Thursday, January 3, 2013

Hatua kuhusu matumizi ya dola milioni 164.6 za “mabomba ya mchina” na mikataba ya miradi ya sasa ya maji jijini Dar es salaam

Tarehe 3 Januari 2013 kwa kutumia kifungu cha 10 cha sheria ya haki, kinga na madaraka ya Bunge nimetaka Wizara ya Maji inipatie nakala ya ripoti ya utekelezaji wa mradi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya Majisafi na Majitaka Jijini Dar es salaam na maeneo ya Bagamoyo na Kibaha (Dar es salaam Water Supply and Sanitation Project-DWSSP) uliotekelezwa kati ya mwaka 2003 mpaka 2010 jijini Dar es salaam.

Nimetaka ripoti hiyo ili kubaini matumizi ya dola milioni 164.6 zinazoelezwa kutumika katika mradi huo maarufu kama wa ‘mabomba ya mchina’ kwa kuwa mpaka sasa mwaka 2013 sehemu kubwa ya mabomba yaliyowekwa wakati wa mradi huo katika Jiji la Dar es salaam hayatoi maji huku kukiwa na upungufu katika uzalishaji, upotevu wakati wa usafirishaji, udhaifu katika usambazaji na tuhuma za ufisadi katika matumizi.

Pamoja na kutaka ripoti ya utekelezaji wa mradi huo, nimetaka pia nakala ya ripoti ya ukaguzi wa kiufundi (technical Audit) uliofanywa na kampuni ya Howard Humphreys kuhusu mradi huo.

Nimetaka pia kupatiwa ripoti za ukaguzi uliofanywa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa Kampuni ya Maji Dar es salaam- DAWASCO (Dar es salaam Water Supply and Sewerage Company) na Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka-DAWASA (Dar es Salaam Water Supply and Sewerage Authority) kwa mwaka miaka mitatu ya 2009/10, 2010/2011, 2011/2012 ili kuweza kufuatilia hatua zinazostahili kuchukuliwa.


Aidha kwa kutumia kifungu hicho hicho cha 10 cha sheria ya haki, kinga na madaraka ya Bunge, katika barua yangu kwa katibu wa Bunge niliyoiwasilisha leo tarehe 3 Januari 2013 nimetaka kupatiwa nakala za mikataba yote ya miradi inayotekelezwa hivi sasa ya maji katika Jiji la Dar es Salaam ili kuendelea kufanya kazi ya kibunge ya kuishauri na kuisimamia serikali kueupusha kasoro zilizojitokeza katika miradi ya miaka iliyopita kujirudia hivi sasa.

Kati ya mikataba niliyotaka kupatiwa ni ile ya miradi ya miundombinu inayoendelea kujengwa na mikopo iliyopatikana kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu huyo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Maalum wa Maji Dar es salaam 2011-2013 ambao uliwasilishwa katika Baraza la Mawaziri mwezi Machi 2011 na kuridhiwa kutekelezwa ukihitaji jumla ya shilingi bilioni 653.85; ambao utekelezaji wake unasuasua.

Izingatiwe kwamba Jiji la Dar es salaam lina adha ya maji ya muda mrefu ambayo kila mkazi wa jiji hili ana wajibu wa kuhakikisha inapatiwa ufumbuzi hivyo mwaka 2013 utumike kuongeza msukumo wa uwajibikaji katika sekta ya maji ambayo ni muhimu kwa uchumi wa nchi na maisha ya wananchi.

Pamoja na kuwa matokeo ya sensa ya mwaka 2012 kiwilaya na kimikoa bado hayajatangazwa, Jiji la Dar es salaam linakadiriwa kuwa na wakazi zaidi ya milioni nne; hivyo ni sawa na takribani asilimia kumi ya watanzania wote milioni 44.9 waliotangazwa.

Upatikanaji wa maji katika Jiji la Dar es salaam miaka michache baada mwaka 1961 ulikuwa zaidi ya asilimia 68; hivi sasa miaka 51 baada ya uhuru tumerudi nyuma na upatikanaji ni kwa wastani asilimia 55 tu tena kwa mgawo.

Pamoja na kero ya mgawo wa maji hali hii imesababisha ongezeko kubwa la bei ya maji kwa wananchi wa kipato cha chini wanaotegemea kupata maji kutoka sekta binafsi ambapo wanaonunua maji kwa madumu hununua bei ambayo ni takribani mara 15 ya bei ya mteja anayepata huduma ya maji ya bomba.

Hali ni mbaya zaidi kuhusu uondoaji wa maji taka ambapo ni chini ya asilimia 10 tu ya makazi ndiyo yaliyounganishwa katika mtandao wa maji taka na hivyo kuleta uchafuzi wa mazingira hususani katika maeneo yasiyopimwa. Hata katika maeneo yaliyopimwa Jijini Dar es salaam mitandao ya maji taka haijakarabatiwa na kupanuliwa kwa wakati kwa kuzingatia ongezeko la watu suala ambalo lisipochuliwa kwa uzito unaostahili madhara yatatokea katika siku za usoni.

Hatua za haraka za kuboresha upatikanaji wa maji safi na uondoaji wa maji taka zinapaswa kuchukuliwa kuhusu hali hii kwa kuzingatia kuwa idadi ya watu katika Jiji la Dar es salaam inaendelea kukua kwa kasi likiwa ni jiji la tatu kwa ongezeko kubwa la watu barani Afrika na la tisa duniani.

Kwa nyakati mbalimbali katika kipindi cha kati ya mwaka 2000 mpaka 2010 Serikali imekuwa ikitoa ahadi za kumaliza tatizo la majisafi na majitaka katika Jiji la Dar es Salaam bila utekelezaji sahihi, kamili na wa haraka; hivyo uamuzi wa kutumia sheria ya haki, kinga na madaraka ya Bunge na kazi zingine za kibunge nitakazozifanya mwaka huu wa 2013 zitaongeza uwajibikaji katika sekta ya maji kwa manufaa ya wananchi na nchi kwa ujumla.

Imetolewa mtandaoni tarehe 4 Januari 2013 na:

John Mnyika (Mb)
Jimbo la Ubungo

No comments: