Thursday, March 21, 2013

MNYIKA ATAKA KAULI YA RAIS KIKWETE KUHUSU UJENZI WA MACHINGA COMPLEX NA JUMBA LA VIWANDA VIDOGO JIMBONI UBUNGO

Mbunge wa Jimbo la Ubungo John Mnyika ametoa mwito kwa Rais Jakaya Kikwete kueleza sababu za kutokutekelezwa mpaka sasa kwa ahadi zake alizotoa mwaka 2010 za ujenzi wa Machinga Complex na jumba la viwanda vidogo katika jimbo hilo kuchangia katika kupanua wigo wa ajira kwa vijana. 

Mnyika aliyasema hayo akijibu swali la mwakilishi wa vijana katika mkutano wake na wananchi alioufanya katika ofisi za Serikali ya Mtaa wa Muungano katika kata ya Manzese uliofanyika mwishoni mwa wiki (16/03/2013). 

Mwakilishi huyo wa vijana alitaka kufahamu hatua ambazo mbunge amechukua kufuatilia kuhusu maeneo ya kufanyia biashara kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo katika jimbo la Ubungo. 

“Kazi ya mbunge ni kuwawakilisha wananchi na kuisimamia serikali ili kuwezesha utatuzi wa kero, matatizo ya maeneo ya wafanyabiashara ndogo ndogo yamedumu kwa muda mrefu kutokana na udhaifu katika mipango miji na hivyo maeneo ya wafanyabiashara na masoko kuuzwa, kuvamiwa au kuwa machache. Nimefuatilia suala hili, kuna ambao wamepata maeneo na wengine wengi bado”, alijibu Mnyika.

Mbunge alieleza kuwa katika mwaka 2011/2012 alikutana na ‘wamachinga’ wa jimbo la Ubungo hatua iliyosababisha kamati maalum inayohusisha wafanyabiashara na Manispaa kuundwa kwa ajili ya kuwezesha wafanyabiashara wa Ubungo kupatiwa maeneo katika masoko yaliyotengwa. Mnyika alisema kwamba atashirikiana na madiwani mwaka huu wa 2013 kutathmini kazi iliyofanywa na kamati hiyo ili kuweza kuchukua hatua ziada. 

Mnyika alieleza kuwa pamoja na hatua hizo za mbunge na manispaa, Rais Kikwete naye anawajibu wa kueleza sababu za Serikali kutokutekeleza mpaka sasa ahadi ya ujenzi wa Machinga Complex katika Jimbo la Ubungo katika eneo la Mbezi Luis. 

“Tofauti na ahadi nyingine ambazo utetezi unaweza kuwa miaka mitano ya utekelezaji bado, suala la ujenzi wa Machinga Complex lilipaswa kutekelezwa na kukamilika ndani ya miaka miwili kwa kuwa Rais Kikwete wakati akihutubia hapa hapa Manzese kwenye uchaguzi wa mwaka 2010 alisema fedha za mkopo toka China zipo toka wakati huo”, alikumbusha mbunge. 

Itakumbukwa kwamba akihutubia mkutano wa kampeni tarehe 17 Oktoba 2010 kwenye eneo la Bakheresa Rais Kikwete alisema kwamba pamoja na ujenzi wa Machinga Complex ya Jiji Ilala kutajengwa Machinga Complex nyingine katika Manispaa zingine za Mkoa wa Dar es salaam zenye kuweza kuchukua jumla ya wafanyabiashara ndogo ndogo 40,000. 

Kwa upande mwingine, Mnyika aliwaeleza wananchi kwamba ujenzi wa Machinga Complex pekee hauwezi kuwa ufumbuzi wa matatizo ya ajira kwa vijana hivyo ni muhimu kuhusisha mikakati mingine yenye kuongeza uzalishaji mijini na vijijini unaombana na ongezeko la ajira na ujira bora. 

“Tanzania haiwezi kuwa taifa la wachuuzi, tunapaswa kuwa nchi ya wazalishaji zaidi ili kuinua uchumi wa nchi na kuboresha maisha ya wananchi. Hivyo, yanahitajika maeneo mengi ya uzalishaji sio kwa ajili ya wakulima bali pia kwa ajili ya viwanda vidogo kwenye kutoa ajira kwa wengi na kwa wingi”, alisisitiza Mnyika.

Mbunge alieleza kwamba ili kutekeleza azma hiyo amewawakilisha wananchi na kuisimamia Serikali bungeni mwaka 2012 kupitia michango na maswali kuhusu viwanda vilivyobinafsishwa au kuuzwa miaka ya nyuma katika Jimbo la Ubungo mathalani Ubungo Garments; Ubungo Spinning Mill; Polysacks Ltd; Tanzania Sewing Thread; Coastal Diaries (Maziwa) na Kiwanda cha Zana za Kilimo (UFI); na hatimaye serikali ilimjibu kuwa waraka utawasilishwa kwenye baraza la mawaziri ili kurejesha viwanda vilivyodidimizwa kinyume cha masharti ya mikataba. 

Kufuatia majibu yao mbunge alipendekeza bungeni kuwa miongoni mwa maeneo ya viwanda yatakayorejeshwa kutengwe eneo maalum kwa ajili ya wenye viwanda vidogo vidogo katika jimbo la Ubungo ili kupanua wigo wa ajira hususan kwa vijana.

“Ninakwenda bungeni mwezi ujao, iwapo mpaka wakati huo Rais Kikwete atakuwa hajaeleza sababu za ahadi ya Machinga Complex na kufuatilia waraka huo kuhusu viwanda vilivyobinafishwa kwa kuwa yeye ndiye mwenyekiti wa baraza la mawaziri; nitawawakilisha kwa hatua zaidi ambazo nyinyi wananchi mtaona zinafaa”, aliahidi mbunge. 

Mnyika alisema kwamba pamoja na haja ya kupata maeneo hayo ambayo vijana wenyewe kupitia mitaji yao midogo midogo wataweza kuwekeza katika viwanda vidogo vidogo, lipo eneo ambalo hilo Serikali inaweza kuwekeza kwa mkopo kujenga jengo ili kuweza kutumiwa na vijana wengi zaidi katika Jimbo la Ubungo na Jiji la Dar es salaam kwa ujumla. 

“Rais akumbuke kwamba toka mwaka 2010 Serikali iliahidi kujenga jumba la viwanda vidogo vidogo katika eneo lililokuwa mali ya TTCL Barabara la Sam Nujoma, ni muhimu akatoa kauli kabla ya mkutano wa bunge kuanza kuwa bilioni 100 za mkopo toka China kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo la viwanda vidogo na majengo mengine ya wafanyabiashara ndogo ndogo zimeishia wapi?”, alihoji Mnyika. 

Imetolewa tarehe 19 Machi 2013 na: 

Aziz Himbuka
Katibu Msaidizi
Ofisi ya Mbunge

No comments: