Monday, October 22, 2012

KAULI TATA KUHUSU HALI TETE YA UMEME, UKWELI KWA UKAMILIFU UELEZWE

Katika kipindi cha zaidi ya mwezi mmoja kuanzia mwanzoni mwa mwezi Septemba 2012 mpaka leo tarehe 21 Oktoba 2012 viongozi na watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini na Shirika la Umeme nchini (TANESCO) wamenukuliwa na vyombo vya habari na wakitoa matumaini potofu kwa wananchi kuhusu hali ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme nchini sanjari na uboreshaji wa utendaji wa Shirika la Umeme (TANESCO).

Viongozi na watendaji hao waliozungumza kwa nyakati tofauti na kutoa kauli mbalimbali ni pamoja Waziri Prof. Sospeter Muhongo, Naibu Waziri wa Nishati George Simbachawene, Katibu Mkuu wa Wizara Eliackim Maswi na Kaimu Mkurugenzi wa TANESCO Felchesmi Mramba.

Kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa Nishati na Madini natoa mwito kwa wanahabari na umma kuzipokea kwa tahadhari kauli hizo kwa kuwa hazielezi ukweli kamili kuhusu hali tete ya umeme kutokana na kususua katika utekelezaji wa Mpango wa Dharura wa Umeme kama nilivyohoji bungeni tarehe 27 Julai 2012.

Kwa mujibu wa nyaraka nilizo nazo za ndani ya Wizara ya Nishati na Madini na TANESCO kuanzia mwezi Septemba mpaka mwezi Oktoba 2012 hali ya uzalishaji na usafirishaji na usambazaji wa umeme imekuwa tete kwa sababu mbalimbali ikiwemo upungufu wa upatikanaji wa mafuta na gesi asili kwa ajili uendeshaji wa mitambo ya kufua umeme na kasi ndogo ya uwekezaji kwa ajili ya kupata ufumbuzi wa kudumu.

Hali hii imesababisha mpaka wakati mwingine umeme kutoka kwenye mabwawa kuzalishwa zaidi ya kiwango kilichopangwa na kusababisha kushuka kwa kina cha maji hali yenye kutishia uendelevu wa mabwawa haya kutokana na maelekezo ya Wizara kwa TANESCO ya kuhakikisha mgawo wa umeme hautangazwi kwa namna yoyote.

Kutokana na hali hiyo na kwa kuzingatia kuwa mamlaka na madaraka ya Bunge kwa mujibu wa katiba ni kuisimamia Serikali kwa niaba ya wananchi nimemwandikia barua Spika wa Bunge ili Wizara ya Nishati na Madini iwajibike kueleza halisi halisi katika mikutano ya kamati za bunge inayoendelea hivi sasa.

Aidha, kwa kuwa kwa sasa Nchi haina Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini ambapo Wizara ingelazimika kueleza ukweli kamili na halisi nimemwandikia Spika atumie madaraka na mamlaka yake kwa mujibu wa Kanuni ya 116 na Kanuni ya 114 fasili ya 14 kukabidhi suala hilo lishughulikiwe na kamati nyingine miongoni mwa Kamati za Kudumu za Bunge zinazoendelea na vikao vyake hivi sasa.

Kwa barua hiyo nimependekeza pamoja na mambo mengine suala la kupokea na kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango wa Dharura wa Umeme na utekelezaji wa mpango wa uboreshaji wa utendaji wa Shirika la Umeme (TANESCO) lishughulikiwe na kamati nyingine kwa haraka kwa kuzingatia maelezo na maelekezo ya Spika aliyoyatoa bungeni wakati wa kuahirisha mkutano wa nane wa Bunge.

Nitakabidhi sehemu ya nyaraka nilizonazo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge itakayoelekezwa na Spika kushughulikia jambo hili lakini iwapo hatua za haraka hazitachuliwa nitatoa baadhi ya nyaraka hizo kwa wanahabari na umma ili Wizara ya Nishati na Madini na TANESCO wawajibishwe kueleza ukweli kwa ukamilifu.

Kwa upande mwingine, mapitio ya utekelezaji wa mpango wa uboreshaji wa utendaji wa Shirika la Umeme (TANESCO) yahusishe pia Kamati ya Kudumu ya Bunge itakayopewa jukumu hilo kuelezwa hatua iliyofikiwa katika uchunguzi wa tuhuma za ufisadi katika TANESCO kwa kuzingatia kuwa siku 60 zimepita ambazo ilielezwa kuwa uchunguzi utakuwa umekamilika.

Ikumbukwe kwamba mwanzoni mwezi Agosti Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (NAOT) iliunda timu ya wakaguzi kufanya ukaguzi maalum wa hesabu za Shirika la Umeme (TANESCO) kufuatia tuhuma za ubadhirifu wa fedha za umma zilitajwa bungeni na Waziri Kivuli wa Nishati na Madini katika maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani tarehe 27 Julai 2012 na Waziri wa Nishati na Madini wakati wa majumuisho ya hoja ya Serikali tarehe 28 Julai 2012.

Aidha Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) nayo ilinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari mwezi Agosti mwanzoni kuanza uchunguzi wa mchakato wa ununuzi wa mafuta mazito ya kuendeshea mitambo ya kufua umeme wa dharura kutokana na tuhuma mbalimbali zilizotolewa bungeni kuhusu ununuzi huo suala ambalo Kambi Rasmi ya Upinzani ilitaka pia tarehe 27 Julai 2012 liundiwe kamati teule ya Bunge ili uchunguzi wa kina uweze kufanyika.

Masuala haya ni muhimu yakafuatiliwa wakati wa vikao vya kamati za kudumu za Bunge vinavyoendelea hivi sasa kwa kuzingatia wakati Mkutano wa Nane wa Bunge uliopita pamoja na Spika kutangaza kuwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imevunjwa alieleza kuwa majukumu yaliyokuwa yakishughulikiwa na kamati hiyo yatashughulikiwa na kamati nyingine kwa mujibu wa madaraka na mamlaka ya Spika.

Hivyo Spika anapaswa kuizingatia barua yangu na kutoa pia kauli kwa umma ya kuwezesha mambo hayo na mengine kushughulikiwa na Kamati nyingine ya Kudumu ya Bunge atakayoelekeza ili kusiwe na kisingizio cha kutokuingizwa katika ratiba ya mkutano wa tisa wa Bunge uliopangwa kuanza tarehe 30 Oktoba 2012.

Wenu katika uwakilishi wa wananchi,

John Mnyika (Mb)
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini
21 Oktoba 2012

No comments: