Saturday, May 21, 2011

Mbunge ahimiza Wananchi Kwembe kushiriki Mkutano wa Maji

Mbunge wa Ubungo, John Mnyika anahimiza wakazi wa Mtaa wa Kwembe kuitikia mwito wa Kamati ya Maji ya Mtaa huo kujitokeza kwa wingi katika mkutano wa watumiaji wa maji wenye kulenga kuunganisha nguvu katika kukamilisha utekelezaji wa miradi ya kuwezesha maji kupatikana katika maeneo yao.

“Nimepokea taarifa ya katibu wa Kamati Joyce Manyerere kuwa Mkutano utafanyika siku ya Jumamosi tarehe 21 Mei 2011 saa nane mchana katika ofisi ya Mtaa wa Kwembe; nahimiza wananchi husika kuitikia mwito huo”.

Manyerere ameeleza kwamba ufungwaji wa mashine mpya ya kusukuma maji yenye uwezo wa kusukuma Lita 90,000 za maji kwa saa moja katika mradi wa maji safi ya bomba katika Mtaa wa Kwembe, Kata ya Kwembe Manispaa ya Kinondoni umekamilika na majaribio ya kusukuma maji kutoka bomba kuu la Ruvu kuanza rasmi.

Kukamilika kwa kazi hiyo kumefanya Mtaa huo kupata ufadhili mwingine wa kujengewa tanki la kuhifadhi na kusambaza maji kupitia vituo vitano chini ya ufadhili wa mradi wa “Maji Yetu” unaofadhiliwa na Jumuia ya Ulaya (EU) na Belgian Technical Cooperation (BTC). Ujenzi wake unatarajiwa kuanza hivi karibuni.

Aidha Shule 3 ikiwemo moja ya Msingi, mbili za Sekondari pamoja na zahanati ya Mtaa wa Kwembe vinatarajiwa kupata ufadhili wa kujengewa miundombinu ya kuhifadhi maji kutoka Shirika la SAWA mara tu baada ya maji safi ya bomba kuanza kutiririka Mtaa wa Kwembe.

Ili kukamilisha miradi yote hii watumiaji wote wa maji safi ya bomba ambao ni pamoja na wakazi wote wa Mtaa huo, wenye viwanja na mashamba katika Mtaa wa Kwembe watakuwa mkutano wa watumiaji maji utakaofanyika Jumamosi Tar 21 Mei 2011, saa nane mchana katika Ofisi ya Serikali ya Mtaa Kwembe.

Ajenda za mkutano huo ni pamoja na:- Kutambua na kuwaorodhesha wahitaji wa huduma ya maji safi ya bomba katika Mtaa wa Kwembe; Kupanga utaratibu wa usambazaji wa vituo vya maji na mabomba binafsi; Kujadili na kupitisha mchakato wa kuanzisha Umoja/Kampuni ya Watumiaji Maji Mtaa wa Kwembe.

Mkutano huu unafuatia wa awali ambao ulifanyika tarehe 30 Januari 2011 ambapo Mbunge Mnyika alihudhuria na kushirikiana kwa hali na mali katika jitihada za kutatua kero ya maji.

Katika mkutano huo wa kwanza ilibainika kwamba mradi wa maji Kwembe ulichangiwa na washirika wa kimaendeleo mwaka 2000 lakini maji hayatoki kutokana na kutokamilika kwa mradi katika kipindi cha takribani miaka kumi toka fedha za mradi huo zitolewe kwa pamoja na mambo mengine kukosekana nguvu ya wananchi.

Baadhi ya sababu nyingine ni pamoja na kampuni iliyotekeleza mradi huo kutaka marekebisho kadhaa yafanyike katika mfumo wa mabomba yanayounganisha tanki na kupokea na kupokea maji kutoka bomba kuu na pampu kabla ya kuwashwa.

Kamati ya maji ilianisha vifaa vinavyohitajika kuwa ni kuondoa kona kali la kupokea maji toka bomba kuu, kufunga vifaa vya kulinda mashine isiharibike pamoja na vifaa vingine na hatimaye mbunge na wananchi wengine walichangia sehemu ya gharama za vifaa hivyo.

Chanzo: Aziz Himbuka (20/05/2011)

No comments: