Saturday, March 2, 2013

WANANCHI OMBENI UJUMBE WA MABARAZA YA KATIBA LAKINI PINGENI ‘MIANYA YA UCHAKACHUAJI’ WA UTEUZI KWENYE KATA ILIYOWEKWA NA MUONGOZO ULIOTOLEWA NA TUME YA MABADILIKO YA KATIBA BILA KUZINGATIA MAONI YA WADAU

Mwongozo kuhusu Muundo, Utaratibu wa kuwapata wajumbe wa mabaraza ya Katiba ya Wilaya (Mamlaka za Serikali za Mitaa) na uendeshaji wake uliotangazwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba haujazingatia maoni ya msingi yaliyotolewa na wadau mbalimbali ikiwemo Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). 

CHADEMA inawatahadharisha wananchi kuhusu ‘mianya ya uchakachuaji’ iliyotolewa na muongozo huo kwa kuzingatia kuwa ‘uchakachuaji’ wa uteuzi wa wajumbe wa mabaraza ya katiba, ni ‘uchakachuaji’ wa utoaji maoni kwenye mabaraza ya katiba, ambayo ni hatua ya awali ya ‘uchakachuaji’ wa rasimu ya katiba. 

Kwa mujibu wa Muongozo huo, ‘mianya ya uchakachuaji’ imeachwa kwenye ngazi ya kamati ya maendeleo ya kata ambayo wajumbe wake ni madiwani na wenyeviti wa mitaa/vijiji ambao kwa mujibu wa matokeo ya chaguzi za mwaka 2009 na 2010 kuna hodhi kwenye vikao hivyo ya chama kimoja (CCM).

Lakini bila kuzingatia hali hiyo, Tume ya Mabadiliko ya katiba kupitia muongozo huo imewapa mamlaka ya kuchagua wajumbe wa mabaraza ya katiba katika kila kata kwa upande wa Tanzania Bara. 

Muongozo huo ‘umeminya’ mamlaka ya wananchi wote kupitia mikutano yao ya vijiji na mitaa kwa upande wa Tanzania Bara kuwa ni ‘kupendekeza’ tu majina badala ya kuchagua. 

Hata hivyo, muongozo huo umetangaza utaratibu tofauti kwa upande wa Zanzibar ambapo wawakilishi wakishaguliwa na wananchi kwenye mkutano wa Shehia majina yao yanawasilishwa moja kwa moja bila kuwa na ‘mianya ya uchakachuaji’ kama ilivyo kwa Tanzania Bara. 

Hivyo, pamoja na kuwahimiza wananchi wakiwemo wanawake na vijana kuomba kwenye ngazi ya kijiji na mitaa kuwa wajumbe kwenye mabaraza hayo ya katiba; CHADEMA inawahimiza pia wananchi na wadau kudai kwamba mara baada ya wananchi kuchagua wawakilishi wao kupitia mikutano mikuu maalum kwenye vijiji na mitaa, wawakilishi hao waingie moja kwa moja kwenye mabaraza ya katiba bila kuchujwa na vikao vinavyotawaliwa na CCM. 

Itakumbukwa kwamba tarehe 14 Februari 2013, CHADEMA kiliwasilisha kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba maoni na mapendekezo ya CHADEMA juu ya muongozo uliotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuhusu muundo, utaratibu wa kuwapata wajumbe wa mabaraza ya katiba ya wilaya (Mamlaka za Serikali za Mitaa) na uendeshaji wake. 

Maoni na mapendekezo yaliyowasilishwa katika nyaraka ya kurasa tisa yalihusu vipengele vyote kumi vya rasimu ya muongozo iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba. 

Katika maoni na mapendekezo hayo, CHADEMA pamoja na mambo mengine hakikubaliana na muundo wa kuwa mabaraza hayo ya wilaya yatakuwa na wawakilishi walioteuliwa na ngazi ya kata; badala yake CHADEMA kilipendekeza kuwa wajumbe wote waliochaguliwa kuwakilisha vijiji au mitaa au shehia waingie moja kwa moja kwenye mabaraza ya wilaya. 

Ikumbukwe kuwa upungufu katika mchakato wa ukusanyaji wa maoni ya wananchi binafsi ilisababisha idadi ndogo ya watu waliotoa maoni ambapo mpaka awamu nne zinakamilika jumla ya watu 318,223 tu ndio waliotoa maoni sawa na asilimia 0.7 ya wananchi wote zaidi ya milioni 44.9. 

CHADEMA kilieleza kuwa muundo na utaratibu huu ni muhimu katika kujenga muafaka wa kitaifa na katika kurekebisha upungufu katika mchakato uliotangazwa kukamiilika wa ukusanyaji wa maoni ya wananchi binafsi uliofanyika kwa awamu nne mwaka 2012 ambapo tume ilifanya mikutano 1776 tu na wananchi wachache kutoa maoni kutokana na sababu mbalimbali. 


Imetolewa tarehe 1 Machi 2013 na: 



John Mnyika (Mb) 
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi

No comments: