Sunday, July 20, 2014

CCM,Chadema wafanya vurugu ziara ya Makalla, Mnyika

Na Mary Geofrey 16th July 2014
Print
Ujumbe ulioongozana na Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla ukiwa ndani ya tenki la maji lililopo Chuo Kikuu cha Ardhi jana.
Wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) jana walifanya vurugu katika ziara ya Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla na Mbunge wa Jimbo la Ubungo (Chadema), John Mnyika ya kukagua miradi ya maji katika jimbo hilo.

Mbali na kukagua miradi ya maji, Makalla na Mnyika alitumia ziara hiyo pamoja na kuzungumza na wananchi juu ya mipango na mikakati ya serikali katika kuhakikisha upatikanaji wa maji jimboni humo.

Vurugu hizo zilianza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi Mavurunza, Kata ya Kimara, baada ya Mnyika kusimama na kutaka kuzungumza na wananchi kuhusu ujio wa Makalla pamoja na juhudi alizozifanya za kuhakikisha maji yanapatikana.

Baada ya Mnyika kusimama wafuasi wa CCM walianza kumshambulia kwa maneno ya kumtaka kuwa muda wake wa kukaa katika jimbo hilo umekwisha na kwamba, hana kazi nyingine anayofanya zaidi ya kutoa hoja bungeni na kuomba mwongozo wa Spika.


Hali hiyo iliwafanya wafuasi wa Chadema nao kujibu mapigo na kuanza kupiga kelele, huku wakishambuliana kwa maneno ya kashfa na kumfanya Mnyika kuanza kuelezea sababu za kuomba mwongozo wa Spika anapokuwa bungeni pamoja na kutoa hoja binafsi.

Majibu ya Mnyika hayakufua dafu, kwani wafuasi wa CCM waliendelea kumshambulia kwa maneno, hali ambayo ilimfanya aamue kumpa nafasi Makalla kuzungumza kile alichotaka kuwaambia wananchi.

“Mkutano huu ni kwa ajili ya kuzungumzia miradi ya maji pekee na namna tunavyoweza kulitatua kwa kushirikiana na serikali. Hivyo, sioni sababu ya wanachama wa CCM na Chadema kuufanya mkutano huu ni wa kisiasa. Naomba tutofautishe kati ya mkutano wa siasa na miradi ya maendeleo,” alisema Mnyika.

Kitendo cha Makalla kusimama na kutaka kuzungumza kilizidisha vurugu kwa wafuasi wa Chadema, huku wakimuasa Makalla kuwa hawataki hadithi na kwamba wanachotaka ni maji.

Kutokana na kushamiri kwa mipasho na vijembe vya wanasiasa hao, Makalla alifanya kazi ya ziada kutuliza fujo hizo kwa kuwataka wasiotaka kumsikiliza kwa madai kuwa anatoa hadithi waondoke na watu, ambao hawataacha kufanya vurugu, Jeshi la Polisi litaingilia kati kuwatuliza.

Kauli hiyo ilimfanya Mnyika kusimama na kuwatetea wanachama wake, huku akimshauri Makalla awaache, kwani hata yeye aliposimama wafuasi wa CCM walimpigia kelele bila kutishiwa kuwa watatulizwa na polisi.

Kutokana na majibizano hayo kushamiri huku viongozi hao wakiwa wamesimama na wafuasi nao wakishambuliana kwa kuashiria kutaka kupigana, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kinondoni, Salumu Madenge, na Diwani wa Chadema Kata ya Kimara, Pascal Manoti nao walishindwa kuzuia tofauti zao na kutaka kupigana.

Mzozo huo ulidumu kwa dakika takriban saba ulimfanya askari polisi aliyekuwa akiongoza msafara, kuzungumza jambo na Makalla, huku wafuasi nao wakiendelea kutulizwa.

Mara baada ya watu kutulizwa Makalla aliendelea kuzungumza na kueleza mikakati waliyonayo serikali na kuwataka viongozi wa ngazi zote kushirikiana na wananchi kumaliza tatizo la upotevu wa maji unaosababishwa na wizi pamoja na uchakavu wa miundombinu.

Chanzo: Gazeti la NIPASHE (http://www.ippmedia.com/frontend/?l=70018)

No comments: