Sunday, October 7, 2012

KUELEKEA WIKI YA VIJANA: WAZIRI AELEZE HATUA ILIYOFIKIWA KATIKA KUANZISHA BARAZA LA VIJANA, BENKI YA VIJANA NA KUPANUA WIGO WA AJIRA KWA VIJANA

Nikiwa mmoja wa vijana wa Tanzania na mbunge kijana sikubaliani na utaratibu mzima ulivyopangwa wa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dkt Fennela Mukangara kutoa ratiba ya maonyesho na maadhimisho mengine bila kueleza hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa ahadi zilizotolewa kwa vijana katika maadhimisho kama hayo mwaka 2011 na pia kuweka mkazo katika maonyesho katika Mkoa mmoja badala ya masuala na matukio muhimu yenye kugusa maisha ya vijana wa katika maeneo mbalimbali nchini mijini na vijijini.

Ikumbukwe kwamba Tarehe 4 Oktoba 2012 Waziri alizungumza na vyombo vya habari kueleza kuhusu maadhimisho ya Wiki ya Taifa ya Vijana. Waziri alieleza kuwa maadhimisho hayo yatahusisha maonyesho yatakayoanza tarehe 8 na kufikia kilele chake tarehe 14 Oktoba 2012 kwenye kilele cha mbio za Mwenge na kumbukumbu ya kifo cha Mwalimu Nyerere mkoani Shinyanga. Waziri ameeleza kuwa mgeni rasmi katika kilele cha maonyesho na maadhimisho hayo anatarajiwa kuwa Rais Jakaya Kikwete.

Hivyo, natoa mwito kwa vijana katika maeneo mbalimbali nchini kutokubaliana na utaratibu huo wa kuweka kipaumbele katika maonyesho zaidi badala yake wafanye maadhimisho kwa kuweka kipaumbele masuala na matukio yenye kugusa maisha ya vijana na mustakabali wa taifa.

Vijana tuitumie wiki hiyo kutafakari masuala ya msingi baina yetu ili tuweze kutimiza wajibu lakini wakati huo huo tuzifuatilie mamlaka zingine zinazohusika na masuala ya vijana kwa upande wao ikiwemo serikali katika ngazi zote kuhusu utekelezaji wa ahadi mbalimbali zilizotolewa kwa vijana kwa nyakati mbalimbali katika mwaka 2011.

Kwa upande wangu, naitaka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ieleze hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa ahadi kipaumbele kuhusu ajira kwa vijana na uundwaji wa Baraza la Taifa la Vijana kama ilivyoniahidi bungeni mwaka 2011 na nyingine kuzirejea bungeni mwaka 2012.

Kuhusu masuala ya ajira, tulipendekeza bungeni na Wizara ikakubaliana nasi kuanzisha Benki ya Taifa ya Vijana ili kuwezesha vijana wasioweza kumudu masharti ya kibenki katika mfumo wa kawaida wa kibenki kuweza kupata mitaji kwa masharti nafuu kwa ajili ya kujiajiri. Aidha, tulipendekeza na Wizara ikakubali kushirikiana na Wizara zingine ili kuwe na mfumo wa kuwezesha wahitimu wa vyuo kutumia vyeti vyao kama dhamana kuweza kukopa katika mabenki kwa ajili ya kujiajiri.

Kuhusu uundwaji wa Baraza la Taifa la Maendeleo ya Vijana, serikali iliahidi kwamba mchakato wa kuundwa kwa baraza hilo ungekamilika katika mwaka wa fedha 2011/2012, hata hivyo mpaka kipindi hicho kinamalizika mwezi Juni 2012 na kuanza kwa mwaka mwingine wa fedha 2012/2013 ahadi hiyo haijatekelezwa. Baraza la Taifa la Maendeleo ya Vijana likianzishwa litaweza kuwaunganisha vijana bila kujali tofauti zao zingine katika kushughulikia vipaumbele mbalimbali vya vijana ikiwemo katika masuala ya elimu, ajira, afya, michezo na maisha ya vijana kwa ujumla.

Imetolewa tarehe 5 Oktoba 2012 na:

John Mnyika (Mb)
Kijana wa Tanzania

No comments: