Wednesday, March 20, 2013

RUFAA DHIDI AGIZO LA ACP CHARLES KENYELA KAMANDA WA POLISI WA MKOA WA KIPOLISI WA KINONDONI KUZUIA MKUTANO WA HADHARA WA MBUNGE NA WANANCHI TAREHE 16 MACHI 2013Kumb. Na. OMU/US/003/2013                                                                                               18/03/2013 


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
S.L.P 9223, 
Dar es Salaam. 

Mheshimiwa: 


RUFAA DHIDI AGIZO LA ACP CHARLES KENYELA KAMANDA WA POLISI WA MKOA WA KIPOLISI WA KINONDONI KUZUIA MKUTANO WA HADHARA WA MBUNGE NA WANANCHI TAREHE 16 MACHI 2013 


Kwa barua hii nawasilisha rasmi rufaa kwa kutumia kifungu cha 43 (6) cha Sheria ya Jeshi la Polisi na Huduma za Polisi wasaidizi sura ya 322 (The Police Force and Auxilliary Service Act Cap 322 RE 2002) dhidi ya agizo la ACP Charles Kenyela Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni kuzuia mkutano wa hadhara wa mbunge na wananchi tarehe 16 Machi 2013. 

Katika kushughulikia rufaa hii zingatia kuwa tarehe 4 Machi 2013 niliwasilisha taarifa kwake kwa mujibu wa kifungu cha 4 cha Sheria ya Kinga, Madaraka na Haki za Bunge na. 3 ya mwaka 1988 (The Parliamentary Immunities, Powers and Privileges Act) kuwa tarehe 16 Machi 2013 nilipanga kufanya mkutano na wananchi Jimboni. 

Katika taarifa hiyo kupitia barua yangu yenye Kumbu. Na. OMU/US/001/2013 ambayo nilitoa pia nakala kwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Afisa Tawala wa Wilaya ya Kinondoni, Afisa Mtendaji wa Kata ya Manzese na Afisa Mtendaji wa Mtaa wa Muungano, nilieleza kwamba mkutano huo nilipanga kuufanya katika Kata ya Manzese Eneo la Bakheresa kuanzia saa 3 asubuhi mpaka saa 5 Asubuhi. 

Katika taarifa hiyo nilieleza kwamba lengo la mkutano huo ni kuwapa mrejesho wananchi kuhusu masuala niliyoyawasilisha katika Mkutano wa Kumi wa Bunge uliomalizika tarehe 08 Februari 2013 na kupokea mambo ya kuyazingatia kuelekea Mkutano wa Kumi Na Moja wa Bunge unaotarajiwa kuanza tarehe 9 Aprili 2013. 

Hata hivyo, kupitia mkutano wake na vyombo vya habari tarehe 14 Machi 2013 na barua yake iliyoletwa ofisini kwangu tarehe 15 Machi 2013, ACP Charles Kenyela Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni alitoa agizo la kuzuia mkutano wa hadhara wa mbunge na wananchi niliopanga kuufanya tarehe 16 Machi 2013. 

Katika agizo hilo alilolitoa chini ya kifungu cha 43 (2) na 43 (3) Sheria ya Jeshi la Polisi na Huduma za Polisi sababu iliyohusu mkutano kwa mujibu wa barua yake yenye Kumb. Na. DSM/KINONDONI/SO.7/2/CHADEMA/284 ni: 

“Eneo la Manzese Bakhresa ambalo unakusudia kufanyia mkutano siyo eneo halali kwa ajili ya mikutano. Eneo hilo kwa mujibu wa maelekezo ya Manispaa ya Kinondoni kupitia mipango miji ni eneo linalotumika kwa ajili ya kuegesha magari makubwa (malori) na ndio maana liko katika eneo kuu la barabara ya Morogoro ambayo iko katika matengenezo. Kuruhusu mkutano wako kufanyikia hapo ni kukiuka sheria ya mipango miji ya Manispaa ya Kinondoni pamoja na kuingilia shughuli za ujenzi wa barabara unaoendelea hivi sasa na kuwabugudhi watumiaji wengine wa eneo hilo”.


SABABU ZA RUFAA NA MAELEZO YA KUTORIDHIKA: 


Nakata rufaa dhidi ya agizo hilo haramu ambalo limekiuka masharti ya kifungu cha 4 cha Sheria ya Kinga, Madaraka na Haki za Bunge kwa sababu zifuatazo: 

Mosi, Eneo la Manzese Bakheresa limetumika na limeendelea kutumika kufanya mikutano kwa nyakati mbalimbali. Agizo lake kuwa eneo hilo siyo halali kwa ajili ya mikutano linamaanisha kwamba polisi waliruhusu Rais Jakaya Kikwete kinyume cha sheria ya Mipango Miji tarehe 17 Oktoba 2010 alipofanya mkutano katika eneo hilo. Kwa nyakati mbalimbali kati ya mwaka 2005 mpaka 2012 nimefanya mikutano katika eneo hilo lakini hakuna wakati wowote ambao Jeshi la Polisi au mamlaka nyingine yoyote imewahi kutoa amri ya kukataza mikutano kufanyika katika eneo hilo. 

Pili, hakuna uhusiano kati ya kufanya katika eneo ambalo linaendelea kutumika (ikiwemo kwa maegesho ya molori) na kisingizio kilichotolewa kuwa mkutano ungeingilia shughuli za ujenzi wa barabara na kuwabughudhi watumiaji wengine. Ifahamike kuwa hata baada ya kuanza kwa ujenzi wa Barabara ya Morogoro eneo hilo limeendelea kutumika pia kwa mikutano hiyo, kati mikutano hiyo ikiwa ni pamoja na ule uliofanywa na CCM na kuhutubiwa na viongozi wake wa kitaifa tarehe 13 Januari 2013. Aidha, Meya wa Manispaa ya Kinondoni Yusuph Mwenda amenukuliwa kwenye baadhi ya vyombo vya habari tarehe 15 Machi 2013 akieleza kwamba Manispaa ya Kinondoni haijafanya uamuzi huo kwa kuwa bado iko kwenye mashauriano na wadau kuhusu matumizi ya eneo husika. 

Tatu, sababu iliyotolewa haikidhi masharti ya yaliyowekwa na kifungu cha 43 (3) cha Sheria ya Jeshi la Polisi na Huduma za Polisi wasaidizi kwa kuwa Jeshi la Polisi ya kwamba Afisa wa Polisi hatatoa amri ya kusitishwa kwa mkusanyiko kutokana na taarifa iliyotolewa kwake isipokuwa tu kama ameridhika kwamba kufanyika kwa mkusanyiko kuna uwezekano wa kusababisha kuvunjika kwa amani au kuathiri usalama wa taifa au kutumika kwa dhumuni lolote lisilokuwa halali. Ikumbukwe kuwa lengo la mkutano nililieleza wazi kuwa ni kuwapa mrejesho wananchi kuhusu masuala niliyoyawasilisha katika Mkutano wa Kumi wa Bunge uliomalizika tarehe 08 Februari 2013 na kupokea mambo ya kuyazingatia kuelekea Mkutano wa Kumi Na Moja wa Bunge unaotarajiwa kuanza tarehe 9 Aprili 2013. 


MAAMUZI NINAYOOMBA YAFANYWE NA WAZIRI WA MAMBO YA NDANI: 


Waziri wa Mambo ya Ndani kwa kurejea kifungu cha 43 (6) cha Sheria ya Jeshi la Polisi na Huduma za Polisi wasaidizi maelezo hayo ya kutoridhika na amri ya kusimamisha mkutano iliyotolewa na kufanya maamuzi kwamba : 

Mosi, ACP Charles Kenyela Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni alifanya makosa kwa kuzuia mkutano wa hadhara wa mbunge na wananchi wa tarehe 16 Machi 2013 bila sababu za msingi, kinyume na matakwa ya Sheria ya Kinga, Madaraka na Haki za Bunge ambayo inaelekeza kwamba mbunge anao uhuru wa kufanya mikutano ya hadhara katika Jimbo lake na mamlaka zote zinazohusika zinawajibu wa kuwezesha mikutano hiyo kufanyika. 

Pili, ACP Charles Kenyela Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni aadhibiwe kwa makosa hayo ambayo yamewanyima pia wananchi haki za msingi kwa mujibu wa matakwa ya Katiba ya Nchi Ibara za 8, 18, 20 na 21 na yamefanyika kinyume na misingi ya utawala bora. 

Tatu, ACP Charles Kenyela Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni aagizwe kugharamia mkutano mwingine wa Mbunge na wananchi kabla ya tarehe 9 Aprili 2013 ili kufidia gharama zilizotumika kwenye maandalizi ya mkutano aliouzuia uliopaswa kufanyika tarehe 16 Machi 2013. Izingatiwe kwamba taarifa ya mkutano alipatiwa tarehe 4 Machi 2013 na agizo la kuzuia lilifika ofisi kwangu tarehe 15 Machi 2013, siku moja kabla ya mkutano ikiwa tayari fedha za rasilimali zingine za maandalizi ya mkutano ikiwemo katika kufanya matangazo ikiwa zimetumika. Irejewe kwamba kifungu cha 43 (2) cha Sheria ya Jeshi la Polisi na Huduma za Polisi wasaidizi kinaruhusu baada ya kuwasilisha taarifa kuendelea kuitisha na kuandaa mkutano. 

Wako katika uwakilishi wa wananchi, 

John Mnyika (Mb) 

Nakala:
· Spika na Katibu- Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

· Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge)

· Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni

· Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora

· Sekretariati ya Maadili ya Viongozi wa Umma

· Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC)

· Katibu Mkuu na Katibu wa Jimbo- CHADEMA

1 comment:

Anonymous said...

MHESHIMIWA MBUNGE NI KWELI KHAKI NI YAKO KABISA KWA WANANCHI KUFAHAMU ULICHOKIONGEA BUNGENI JUU YAO , NA NIWAJIBU WAO WANANCHI KUKUOJI NINI UMEPANGA KIFANYIKE JUU YA HICHO ULICHOKIONGEA, KAMANDA KIJERA ANAWANYIMA WANANCHI HAKI YAO YA MSINGI PIA HATA YEYE MWENYEWE WEWE SI MBUNGE WAKE HAITAJI MAJI PIA AHANGALIE HILO PIA ASITUMIE SANA UKAMANDA ANAWANYIMA FURSA WANANCHI YA KUKUTANA NA MBUNGE WAO, SIJAFURAHISHWA NA HILO JAMBO BINAFSI.