Friday, January 18, 2013

Rais na Mawaziri wanadharau wabunge kuhusu mabadiliko ya mzunguko wa Bajeti

Yaliyojiri na yanayoendelea kujiri ndani ya Baraza la Mawaziri na Wizara ya Fedha kuhusu mabadiliko ya mzunguko na mchakato wa bajeti yanaashiria kwamba Rais na Serikali wanadharau mamlaka na madaraka ya Bunge na wabunge.

Aidha, kutokana na umuhimu wa mzunguko na mchakato wa bajeti katika kuwezesha uwajibikaji kwenye mapato na matumizi ya rasilimali za umma; Waziri wa Fedha anatakiwa aweke wazi kwa umma mabadiliko hayo yaliyofanyika ili wananchi na wadau waweze kutoa maoni na Bunge liweze kuyazingatia wakati wa marekebisho ya kanuni za Bunge yanayotarajiwa kufanywa katika mkutano wa kumi wa Bunge.

Wakati Katibu wa Bunge amenukuliwa tarehe 17 Januari 2013 akisema kwamba pendekezo la mabadiliko ya mzunguko na mchakato wa bajeti bado linajadiliwa na kwamba iwapo litaafikiwa, uamuzi utatangazwa mapema mwezi ujao (Februari 2013) wakati wa mkutano wa Bunge; upande wa Rais na Wizara ya Fedha wameshapitisha na kuanza kutekeleza mzunguko na mchakato mpya wa bajeti kuanzia mwezi Disemba 2012.

Kwa upande wangu nitashiriki vikao vya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Fedha na Uchumi wiki ijayo ili nipate mwanya wa kumhoji Waziri wa Fedha kwa kurejea matakwa ya Katiba ya Nchi, Sheria ya Fedha za Umma, Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sheria ya Ununuzi, Sheria ya Ukaguzi na kanuni zinazoongoza mzunguko na mchakato wa bajeti nchini.

Rais na Serikali wamepitisha na kuanza kutekeleza mzunguko na mchakato huo mpya wa bajeti bila kujali kwamba suala hilo; pamoja na kanuni za ndani ya Serikali linatawaliwa zaidi na Kanuni za Kudumu za Bunge (Kanuni ya 77 mpaka 82) ambazo hazijafanyiwa marekebisho mpaka sasa.

Tafsiri ya uamuzi huo wa Rais na Serikali wa kuanza kutekeleza mzunguko na mchakato mpya wa bajeti bila kanuni za Bunge kufanyiwa marekebisho ni kwamba Rais na Serikali wanahakika kwamba marekebisho hayo yatafanyika kama serikali ilivyopitisha kwa upande wake; huku ni kulifanya bunge na wabunge kuwa mihuri ya kupitisha tu yaliyopangwa na Serikali (Rubber Stamps).

Rais akiongoza Baraza la Mawaziri wamepitisha na kuanza kutekeleza uamuzi wa kwamba sasa mipango na bajeti ya nchi itajadiliwa na kuidhinishwa na Bunge ya mwisho wa mwaka wa fedha mwishoni mwa mwezi Juni.

Wizara ya Fedha baada ya kupitishwa kwa uamuzi huo imeshaanza kuutekeleza kabla ya marekebisho ya kanuni na tayari imeshatoa miongozo kwa Wizara, Idara na Mamlaka zinazojitegemea, Sekretariati za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuwasilisha makadirio ya bajeti zao mwezi Machi.

Tayari Serikali imeshapanga kwamba Kamati za Kudumu za Kisekta za Bunge zitafanya vikao vya kupitia bajeti mwezi Aprili na hatimaye bajeti za wizara zote kujadiliwa na bajeti ya ujumla kupitishwa ifikapo tarehe 30 Juni 2013; maamuzi hayo yamefanywa na Rais na Baraza la Mawaziri wakati ambapo ratiba za mikutano na vikao vya Bunge hupangwa na Bunge.

Natambua kwamba kwa nyakati mbalimbali wabunge tumetaka marekebisho ya kanuni za Bunge ikiwemo kuhusu mzunguko na mchakato wa bajeti; hata hivyo, Serikali haina madaraka na mamlaka kufanya maamuzi na kuanza kutekeleza mabadiliko hayo bila Bunge kuridhia.

Natoa mwito kwa kila mmoja wetu kutimiza wajibu wa kiraia kudhibiti hali hii kwa kuwa ushiriki wa kibunge kwenye mzunguko na mchakato wa bajeti kuanzia usimamizi wa maandalizi, upitishaji na ufuatiliaji wa utekelezaji ni suala muhimu katika kuhakikisha uwajibikaji kwa maendeleo ya nchi.

Wenu katika uwakilishi wa wananchi,


John Mnyika (Mb)
19/01/2013

No comments: