Wednesday, November 27, 2013

Taarifa kwa umma kuhusu serikali kupandisha bei ya umeme

Gazeti la Tanzania Daima Toleo na. 3280 la tarehe 26 Novemba 23 limenukuu kauli iliyotolewa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini George Simbachawene wakati akizungumza na kipindi cha Kumepampazuka kilichorushwa na Redio One juu ya Serikali kupandisha bei ya umeme kama Shirika la Umeme (TANESCO) lilivyoomba.

Katika habari hiyo Simbachawene amenukuliwa akisema kwamba endapo kuna mwananchi yeyote atakayeona gharama za umeme ni kubwa ni vema akaamua kuwasha kibatari au akae giza. 

Rais Jakaya Kikwete anapaswa kumwagiza Waziri wa Nishati na Madini Prof Sospter Muhongo kuwaomba radhi wananchi kwa kauli hiyo iliyotolewa na Naibu Waziri Simbachawene kwa niaba ya wizara anayoiongoza.

Aidha, ni vyema Rais Kikwete kwenye hotuba yake kwa taifa ya mwisho wa mwezi huu akawaeleza wananchi iwapo uamuzi huo wa kupandisha kwa mara nyingine bei ya umeme ndio utekelezaji wa ahadi ya maisha bora aliyoitoa kwa watanzania kuanzia kwenye uchaguzi wa mwaka 2005.

Hii ni kwa sababu kupandisha bei ya umeme kuna athari ya kuchangia katika ongezeko la gharama na ugumu wa maisha kwa kuwa shughuli za uzalishaji na maisha ya kila siku zinategemea kwa kiwango kikubwa nishati.

Kauli hiyo ya Simbachawene inadhihirisha mtazamo finyu wa kisera kwa Serikali inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) kwamba mahitaji ya nishati ya umeme ni kwa ajili ya kuondoa giza ambapo mbadala wa haraka ni kibatari.

Serikali inayoongozwa na CCM inapaswa kutambua kwamba mbadala wa nishati kwenye uzalishaji, huduma za kijamii na maisha ya kila siku ya wananchi katika karne ya sasa ya sayansi na teknolojia hauwezi kuwa kibatari.

Kwa upande mwingine, umma ni muhimu ukafahamu kwamba uamuzi huu wa Serikali kupandisha bei ya umeme wakati huu ni matokeo ya kutekeleza masharti ya Benki ya Dunia ambayo Serikali ilipewa Washington DC Oktoba 2013 bila kuzingatia hali halisi ya uchumi wa nchi na ustawi wa wananchi.

Aidha, uamuzi huu ni wa kuwabebesha wananchi mzigo wa gharama za muda mrefu za ufisadi katika sekta ya nishati nchini na ubovu wa mikataba inayoendelea kutumika mpaka hivi sasa katika sekta hii nyeti.

Hata hivyo Waziri wa Nishati na Madini Prof Muhongo alisema uongo bungeni kwa nyakati mbalimbali mwaka 2012 na 2013 nilipohoji kuhusu masuala muhimu ya nishati ambayo iwapo hatua muafaka zingechukuliwa kwa wakati zingeepusha nchi kulazimika kuongeza kwa mara nyingine gharama za umeme.

Naomba Rais Kikwete katika hotuba yake kwa taifa arejee hotuba nilizowasilisha kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) tarehe 27 Julai 2012 na 22 Mei 2013 na kutoa majibu ya kweli kwa wananchi katika masuala yote tuliyohoji kuhusu nishati.

Nakala ya Hotuba hizo zinapatikana katika tovuti ya bunge na kwenye mtandao wa http://mnyika.blogspot.com

( Hotuba ya Julai 2012- http://mnyika.blogspot.com/2012/07/hotuba-ya-kambi-rasmi-ya-upinzani.html na Hotuba ya Mei 2013- http://mnyika.blogspot.com/2013/05/hotuba-ya-msemaji-wa-kambi-rasmi-ya.html )

Udhaifu uliotajwa kwenye hotuba hizo na katika kauli za Waziri Muhongo na Naibu Waziri Simbachawene kwa nyakati mbalimbali unaweza kusababisha Matokeo Mabaya Sasa- Bad Results Now (BRN) badala ya Matokeo Makubwa (Big Results) kwenye sekta ya nishati.

