Monday, March 25, 2013

Mwaliko wa kushiriki ufuatiliaji wa mradi wa maji na mkutano wa mbunge na wananchi katika kilele cha wiki ya maji kitaifa na siku ya maji kimataifa leo tarehe 22 Machi Mtaa wa Makoka kata ya Makuburi.

Leo tarehe 22 Machi ni kilele cha wiki ya maji kitaifa na siku ya kimataifa ya maji. Katika kazi zake ikiwa ni sehemu ya siku hiyo Mbunge wa Ubungo John Mnyika saa 9 alasiri atakuwepo eneo la Uluguruni Mtaa wa Makoka Kata ya Makuburi kufanya ufuatiliaji wa mradi wa maji.

Mradi umetekelezwa kwa ushirikiano na Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASCO) baada ya kuchochewa kwa kuchangiwa milioni kumi na Mfuko wa Maendeleo (CDCF) Jimbo la Ubungo ambao Mnyika ni mwenyekiti wake pamoja na kuunganisha nguvu za wananchi katika maeneo husika.

Aidha, baada ya kukagua mradi huo kuanzia saa 10 Jioni mbunge atafanya mkutano na wananchi kwa ajili ya kutoa ujumbe kuhusu hatua za haraka za kuboresha upatikanaji wa majisafi na ushughulikiaji wa majitaka katika Jiji la Dar Es Salaam zinazopaswa kuchukuliwa hata baada ya wiki ya maji.

Pia kufuatia mwaliko wa Rais Jakaya Kikwete wakukutana tarehe 25 Machi 2013 na Mkuu wa Mkoa, DAWASA, DAWASCO, Mnyika na wabunge wengine wa Mkoa wa Dar es Salaam kujadili hatua za haraka za kuboresha upatikanaji wa maji, mbunge atatumia mkutano wake na wananchi kusikiliza maoni na mapendekezo kuhusu hatua za ziada zinazopaswa kuchukuliwa.

Imetolewa tarehe 22 Machi 2013 na: 

Gaston Shundo 

Afisa katika Ofisi ya Mbunge Ubungo

No comments: