa kuisimamia serikali tamko hili linatolewa kutaka Wizara ya Nishati na Madini hususani Waziri wake William Ngeleja (Mb) kuwajibika kutokana na athari za kutochukua hatua kwa wakati na Rais Jakaya Kikwete akiwa ndiye Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri kueleza kwa umma hatua ambazo serikali yake inakusudia kuchukua kurekebisha hali hiyo ikiwemo kuwachukulia hatua kwa wanaohusika. Rais Kikwete alishatembelea Wizara na kutoa maagizo na akarudia tena maagizo yale yale kwa kutumia mamilioni ya walipa kodi kupitia semina elekezi; kinachotakiwa hivi sasa sio maagizo tena bali ni mkuu wa nchi kuchukua hatua. Aidha iwapo tamko hili halitazingatiwa maelezo na vielelezo zaidi vitawasilishwa kwenye vikao vya kambi rasmi ya upinzani na hatimaye masuala husika na mengine zaidi yataibuliwa bungeni kwa ajili ya wahusika kuwajibishwa na pia vipaumbele kuzingatiwa kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2011/2012.

Imetolewa tarehe 22 Mei 2011 na:

John Mnyika (Mb)
Waziri Kivuli (Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani)
Wizara ya Nishati na Madini

No comments: