Taarifa inatolewa kwa umma kwamba jana tarehe 6 Mei 2011 Mbunge wa Ubungo, John Mnyika ametembelea kata za Saranga na Kimara kufuatilia utekelezaji wa mipango ya maendeleo.
Akizungumza na wananchi waliomzunguka katika eneo la Golani ambapo matengenezo ya barabara yameanza, Mnyika aliwaeleza wananchi hao kwamba matengenezo hayo yatahusisha ukarabati wa barabara kuanzia Kimara Suca, Golani, Saranga mpaka Temboni.
Aidha Mnyika aliwatangazia wananchi hao kwamba jumla ya shilingi milioni zaidi ya mia tano (501,973,470) zimetengwa kwenye bajeti ya Halmashauri ya Kinondoni kwa mwaka wa Fedha 2011/2012 kwa ajili ya kujenga Daraja Kubwa la Burura/Golani katika Mto Ubungo.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Saranga Ephraim Kinyafu alimshukuru mbunge kwa jitihada za kufuatilia kero za wananchi.
“Kwa zaidi ya miaka kumi wananchi wa eneo hili wamekuwa na kero ambapo nyakati za mvua mawasiliano hukatika lakini katika kipindi kisichofikia hata mwaka mmoja umefanikiwa kushawishi fedha kutengwa kwa ajili ya mradi huu muhimu”, alisema Kinyafu.
Kwa upande mwingine, akizungumza na wakazi wa Mavurunza katika mkutano uliofanyikia katika ukumbi wa G5 Mnyika aliwataarifu wananchi kwamba matengenezo ya Barabara ya Kimara, Mavurunza mpaka Bonyokwa nayo yanatarajiwa kuanza mwezi huu baada ya kupungua kwa mvua.
Akijibu swali la Mwenyekiti wa umoja wa wakazi hao ujulikanao kama Wanaume Upendo, Cleophas Malima kuhusu hatua mahususi ambazo zimechukuliwa na mbunge kuhusu barabara husika ambayo imekuwa kero kwa wananchi; Mnyika alisema kwamba hatua hizo zinahusisha ngazi mbili.
“ Mtakumbuka kwamba ujenzi wa barabara ya Kimara Bonyokwa ni kati ya ahadi ambazo alizitoa Rais Jakaya Kikwete mwezi Mei mwaka 2010. Mara baada ya uchaguzi katika vipindi mbalimbali nimefuatilia kwa karibu utekelezaji wa ahadi hii.
Zoezi la kuipandisha hadhi barabara hii kuwa ya mkoa limeshafanywa na wakala wa barabara (TANROADS) na upembuzi yakinifu umefanyika hivyo kupitia kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Dar es salaam ambacho mimi ni mjumbe cha tarehe 02 Februari 2011 nilitoa mwito kwamba tathmini ya fidia iweze kufanyika mapema zaidi ya ilivyopangwa awali ili hatua za ujenzi zichukuliwe kwa wakati.
Tarehe 21 Aprili 2011 nimewaandikia barua TANROADS yenye kumbukumbu na OMU/MB/006/2011 kuwakumbusha kuzingatia suala hili katika vipaumbele vya bajeti ya mwaka wa fedha 2011/2012 kama sehemu ya mkakati wa kupunguza foleni katika jiji la Dar es salaam kwa kuwa barabara hiyo inaungana na Tabata Segerea”, Alisema Mnyika.
Mnyika aliendelea kufafanua kuwa wakati hatua hiyo ikisubiriwa kunahitajika hatua ya dharura katika kipindi hiki cha mpito kutokana na ubovu mkubwa wa barabara hivyo tarehe 19 Aprili 2011 kupitia kikao cha Kamati ya Fedha na Uongozi cha Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni alitoa mwito kwa mkurugenzi kuhakikisha mhandisi anatembelea eneo hilo na hatua za haraka kuchukuliwa.
Mnyika aliwaeleza wakazi hao kuwa ameshafuatilia katika manispaa na kwamba matengenezo ya barabara hiyo yataanza mwezi huu ili kupunguza adha kwa wananchi na kwamba ukarabati huo usipoanza kwa wakati atawaeleza hatua zitazochukuliwa.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Kimara Pascal Manota alimueleza mbunge maeneo korofi katika barabara hiyo hususani maeneo ya vyumba vinane, kwa kyauke mpaka darajani na kusisitiza kuwa iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa daraja mojawapo litasombwa na maji kutokana na barabara kubomoka na hivyo kusababisha hasara zaidi kwa umma.
Imetolewa tarehe 07/05/2011 na:
Aziz Himbuka
Katibu Msaidizi
Ofisi ya Mbunge
No comments:
Post a Comment