Hivyo iwapo Rais kupitia hotuba yake kwa taifa mwishoni mwa mwezi huu wa Novemba 2013 hataeleza hatua alizochukua kuondoa udhaifu huo; nitaeleza hatua za ziada ambazo tutachukua katika kuisimamia Serikali kunusuru uchumi wa nchi na ustawi wa wananchi kutokana na ongezeko la bei ya umeme na mapungufu mengine kwenye sekta ya nishati.

Wenu katika uwakilishi wa wananchi,

John Mnyika (Mb)
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini

8 comments:

Unknown said...

Viongozi watanzania wana kauli chafu sana sasa kumwambia mwananchi eti kama bei ya umeme ataiona kubwa ni bora awashe kibatali au akae giza ndyo maana yake nini sasa! Viongozi mbadilike hizo sio kauli za kuwananchi wenu mnao waongoza

Unknown said...

Chini ya serikali ya ccm hakutakuwa na unafuu wa maisha kwa watanzania masikini. Kwakuwa viongozi wa ccm na serikali yao ni wapumbavu wameiingiza nchi katika mikataba ya kinyonyaji ili wajinufaishe kwa mikataba hiyo.

SWEETBERT RWABUKAMBARA said...

Wewe Mnyika wala hata usihangaike sana,usije kung'olewa meno na kucha bure! Tumeshazoea kunyonywa na Serikali yetu mpaka tumekuwa sugu! Majibu watayapata 2015 kuwa unyonge una mwisho!
Viongozi wanaongea ovyo,watu wanalala njaa wao wamekazania kupandisha bei za Luku. 2015 Magamba hamrudi,na tukishachukua nchi yetu,wale mafisadi wote tuwapeleke The Hague baadae wakaozee Guantanamo

Anonymous said...

Watananzania ni watu wenye asili ya uwoga tangu zamani. Hivyo kuna wakati mwingine wananyamaza kimya kungali kuna mapungufu. Leo hii inafika hatua muwajibikaji wako anakupandishia bei ya umeme harafu anakukejeli eti kama unashindwa kuimudu basi washa kibatari au ukae giza . (hajakamilika kiakili)

Anonymous said...

Simba amenisononesha sana, sio kauli ya kiungwaa mbali na kwamba alilozungumza halimponyi maskini zaidi ya kumuumiza. Taifa kua na kiongozi mwenye ulimi kama 'huu' ni sikitiko timilifu!!"

Nathan Junior said...

Mimi nachoomba serikali iwaangalie wananchi, jinsi maisha yalivyo magumu na bado inataka kuruhusu bei ya umeme ipande,Tusipokuwa makini tunaelekea pabaya.

Anonymous said...

Hawa watu wakiongea tuwe na clip au voice zao tunaweka wasije kusema Hiyo Kauli hawajaisema ni Kauli chafu sana na yenye zarau na inaonyesha hawajali watu. Ila na sie tuangalie ukweli wa umeme sio tu sababu umepandishwa tunawaka kuwe na sababu why umepanda ? ukipungua kwa sababu zipi? sio sababu umepanda kwasababu sie Chadema tuonyeshe wananchi sie usingepanda au kuwapandishia wananchi tuwe na sie Kama Chadema Pengine tungekuwa serikalini ungepanda na kwasababu zipi, ila sio kuweka Kauli chafu na za zarau. MZ

Unknown said...

Tumezoea aman sana ya kijinga tz,ingekuwa nchi zingine wananchi wangeandamana kumtaka wazir na naibu wake wajiuzulu... Mi naona ccm wanakusanya pesa kwa njia haram ya kuwakomoa watanzania kwa ajil ya uchaguz wa 2015..bei ya umeme kubwa sana