Monday, October 29, 2012

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Awali ya yote niwatikie nyinyi wanahabari kheri ya sikukuu na kupitia kwenu nifikishe salamu kwa ndugu zetu waislam na watanzania wote katika kuadhimisha Iddi Ell-Hajj.

Tarehe 15 Oktoba 2012 nilitoa taarifa kwa umma kuwa niliwasilisha kwa Katibu wa Bunge kusudio la kuwasilisha Muswada Binafsi wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (The Social Security Laws (Ammendments) Act wa mwaka 2012 kwa hati ya dharura kwa mujibu wa Kanuni ya 81 ya Kanuni za Kudumu za Bunge (Toleo la Mwaka 2007) iwapo Serikali haitatoa kauli kwa umma ya ratiba ya kupata mapendekezo toka kwa wadau wa hifadhi ya jamii pamoja na kamati husika ya kudumu ya Bunge na kuwasilisha muswada husika bungeni kama ilivyoazimiwa bungeni tarehe 6 Julai 2012.

Kufuatia hatua yangu na hatua za wadau wengine Serikali kinyume na msimamo wa awali ambalo ulielezwa na Naibu Waziri wa Kazi na Ajira Makongoro Mahanga tarehe 14 October 2012 ambaye alieleza kuwa marekebisho ya kurejesha fao la kujitoa hayatafanyika mpaka mkutano wa kumi wa Bunge mwezi Februari mwaka 2013; Serikali imechapa katika gazeti la Serikali Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali na. 40 Juzuu namba 93 ambao katika sehemu ya 6 vifungu vya 13, 14 na 15 imependekeza kurejesha fao la kujitoa kwa upande wa mfuko mmoja wa mashirika ya umma (PPF) hata hivyo muswada huo haujawasilishwa kwa hati ya dharura kama ilivyoazimiwa na kuahidiwa.

Kwa upande mwingine, sehemu hiyo ya sita ya muswada huo wa marekebisho ya sheria mbalimbali haijakidhi mahitaji na matakwa ya azimio la bunge la tarehe 6 Agosti 2012 lililoungwa mkono na wabunge katika kikao cha 41 cha Mkutano wa Nane wa Bunge na itasababisha mgogoro mwingine katika ya serikali na wafanyakazi kwa upande mmoja, wafanyakazi na waajiri kwa upande mwingine na kuathiri uchumi wa nchi na maisha ya wafanyakazi katika maeneo mbalimbali nchini kwa kutoresha fao la kujitoa katika mifuko mingine ikiwemo NSSF, PSPF na LAPF.

Kwa kuzingatia kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara imeeleza kuwa Rais ndiye mkuu wa Nchi na Kiongozi wa Serikali na Ibara ya 34 imeeleza kwamba mamlaka yote yapo mikononi mwake na kwamba madaraka hayo yanaweza kutekelezwa na watu wengine kwa niaba yake na kwamba Ibara ya 35 imeeleza bayana kwamba shughuli zote za serikali zitatekelezwa na watumishi wa serikali kwa niaba yake; wakati umefika sasa wa wafanyakazi na wadau wengine kuchukua hatua za kuwezesha  Rais kuingilia kati kabla ya mkutano wa Bunge kuanza tarehe 30 Oktoba 2012 kutumia madaraka na mamlaka yake kuondoa udhaifu uliojitokeza wa Waziri wa Kazi na Ajira Gaudencia Kabaka, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Fredrick Werema na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) Irene Isaka kutokutekeleza kwa wakati na kwa ukamilifu mapendekezo na maamuzi ya Bunge pamoja na ahadi za Serikali kwa wabunge.

Mosi; Rais azingatie masharti ya Kanuni za Kudumu za Bunge na kutia saini hati ya  dharura ya kuwezesha muswada wa marekebisho ya sheria mbalimbali wenye vifungu vya nyongeza vinavyowezesha fao la kujitoa kurejeshwa kwa mifuko yote ikiwemo NSSF, PSPF na LAPF kuwasilishwa bungeni. Kanuni ya 80 Fasili ya 4 inaelekeza kwamba “Muswada wowote wa sheria wa Serikali wa dharura hautaingizwa kwenye shughuli za Bunge bila ya kuwa na hati iliyowekwa saini na Rais inayoelekeza kuwa muswada uliotajwa kwenye hati hiyo ni wa dharura”.

Iwapo Rais hataweka saini hati ya dharura au Serikali haitawasilisha bungeni hoja kwa mujibu wa Kanuni ya 93 fasili ya 4 bunge litabanwa na fasili ya 1 ambayo inakataza bunge kushughulikia hatua zaidi ya moja katika mkutano mmoja wa bunge; tafsiri yake ni kwamba sheria hii itasubiri kupitishwa katika mkutano wa kumi wa Bunge mwezi Februari 2012 na hivyo wafanyakazi kuendelea kunyimwa mafao ya kujitoa kinyume na azimio la Bunge.

Pili, Rais atengue tangazo na agizo la Mamlaka ya Udhibiti wa Hifadhi ya Jamii (SSRA)  kueleza kuwa “kufuatia kuanza kutumika kwa Sheria hiyo (ya 13 Aprili 2012) maombi mapya ya kujitoa yamesitishwa kwa kipindi cha miezi sita hadi pale miongozo itakapotolewa ili kuwezesha Mamlaka na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kutoa elimu kwa Wadau” ambalo limesababisha mifuko yote kuacha kutoa mafao ya kujitoa hata kwa wafanyakazi .

Hii ni kwa sababu marekebisho ya sheria ya mifuko ya hifadhi ya jamii kwa upande wa kusitisha fao la kujitoa yaliyofanyika tarehe 13 Aprili 2012 yalihusu zaidi Mfuko wa Mashirika ya Umma (PPF); hivyo hayakupaswa kabisa kutumika kama sababu ya kusitisha mafao kwa mifuko yote ikiwemo NSSF, PSPF na LAPF na kwa upande mwingine wafanyakazi wanaodai mafao hayo kabla ya kujiunga na mifuko hiyo walijiunga wakiwa wameelezwa kama kati ya haki na stahili zao ni pamoja na kupata fao la kujitoa mazingira yakilazimisha hivyo kabla ya pensheni ya uzeeni. Hivyo, kusubiriwa kwa marekebisho ya sheria hakupaswi kuwa kisingizio cha kuendelea kusitisha mafao yao ya kujitoa, ama sivyo Rais aeleze sababu za ziada za kuzuia mafao ya kujitoa kwa kuzingatia Taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali juu ya uendelevu wa mifuko katika siku  chache zijazo kufuatia kushindwa kwa makampuni na Serikali yenyewe iliyokopeshwa na mifuko ya hifadhi ya jamii kuheshimu matakwa ya malipo ya mikopo kutoka mifuko husika ambayo fedha zake zinatokana na makato ya pensheni toka kwa wafanyakazi na waajiri.

Rais arejee kumbukumbu rasmi ya Bunge (Hansard) ya tarehe 7 Agosti 2012 za kikao cha 42 cha Mkutano wa Nane wa Bunge ambao nilishika mshahara wa Waziri Bunge lilipokaa kama kamati na  “nilitaka ufafanuzi wa kisera wa Serikali pamoja na uamuzi wa kuahidi kwamba kwenye mkutano wa Bunge ujao italeta Muswada wa dharura kuhusiana na Fao la Kujitoa, nilitaka kauli ya Serikali juu ya agizo lilitolewa na SSRA la kusitisha utoaji wa mafao ya kujitoa katika kipindi hiki cha miezi sita (6) na kuhusiana na wafanyakazi waliosimamishwa katika hatua ya kudai hayo mafao.

Sasa iwapo Wizara inatoa kauli ya kutengua sitisho hilo na vilevile inatoa kauli ya kutaka kurejeshwa kwa wafanyakazi waliosimamishwa katika hatua ya madai ya fao hili la kujitoa”. Waziri wa Kazi na Ajira alijibu kuwa “tutalifanyia kazi agizo hilo”, hata hivyo mpaka sasa agizo hilo la SSRA halijatenguliwa na wafanyakazi waliosimamishwa wengine hawajarudishwa mpaka hivi sasa na baadhi wamefukuzwa kazi kabisa kutokana na mgogoro uliosababishwa na Serikali kusitisha fao la kujitoa bila kuzingatia haki za binadamu, mazingira ya ujira nchini na ushirikishwaji wa wafanyakazi na wadau wengine muhimu wa hifadhi ya jamii.

Wenu katika utumishi wa umma,


John John Mnyika (Mb)
26/10/2012

1 comment:

Kagaruki said...

Mkuu, nguvu zako hazikupotea bure,hili limezaa matunda, and as we speek tumeshaanza process na tumeahidiwa malipo by 22nd Nov 2012. Tunashukuru kwa jitihada zako.