Saturday, October 6, 2012

Taarifa ya ufafanuzi kuhusu utafutaji wa mafuta na gesi asili nchini iliyotolewa na Wizara ya Nishati na Madini tarehe 21 Septemba 2012 ifutwe kwa kuwa italinda ufisadi na kukwaza utetezi wa rasilimali za taifa:


Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo afute taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo kuwa lengo la agizo lake la kupitiwa kwa mikataba yote 26 ya utafutaji mafuta na gesi asili ni “kuhakikisha kwamba endapo kuna mapungufu katika mikataba hiyo, mapungufu hayo yasijirudie tena katika mikataba mipya ya baadaye” kwa kuwa ikiachwa ilivyo italinda ufisadi na kukwaza utetezi wa rasilimali za taifa.

Ufafanuzi uliotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini unatoa mwanya kwa mikataba mibovu kulindwa wakati ambapo kuna madai tuliyotoa toka mwaka 2011 kwamba baadhi ya mikataba hiyo imeingiwa kifisadi na mwaka huu wa 2012 zimeibuka tuhuma za vigogo wa serikali kuingiziwa fedha kifisadi katika akaunti zao za nchini Uswisi na makampuni ya nje ya utafutaji mafuta na gesi asili.

Tafsiri ya ufafanuzi huo uliotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini ni kwamba hata kama mikataba iliyopo ina mapungufu yasiyozingatia maslahi ya taifa, matokeo ya mapitio hayo hayatarekebisha mikataba iliyopo bali mikataba ya baadaye.

Taarifa hiyo ya Katibu Mkuu wa Wizara ni ya kurudi nyuma tofauti na kauli za awali za Waziri Muhongo zilizokubaliana na madai yetu ya toka mwaka 2011 ndani na nje ya bunge ikiwemo kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa Nishati na Madini ya kutaka mikataba yote ipitiwe upya, isiyozingatia maslahi ya taifa ivunjwe au ifanyiwe marekebisho makubwa na mikataba mipya isiingiwe mpaka kwanza kuwepo sera na sheria bora zenye kulinda uchumi na usalama wa nchi.

Itakumbukwa kwamba tarehe 15 Septemba 2012 wakati wa uzinduzi wa Bodi Mpya ya Wakurugenzi ya Shirika la Maendeleo la Petroli Tanzania (TPDC) Waziri wa Nishati na Madini aliagiza bodi hiyo kuipitia mikataba yote 26 ya utafutaji mafuta na gesi asili ili kujiridhisha endapo maslahi ya taifa yalizingatiwa.

Agizo hilo la Waziri limeendana na mapendekezo niliyotoa mwaka 2011 ya kutaka mapitio ya mikataba yote ya mafuta na gesi asili ambapo pamoja na mambo mengine niliitaka Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini na taasisi zake kuacha kuingia mikataba ya muda mrefu  ya utafutaji wa mafuta na gesi asili katika maeneo mbalimbali nchini yenye mianya ya kuhujumu uchumi wa nchi na haki za wananchi masuala ambayo yalipingwa na Waziri wa zamani.

Kutokana na kutozingatiwa kwa mapendekezo hayo tarehe 21 Februari 2012 nilitoa kauli ya kutaka Waziri wa Nishati na Madini wa wakati huo William Ngeleja kuwajibishwa kwa kuendelea kuruhusu kusainiwa kwa mikataba bila maagizo ya msingi kuzingatiwa na kueleza kwa umma sababu za serikali kuendeleza usiri na kuacha kufanya mapitio ya mikataba mibovu iliyopo.

Nilitoa kauli hiyo baada ya tarehe 20 Februari 2012 Serikali kusaini mkataba wa kutafuta mafuta na gesi asili na kampuni ya Swala katika maeneo ya Kilosa Mkoani Morogoro na Pangani Mkoani Tanga na Januari 2012 Serikali kuweka saini mikataba na kampuni za kimataifa za Petrobras Tanzania Ltd, Heritage Rukwa Tanzania Ltd na Motherland Industies Ltd na Oktoba 2011 Serikali kusaini mikataba mingine na kampuni za Ndovu Resource na Heritage Oil za Uingereza kwa ajili ya utafutaji wa nishati ya mafuta na gesi katika kisiwa cha Songosongo na Ziwa Rukwa huku nchi ikiwa haina mwelekeo sahihi wa sera, sheria, mipango na usimamizi wa sekta hizo nyeti kwa usalama na uchumi wa nchi na maisha ya wananchi kwa ujumla.

Waziri Muhongo na Katibu Mkuu Maswi wanapaswa kuendelea kuonyesha kwa maneno na matendo tofauti yao na viongozi waliowatangulia katika Wizara ya Nishati na Madini Waziri Ngeleja na Katibu Mkuu Jairo kwa kutoa ufafanuzi wa ziada na kuchukua hatua zaidi vinginevyo taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa tarehe 21 Septemba 2012 itakuwa ni mwendelezo wa kulinda udhaifu wa kimfumo uliojikita katika Wizara hiyo na serikali kwa ujumla.

Ni vizuri Waziri na Katibu Mkuu wakaendelea kuzingatia ushauri niliwapa bungeni kwamba sehemu kubwa matatizo katika sekta za nishati na madini yamechangiwa na sababu za kibinadamu za kutowajibika ipasavyo kisera, kimaamuzi, kiusimamizi na kiutendaji kwa viongozi wa kiserikali wenye dhamana na watendaji wengine na hivyo kusababisha ugumu wa maisha kwa wananchi na kuathiri uchumi wa nchi; hivyo nguvu zielekezwe katika kurekebisha hali hiyo.

Imetolewa tarehe 4 Oktoba 2012 na:

John Mnyika (Mb)
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini

No comments: