Sunday, July 20, 2014

Waziri anusurika kichapo


Imeandikwa na Sharifa Marira

*Aondolewa chini ya ulinzi baada Chadema, CCM kuzusha vurugu

*Ni baada ya kudaiwa kuingiza u-CCM katika ziara ya kiserikali


KITENDO cha Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla, kumkaribisha Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kinondoni, Salum Madenge, kusalimia wananchi kwenye mkutano wa kiserikali, jana kilizua balaa na kulazimisha nguvu za dola kuingilia kati kumnusuru mteule huyo wa Rais.

Tafrani hiyo ilizuka jana mchana huko Goba, wakati Makalla, ambaye yupo kwenye ziara ya siku nne kukagua miradi ya maji jijini Dar es Salaam, alipokuwa katika mkutano wa mwisho wa hadhara kwa siku hiyo.

Kitendo cha kada wa CCM, Madenge, kuitwa jukwaani, hakikuwapendeza wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) waliokuwapo kwenye mkutano huo, kwa madai kuwa huo haukuwa mkutano wa kisiasa, ndipo wanachama hao walipokumbana na wenzao wa CCM na kuzusha vurugu kubwa zilizodumu kwa takriban dakika 30.

Wanachama wa CCM walikuwa wakishinikiza viongozi wa Chedema; wabunge John Mnyika (Ubungo) na Halima Mdee (Kawe) walikuwa jukwaani waondoke ili kuwe na usawa.

Vurugu na kelele za wafuasi wa vyama hivyo ziliposhamiri, polisi walilazimika kutumia nguvu kuwadhibiti na kuwazingira viongozi waliokuwa jukwaani kulinda usalama wao.

Baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya, mwandishi wa gazeti hili alishuhudia askari polisi wakimwondoa jukwaani Makalla chini ya ulinzi mkali na kumuingiza kwenye gari lake, huku viongozi wa Chadema wakiendelea kuzozana na polisi waliosalia.

Akizungumza na waandishi wa habari akiwa ndani ya gari baada ya kuondolewa jukwaani, Makalla alisema vuruguru hizo zilisababisha wananchi kukosa haki yao ya msingi ya kuzungumza na viongozi, kutokana na siasa kuingilia mkutano huo.

“Haya niliyataria, kwa hiyo siwezi kushangaa. Wakati wananchi wakifurahia ujio wa Waziri katika maeneo yao ili watoa malalamiko yao, hali imekuwa sivyo na siasa zimezidishwa, matokeo yake tumeshindwa kuzungumza na wananchi kuhusu mambo ya msingi,” alisema.

Alisema amekamilisha jukumu lake kwa kufika kwa wananchi kuwaeleza mipango ya Serikali katika kutatua kero ya maji, akidai kuwa tatizo mkutano wake uliingiliwa na wanasiasa wasio wakazi wa kata hiyo.

“Nakiri kuwa, mbali ya wananchi kujiunganishia maji kwa njia za wizi, lakini viongozi wa Dawasco, wanahusika kwa asilimia kubwa, kwa sababu haiwezekani watu wajiunganishie maji kwenye bomba kubwa, ni wazi kuna msaada wa watumishi wasio waaminifu. Baada ya ziara hii nitafumua uongozi wa Dawasco, ili tuweke watu tunaoamini tutafanya nao kazi kama tunavyotaka sisi,” alisisitiza Makalla, wakati akizungumza na mwandishi wa gazeti hili baadaye kwa njia ya simu.

Mbunge wa Ubungo, Mnyika, alisema vurugu zilianzishwa na wafuasi wa CCM ambao siyo wakazi wa eneo hilo kwa lengo la kumvuruga naibu waziri asizungumze na wananchi.

Hata hivyo, Mnyika, ambaye mwanzoni mwa ziara hizo alipishana kauli na Makalla walipokuwa Kata ya Mavurunza, alimtupia lawama Makalla kwa kuwaacha wananchi bila majibu waliyokuwa wakiyasubiri kwa muda mrefu.

“Kitendo cha Makalla kuondoka huku wanachama wake wakiendelea kufanya vurugu, ni wazi anakwepa kujibu maswali ya wananchi kuhusu masuala ya maji, hivyo sisi hatutaondoka hadi wanachama wetu wafahamu lini watapata maji ya uhakika,” alisema Mnyika wakati yeye na makada wengine wa Chadema wakiendelea na mkutano ‘usio rasmi’ na wanchama wao.

Awali, Makalla na Mnyika, ambaye ni Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, walitembelea maeneo ya Kigogo na kuwakamata wezi watano wa maji waliokuwa wakijiunganishia maji kinyemela.

Akizungumza baada ya kufanya ukaguzi katika nyumba hizo Makalla alisema vingozi na wananchi wana majukumu ya kuwatambua na kuwaripoti watu ambao wanahujumu uchumi wa nchi. Watu hao watano wamekuwa wakiikosesha DAWASCO Sh. bilioni 1.2 kwa mwezi.

Chanzo: Gazeti la RaiaTanzania (http://raiatanzania.co.tz/index.php/habari-tangulizi/983-waziri-anusurika-kichapo)

No comments: