Monday, March 25, 2013

Mnyika na harakati za kuhakikisha Maji ndani ya Jimbo la Ubungo

21 Machi, 2013 Mnyika aitwa Ikulu, JK awakumbuka Mabwepande
na Asha Bani

HOJA ya Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA) kuhusiana na suala la tatizo la upatikanaji wa maji katika Mkoa wa Dar es Salaam, inaelekea kupata ufumbuzi kutokana na Rais Jakaya Kikwete kumuita Ikulu mbunge huyo Jumatatu wiki ijayo.

Wengine walioitwa kukutana na rais ni Mkuu wa Mkoa, Mecky Sadick, wakuu wote wa wilaya pamoja na wabunge na wataalamu kutoka Wizara ya Maji.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam katika uzinduzi wa daraja la Mtaa wa Golani, Kata ya Saranga, Rais Kikwete alisema kuwa kutokana na wananchi wa kata hiyo kupiga kelele kuhusiana na suala la maji ameamua kukutana na viongozi hao ili kupatiwa ufumbuzi.


Kikwete pia alitaka kuwepo na mfumo maalumu wa mabomba ya maji yatakayojengwa kwa saruji kutoka Ruvu Chini na kuja jijini Dar es Salaam moja kwa moja bila kuchepuliwa sehemu yeyote.

Katika hatua nyingine, Rais Kikwete alikiri kuwepo kwa wizi wa maji katika maeneo ambayo mabomba ya maji yamepita.

“Watu wasifanye ukanjanja katika masuala ya maji, mabomba yanatandazwa na watu wanaiba maji, shida inayotokea ni maji hayo kutokufika jijini Dar es Salaam,” alisema.

Alifafanua kuwa lita milioni 65 zinahitajika ili kukabiliana na tatizo la maji na kwamba upanuzi wa Ruvu Juu na Chini ujenzi wake utakamilika Julai na kutaka hatua za haraka kuchukuliwa kuhakikisha maji yanapatikana kwa haraka ili kumaliza tatizo.

Hatua ya Mnyika kuitwa Ikulu imetokana na kusimama kidete katika suala la maji ambapo Aprili 4, mwaka huu aliwasilisha hoja binafsi na kuitaka serikali kuchukua hatua za haraka za kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jiji la Dar es Salaam hoja ambayo ili iliondolewa bungeni kibabe.

Wakati huo huo, Rais Kikwete amemaliza kilio cha muda mrefu kwa wakazi 604 wa mji mpya Mabwepande Manispaa ya Kinondoni kwa kumpa kila mmoja mifuko 100 ya saruji itakayogharimu sh milioni 840.

Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Home Shopping Center (HSC), Ghalib Mohamed, aliahidi kutoa mabati 30 kwa kila mkazi ili waondokane na kuishi kwenye mahema yaliyotoboka.

Rais alikuwa katika mwendelezo wa ziara yeka mkoani hapa kukagua shughuli za maendeleo ambapo pia alifungua shule ya msingi, kituo cha polisi, nyumba za walimu na polisi vilivyojengwa kwa ushirikiano wa Kampuni za HSC na TSN katika mji.

Wakazi hao ni wale ambao nyumba na mali zao zilizolewa na mafuriko mwaka 2011.

Rais alisema serikali imeamua kufanya hivyo baada ya kutembelea mahema ambayo wanaishi kwa sasa na kubaini kuwa yametoboka na kwamba wakati wa mvua wamekuwa wakiishi kwa taabu.

Alisema fedha hizo leo zitakuwa zimefika kwa mkuu wa mkoa ili waweze kununuliwa saruji hiyo ambapo pia wakazi 21 kati yao walikabidhiwa hati za makazi na rais huku akiagiza hati nyingine ziweze kukamilika haraka iwezekanavyo.

Naye Mkurugenzi wa HSC, alisema kupitia sera ya kampuni yao watatumia sehemu ya faida kuwasaidia wananchi mbalimbali waliokumbwa na matatizo kwani ni vema kugawana na wasio nacho.

Chanzo: http://www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=46963 

No comments: