Mbunge wa Ubungo, John Mnyika ambaye pia ni Mwenyekiti wa CHADEMA katika Mkoa wa kichama wa Kinondoni amefanya ziara ya kichama katika kata za Mabibo na Manzese jana (22/05/2011) kwa lengo kujenga oganizesheni ya chama ngazi ya chini.
Katika ziara hiyo Mnyika ameingiza wanachama wapya na kufungua misingi/matawi ya chama katika mitaa mbalimbali ya kata hizo sambamba na kuzindua ofisi za chama katika maeneo hayo.
Katika ziara hiyo Mnyika akiambatana na viongozi wa chama na wanachama wa chama hicho walitembea kwa miguu katika nyumba mbalimbali kuwashukuru wananchi kwa kumchagua na kufuatilia masuala ya kimaendeleo.
“ Pamoja na kuwa baada ya uchaguzi nilifanya mikutano ya hadhara ya kiserikali kwa ajili ya kuwashukuru; nimekuja kwenu leo kwa kuwa niliahidi kwamba mkinichagua nitarudi kwa njia ile ile niliyopitia kuomba kura ili kuwashukuru na kushirikiana nanyi kutimiza wajibu”, alisema Mnyika.
Akihutubia wananchi wakati wa uzinduzi wa ofisi ya CHADEMA katika kata ya Mabibo Mtaa wa Jitegemee, Mnyika alieleza manufaa ya kuchagua vyama mbalimbali katika kuleta uwajibikaji kwa kuwa kwa mara ya kwanza halmashauri ya Kinondoni imeweza kutenga bilioni tano katika bajeti ya mwaka wa fedha 2011/2012 kwa ajili ya matengenezo ya barabara.
Mnyika alisema kwamba jumla ya shilingi milioni 595 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo maalum ya Barabara ya kutoka Mburahati mpaka Mabibo eneo la Chuo Cha Usafirishaji (NIT) na kuahidi kuendelea kushirikiana na madiwani kuondoa kasoro nyingine zilizobainika katika bajeti iliyopitishwa.
Akizindua ofisi ya chama kata ya Manzese Mnyika alieleza umuhimu wa kuwa chama thabiti kwa ajili ya kusimamia vizuri utendaji wa serikali na viongozi wa kuchaguliwa na wananchi.
“ Hayati Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kwamba chama legelege, huzaa serikali legelege. Ombwe la kiungozi lililopo kwenye serikali hivi sasa katika ngazi mbalimbali ni ishara ya udhaifu wa chama kinachotawala; CHADEMA lazima ionyeshe tofauti katika kuwawajibisha viongozi wake waweze kuutumikia umma ipasavyo”, alisema Mnyika.
Mnyika alisema CCM inazungumza kujivua gamba lakini bado mafisadi wanakumbatiwa ndani ya serikali na pia serikali inashindwa kushughulikia kikamilifu kero za wananchi kama maji na kupanda kwa gharama za maisha wakati kodi za wananchi hazitumiwi vizuri.
Mnyika alisema kwamba ofisi hiyo ya chama isifanye tu kazi za kuhudumia wanachama bali izibe pengo pale wananchi wanapokwenda kuwasilisha malalamiko yao kwa ofisi za kiserikali lakini hatua stahili hazichukuliwi kwa wakati.
“ Wajibu wenu uwe ni kuunganisha nguvu ya umma, nimetembelea mitaa mbalimbali ya Manzese na kukutana vioski vingi vya Kampuni ya Maji Dar es Salaam (DAWASCO) havitoi maji na sehemu kubwa ya miundombinu ya maji iliharibiwa wakati wa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara na haikurejeshwa. Viongozi wa ngazi ya chini wa kiserikali hawajafuatilia kero hii kwa muda mrefu; hivyo ni wajibu wenu kuwasukuma na mkikwama mtaarifu ngazi za juu kwa hatua zaidi”, alieleza Mnyika.
Akihutubia Mkutano wa hadhara katika Mtaa wa Chakula Bora kata ya Manzese ikiwa ni sehemu ya kuhitimisha ziara hiyo Mnyika aliwaeleza wananchi hatua ambayo amefikia katika kutekeleza ahadi ya kuwawakilisha wananchi kwa kuweka kipaumbele katika masuala ya elimu, ajira, maji, maji, miundombinu, uwajibikaji, usalama, ardhi na afya katika kipindi cha miezi mitano toka achaguliwe na kuahidi kuendelea kuwashikirisha wananchi katika kila hatua atakayofikia.
“ Kuanzia wiki hii tunaanza vikao vya kamati za bunge mpaka mwezi Juni mwanzoni ambapo mkutano wa bunge utaanza rasmi, na hili ni bunge muhimu la bajeti hivyo kuna mambo mengi zaidi itakwenda kuwawakilisha katika mkutano huo na nawashukuru kwa hoja mbalimbali ambazo mmenitaka niziwekee mkazo”, alisema Mnyika.
Imetolewa tarehe 23 Mei 2011 na:
Aziz Himbuka
Katibu Msaidizi
Ofisi ya Mbunge Ubungo
No comments:
Post a Comment