Saturday, May 21, 2011

Mbunge atoa rambirambi msiba wa msanii

Mbunge wa Ubungo, John Mnyika amesema kuwa amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Mkurugenzi wa kikundi cha maigizo na filamu cha Jakaya Theatre Arts.

Mnyika aliyasema hayo jana (15/05) alipotembelea nyumbani kwa familia ya marehemu katika kata ya Ubungo Jijini Dar es salaam kwa ajili ya kuwasilisha rambirambi.

Akizungumza na mbunge, Chediel Senzighe ambaye ni kaka wa marehemu na mmoja wa wasanii wa kundi hilo anayefamika kwa jina la kisanii kama “Kakoba Chapombe” alisema kwamba marehemu alifikwa na mauti katika ajali iliyotokea juzi eneo la Kimara Resort baada ya kontena la lori la mizigo kuanguka kwenye kituo cha basi.
Chediel ameeleza kuwa maziko ya Thomas Senzighe yanatarajiwa kufanyika kesho na kwamba mwili wa marehemu utaagwa Ubungo eneo la Gide.

Kwa upande mwingine Mnyika amesema kwamba marehemu Thomas Senzighe ameacha pengo katika medani ya sanaa kwa kuwa alikuwa mhimili nyuma ya mafanikio ya kikundi hicho ambacho kimeonyesha maigizo mbalimbali kupitia kituo cha luninga cha ITV mathalani ‘Taharuki’, ‘Kivuli’, ‘Mwiba’ na ‘Kovu la Siri’

Mnyika alisema kwamba mara ya mwisho kuwasiliana na marehemu alimjulisha kwamba wanaandaa filamu na kwamba pamoja na filamu marehemu amekuwa akijishughulisha na kazi za lugha ya Kiswahili kupitia tovuti www.swahilicenter.com.

Imetolewa tarehe 16 Mei 2011

No comments: