Thursday, January 24, 2013

Nimemwandikia Spika Bunge liwezeshe ufumbuzi wa mgogoro wa gesi asilia

BUNGE LIINGILIE KATI KUWEZESHA UFUMBUZI WA MGOGORO WA GESI MTWARA. SPIKA ATUMIE MAMLAKA YAKE KUELEKEZA KAMATI ITAYOKUTANISHA SERIKALI NA WANANCHI. RAIS NA SERIKALI WAJISAHIHISHE NA KUONDOA UDHAIFU BADALA YA KUENDELEA KULAUMU NA KUPOTOSHA 

Nimemwandikia barua Spika atumie mamlaka na madaraka yake kutoa nafasi Bunge liingilie kati kuwezesha ufumbuzi wa mgogoro unaoendelea kati ya Serikali na wananchi kuhusu utafutaji, uvunaji, usafirishaji na utumiaji wa gesi asilia kutoka Mtwara.

Katika hatua ya sasa Serikali ni kupitia Wizara ya Nishati na Madini na taasisi zake ni sehemu ya watuhumiwa na washutumiwa hivyo ni muhimu majadiliano kati ya Serikali na wananchi kuwezesha ufumbuzi wa mgogoro huo yakasimamiwa na muhimili mwingine kwa dola.

Rais naye tayari ameshachukua upande bila kusikiliza kwa kina na kuyaelewa madai ya wananchi hivyo katika hali ya sasa ni muhimu kurejea katika madaraka na mamlaka ya wabunge kwa mujibu wa katiba ya nchi kuwezesha ufumbuzi wa mgogoro huu kuepusha hali tete inayoweza kuzuka na kuathiri uchumi na usalama katika maeneo husika.

Katiba ya Nchi Ibara ya 63 (2) inaelekeza kwamba sehemu ya pili ya Bunge (inayoundwa na wabunge) itakuwa ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano ambacho kitakuwa na madaraka, kwa niaba ya wananchi kuisimamia na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa katiba.


Ili kuliwezesha Bunge kutumia mamlaka na madaraka hayo katika Mkutano wa Kumi wa Bunge unaotarajia kuanza mwishoni mwa mwezi huu wa Januari 2013 katika kipindi hiki ambacho Nchi haina Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, nimemwandikia barua Spika atumie mamlaka na madaraka yake mujibu wa Kanuni ya 116 na Kanuni ya 114 fasili ya 14 ya Kanuni za Kudumu za Bunge kuelekeza mgogoro huu ushughulikiwe na Kamati mojawapo ya kudumu za Bunge wakati wa vikao vinavyoendelea hivi sasa Dar es salaam na vitavyofanyika Dodoma ili pande zote mbili; serikali na wananchi ziweze kuitwa kueleza madai na maelezo yake ufumbuzi wa haraka uweze kupatikana.

Itakumbukwa kwamba katika Mkutano wa Nane wa Bunge Spika alitangaza kuwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imevunjwa na kwamba majukumu yaliyokuwa yakishughulikiwa na kamati hiyo yatashughulikiwa na kamati nyingine kwa mujibu wa madaraka na mamlaka ya Spika; hata hivyo mpaka sasa Spika hajatimiza wajibu huo hali ambayo imeacha ombwe la usimamizi katika kipindi hiki chenye migogoro mingi katika sekta za nishati na madini.

Mgogoro kati ya Serikali na wananchi kuhusu utafutaji, uvunaji, usafirishaji na utumiaji wa gesi asilia kutoka Mtwara usingefikia kiwango cha sasa iwapo Spika angetekeleza mapendekezo niliyoyatoa kwa nyakati mbalimbali kuanzia mwezi Oktoba mwaka 2012 wa kutaka kuzibwa kwa ombwe la usimamizi kutokana na utekelezaji wa miradi kuendelea bila kuwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ambayo ingepaswa kuishauri na kuisimamia Serikali.

Irejewe kwamba nilimwandikia barua Spika mwezi Oktoba mwaka 2012 kumkumbusha kutumia madaraka hayo lakini mpaka sasa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa wala barua kujibiwa; hivyo kwa kuwa mgogoro umezidi kuongezeka na kuanza kuleta athari naamini barua nitayomuandikia sasa ataifanyia kazi kwa haraka.

Izingatiwe kwamba katika barua hiyo nilitoa mwito kwa Spika atumie madaraka na mamlaka yake kutangaza kwa umma kamati nyingine ya kudumu ya Bunge itayoshughulikia nishati na madini ikiwemo masuala ya gesi asili kwa sasa kufuatia hali tete na tata kuhusu sekta ndogo ya gesi asilia nchini na kwa kuzingatia umuhimu na unyeti wa sekta hiyo katika uchumi wa nchi na maisha ya wananchi.

Pamoja na mambo mengine nilipendekeza Spika aelekeze kamati hiyo kupokea na kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge ya mwaka 2011 kuhusu Sekta Ndogo ya Gesi Asili ikiwemo juu ya hatua iliyofikiwa katika kushughulikia tuhuma za ufisadi, madai ya mapunjo ya fedha za mauzo ya Gesi asili na hatua iliyofikiwa katika maandalizi ya sera, mpango mkakati, sheria ya gesi asili na utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya gesi ikiwemo ujenzi wa bomba.

Itakumbukwa kwamba siku moja kabla ya maandamano ya wananchi wa Mtwara yaliyofanyika tarehe 27 Disemba 2012, nilieleza kusudio langu la kutumia kifungu cha 10 cha Sheria
ya ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge kutaka nakala ya mkataba wa mkopo wa masharti kiasi cha Dola za Marekani bilioni 1.225 (shilingi trilioni 1.86) kutoka China. Pia nilitaka nakala za mikataba wa mradi wa miundombinu ya gesi asilia ambayo itahusisha ujenzi wa mitambo ya kusafishia gesi asilia katika mikoa ya Lindi na Mtwara na ujenzi wa bomba kuu la kusafirishia gesi asilia la inchi 36 kutoka Mtwara kupitia Lindi, Pwani hadi Dar es Salaam lenye umbali wa kilometa 532.

Nilieleza kusudio la kuchukua hatua hiyo kwa sababu mpaka sasa Wizara ya Nishati na Madini haijatekeleza pendekezo nililowasilisha bungeni tarehe 27 Julai 2012 kwamba kutokana na unyeti wa mradi huo kwa mustakabali wa nchi na maisha ya wananchi wa sasa na baadaye Serikali ilipaswa kuwasilisha bungeni na kuweka wazi kwa umma mkataba wa mradi husika.

Pendekezo hilo lingetekelezwa toka wakati huo lingeepusha maandamano na mgogoro kwa kuwa majadiliano yangefanyika kuanzia bungeni na Bunge kuishauri na kuisimamia serikali kuanzia katika hatua za awali kuhakikisha kwamba maslahi ya taifa yanalindwa katika hatua zote na pia wananchi wakiwemo wa Mtwara wananufaika kutokana na fursa za uwekezaji huo mkubwa.

Ifahamike kwamba Tarehe 27 Julai 2012 nilieleza bungeni kuwa pamoja na ujenzi wa mitambo miwili ya kusafishia gesi asili Mnazi Bay na Songo Songo kama sehemu ya mradi wa ujenzi wa Bomba la Gesi; niliitaka Serikali kueleza ni miradi ipi inayoambatana na mradi huo ambayo imepangwa kuwanufaisha wananchi wa mikoa ya Lindi na Mtwara ikiwemo kuharakisha utekelezaji wa mradi wa kuzalisha umeme wa MW 300 Mtwara na MW 230 wa Somanga Fungu (Kilwa); hata hivyo Serikali haikutoa ufafanuzi wa kuridhisha bungeni.

Kwa mantiki hiyo badala ya Rais na Serikali kulaumu na kupotosha ni muhimu yeye na serikali wakajisahihisha kwa udhaifu ulioonyeshwa wakati wa maandalizi ya mikataba ya miradi husika bila kuzihusisha kamati za kisekta za Bunge kuanzia mwaka 2011 na wakati wa uzinduzi wa mradi tarehe 8 Novemba 2012 Mkoani Dar es salaam wa kuendeleza usiri; hali ambayo imechangia katika migogoro inayoendelea inayohitaji wabunge na bunge kuingilia kati kuwezesha ufumbuzi wa haraka.

Wenu katika uwakilishi wa wananchi,

John Mnyika (Mb)
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini
24 Januari, 2013

3 comments:

Anonymous said...

muheshimiwa mbunge pole kwanza kwa jukumu kubwa taifa lililokupa la kutetea haki za raia,
bado wananchi wa Goba tunalia na swala la maji na umeme ingawa maji tunaona ni gumu lakini tunapata kwa watu wanaouza na magari haina shida sana tumeshazoea.
Umeme muheshimiwa ndio kimbembe na tumeshachanga michango iko tangu desemba lakini tanesco bado hawatuletei umeme, hili ni tatizo kutokana na kwamba hata shughuli za kiuchumi ni vigumu kuendesha, achilia mbali hilo vitendo vya wizi vimekithiri kutokana na giza, watoto wanasomea vibatari which s not good kwa macho yao, plz chadema tunajua ni watenda kazi na mtatusaidia juu ya hili, na wananchi wa Goba tutawapa kura zetu, CHADEMA OYEEE!

Anonymous said...

Nadhani wanachokitaka watu wa Mtwara kitafaidisha wajanja wachache. CHADEMA na kambi nzima ya upinzani kuweni makini maana wakubwa/wajanja wameshashika maeneo tayari kujenga vitega uchumi au kuuzia wawekezaji. Mwananchi wa kawaida atafaidi vipi gesi hiyo? Je ni kwa kuajiriwa kuwa kibarua,houseboy/girl kwa wakubwa hawa?
Maendeleo ya viwanda yanakuja na tabia za ajabu ambazo mtwara hawajawahi kuona n.k.
MIMI NINGESGAURI CHADEMA/UINZANI WASIMAMIE MSIMAMO KUWA UUNDWE MFUKO(FUND) UTAKAOGHARIMIWA NA PERCENT YA MAPATO YA GESI KA KAZI YAKE KUBWA IWE NI MIUNDOMBINU YA HUDUMA ZA JAMII KAMA BARABARA/MAJI/SHULE/ZAHANATI NA HATA IKIBIDI SCHOLARSHIPS KWA WATOTO WENYE KIPAJI LAKINI WAZAZI HAWANA UWEZO. Mssingie kwenye mtego huu wa viwanda bila kujua ni ajira ngapi zitawanufaisha watu wa mtuwara kwa ukweli. Viwanda vitajengwa na malalamiko yatakuwa mbona hatupati kazi.

Unknown said...

tatiz langu ni huu usili mkubwa wa mikataba ya gesi na vitu vingine vinavyohusika moja kwa moja maisha ya watz wote, ila lai yangu ni kwamba wanachoongea wanamtwara siyo majibu wanayos ccm selikari yao,, kwa hili la gesi naomba viongozi wasikulupuke kama kwamba wanaenda kipiga miswaki meno yao yao,,